Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Upelelezi kesi ya mtendaji mkuu Benki M haujakamilika

54645 Pic+benk+m

Tue, 30 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es salaam. Aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Benki M (Tanzania), Sanjeev Purushothaman anaendelea  kusota rumande kwa siku 54, sasa kutokana na upelelezi wa kesi inayomkabili kutokukamilika.

Purushothaman (63), anakabiliwa na mashtaka 29 yakiwemo ya kutakatisha fedha, kughushi na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kiasi cha Sh 6 bilioni katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Mshtakiwa huyo alifikishwa kwa mara ya kwanza Kisutu, Machi 7, 2019 akikabiliwa na mashtaka hayo katika kesi ya jinai namba 73/2019.

Wakili wa Serikali, Ashura Mzava amedai hayo leo Aprili 29, 2019 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, wakati shauri hilo lilipokuja kwa ajili ya kutajwa.

"Upelelezi wa kesi hii bado haujakamilika, hivyo tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa," amesema Mzava.

Baada ya kueleza hayo, Hakimu Shaidi ameutaka upande wa mashtaka kuhakikisha kuwa wanakamilisha haraka upelelezi ili mshtakiwa ajue hatima yake.

Hakimu Shaidi ameahirisha kesi hiyo hadi Mei 10, 2019 itakapotajwa na mshtakiwa amerudishwa rumande kutokana na mashtaka ya kutakatisha fedha yanayomkabili kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria.

Katika mashtaka hayo 29, 13 ni ya kutakatisha fedha, 14 ni ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, shtaka moja ni la kughushi na moja ni la kuwasilisha nyaraka za uongo kwa mdhibiti wa hesabu za ndani wa Benki M.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, mshtakiwa anadaiwa kuwa  Machi 10, 2010, katika ofisi za Benki M (Tanzania) Limited, aliwasilisha nyaraka ya uongo na barua pepe , akionyesha kuwa Dola15,000 za Marekani, zilipwe kwake kama gharama za kuendeleza biashara wakati akijua ni uongo.

Shtaka la pili, ambalo ni kuwasilisha nyaraka ya uongo, Purushothaman, anadaiwa Machi 8, 2010 katika ofisi hizo, kwa njia ya udanganyifu aliwasilisha nyaraka ya uongo kwa Yahaya Mbaka, ambaye ni  mdhibiti wa hesabu za ndani wa Benki M kwa kumtumia barua pepe akiomba fedha hizo kwa ajili ya kuendeleza biashara ya benki.

Katika shtaka la tatu hadi la 16, mshtakiwa anadaiwa kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, kiasi cha Sh 6,039,103,579, akidai kuwa ni kwa ajili ya kuendeleza biashara ya benki hiyo wakati akijua kuwa ni uongo.

Miongoni mwa mashtaka ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu ni kwamba, mshtakiwa anadaiwa  kati ya Januari 8, 2015 na Juni 30, 2015 katika Ofisi za Benki M, alijipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kiasi cha Sh 1, 107,267,260, akidai kuwa fedha hizo ni kwa ajili ya kuendeleza  biashara  ya benki hiyo wakati akijua kuwa ni uongo.



Chanzo: mwananchi.co.tz