Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Upelelezi kesi ya mawakala ATCL bado kitendawili

Wed, 9 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Upande wa utetezi katika kesi inayowakabili mawakala 10 wa Shirika  la Ndege Tanzania (ATCL) imeutaka upande wa mashtaka kuharakisha upelelezi katika kesi hiyo.

Mawakala hao wanakabiliwa na mashtaka matatu ikiwemo kujipatia Sh10,874,280 kwa njia ya udanganyifu kwa lengo la kuwakatia watu tiketi za ndege za shirika hilo

Washtakiwa katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 97/2018 ni Fabian Ishengoma (34), Adamu Kamara (27), Marlon Masubo (29), Alexander Malongo (24), Tunu Kiluvya (32), Jobu Mkumbwa (30), Mohamed Issa (38), Godfrey Mgomela, Absalom Nyusi na Janeth Lubega(24).

Hatua hiyo inatokana na upande wa mashtaka kuieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika.

Leo Jumatatu Januari 7, 2019 wakili wa Serikali, Ester Martine amedai mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mkazi ,Janeth Mtega kuwa shauri hilo lilikuja kwa ajili ya kutajwa hivyo kuiomba Mahakama ipange tarehe nyingine.

Baada ya maelezo hayo wakili wa utetezi, Augustine Kulwa ameutaka upande wa mashtaka kuharakisha upelelezi ili washtakiwa wapate haki yao.

"Hatuna pingamizi na upande wa mashtaka rai yetu tunasisitiza upelelezi ufanyiwe kazi kwa haraka zaidi ili washtakiwa wapate haki yao kwa wakati," amedai Kulwa.

Hakimu Mtega ameahirisha kesi hiyo hadi Januari 17, 2019 itakapotajwa tena.

Katika shtaka jingine washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kati ya Machi10 na Oktoba 9, 2018 wakiwa katika mkoa wa Dar es Salaam na  Mwanza walitumia njia ya udanganyifu kujipatia kiasi cha Sh10,874,280 kwa lengo la kuwakatia watu tiketi za ndege la shirika hilo.

Wanadaiwa kuwa katika shtaka la tatu la utakatishaji wa fedha washtakiwa wote kwa pamoja kati ya Machi10 na Oktoba 9, 2018 wakiwa katika mkoa wa Dar es Salaam na Mwanza walijipatia Sh10,874,280  mali ya ATCL huku wakijua ni kosa kisheria.



Chanzo: mwananchi.co.tz