Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Upelelezi kesi ya mauaji inayomkabili askari JWTZ wakamilika

Tue, 2 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dara es Salaam. Upelelezi wa kesi ya mauaji inayomkabili, mwanajeshi wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Ramadhani Mlaku (28), umekamilika.

Mlaku ambaye ni mwanajeshi kutoka kambi ya Makongo, anadaiwa kumuua  mwanajeshi mwenzake kwa kumpiga risasi.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Patrick Mwita, ameeleza hayo, leo Jumatatu April mosi, 2019, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Thomas Simba.

"Kesi hii ilikuja kwa ajili ya kutajwa, naomba niiambie mahakama yako kuwa upelelezi wa shauri hili umekamilika," amedai Mwita.

Mwita amedai kwa sasa jalada halisi la kesi hiyo limepelekwa ofisi ya upelelezi mkoa wa Ilala (RCO) kwa ajili ya kuandaliwa taarifa.

"Jalada hilo baada ya kutoka kwa RCO litapelekwa ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), hivyo tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa," amedai Mwita.

Awali, kabla ya kesi hiyo kuahirishwa, mshtakiwa ameomba apatiwe dhamana kwa madai kuwa hata yeye alipigwa risasi mbili mguuni na hajui aliyempiga.

"Mheshiwa hakimu na mimi nilishambuliwa kwa risasi mbili mguuni na aliyenipiga risasi hizo simjui, hivyo kutokana na upelelezi wa kesi hii kukamilika naomba na mimi nipatiwe dhamana,” amesema.

Hakimu Simba amesema kuwa kesi inayomkabili Mlaku ni kesi ya mauaji na haina dhamana hivyo kama ana malalamiko ayawasilishe kwa mkurugenzi wa mashtaka nchini kupitia mkuu wa gereza husika.

"Kesi inayokukabili ni kesi ya mauaji na haina dhamana, hivyo basi kama una malalamiko andika barua uipeleke kwa mkuu wa gereza lako ambaye atakusaidia kuipeleka barua hiyo kwa DPP," alisema Hakimu Simba.

 

Hakimu Simba baada ya kueleza hayo, ameahirisha kesi hiyo hadi April 15, 2019 itakapotajwa na kupangiwa tarehe ya kumsomea mshtakiwa maelezo ya mashahidi na vielelezo (Committal Proceedings).

Mlaku alifikishwa Mahakama ya Kisutu kwa mara ya kwanza, Machi 14, 2018 kujibu shtaka hilo.

Katika kesi ya msingi,  mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo, Oktoba 30, 2017, makao makuu ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Upanga jiji Dar es Salaa.

Mlaku  akiwa makao makuu ya jeshi hilo, anadaiwa kumuua mwanajeshi mwenzake, mwenye namba MT 79512, Sajenti Saimon Munyama kwa kumpiga risasi.

 

 



Chanzo: mwananchi.co.tz