Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Upelelezi kesi ya anayedaiwa kumuua mkewe, kumchoma moto haujakamilika

MAUAJI MKEWE Upelelezi kesi ya anayedaiwa kumuua mkewe, kumchoma moto haujakamilika

Thu, 1 Dec 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeelezwa kuwa upelelezi katika kesi ya mauaji inayomkabili mfanyabiashara, Hamisi Luongo maarufu kama Meshack (41) bado haujakamilika.

Luongo anadaiwa kumuua Naomi Marijani ambaye ni mkewe kisha kumchoma moto kwa kutumia magunia mawili ya mkaa na baadae kuchukua majivu yake na kwenda kuyafukia shambani.

Wakili wa Serikali, Adolf Verandumi, ameieleza mahakama hiyo leo Alhamisi Desemba Mosi, 2022 wakati shauri hilo lilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

Verandumi ametoa maelezo hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Rhoda Ngimilanga, anayesikiliza shauri hilo.

" Kesi hii imekuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wa shauri hili bado unaendelea hivyo tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa" amedai Verandumi.

Hakimu Ngimilanga baada ya kusikiliza maeneo ya upande wa mashtaka, ameahirisha kesi hiyo hadi Januari 15, 2023 itakapoitwa kwa ajili ya kutajwa.

Hata hivyo leo, mshtakiwa huyo hakuweza kuletwa mahakamani hapo na badala yake kesi hiyo imeahirishwa kwa njia ya video Conference akiwa gerezani.

Kwa kawaida kesi nyingi ambazo zipo katika hatua ya kutajwa zinazowakabili washtakiwa ambao makosa yao hayana dhamana kwa mujibu wa sheria ikiwemo kesi ya mauaji, unyang'anyi wa kutumia silaha washtakiwa huwa hawapelekwi mahakamani na badala yake kesi hizo huahirishwa kwa njia ya video conference.

Utaratibu huo ulikuwa unatumika kwa kiwango kidogo hapo nyuma lakini sasa unaendelea kufanyika baada ya ugonjwa wa Uviko 19.

Hata hivyo, upelelezi wa kesi hizo, unapokamilika na kuanza kusikilizwa, washtakiwa hao hupelekwa mahakamani kwa ajili ya usikilizwaji.

Katika kesi ya msingi, mshtakiwa anakabiliwa na kesi ya mauaji namba 5/2022.

Anadaiwa kutenda kosa hilo, Mei 15, 2019 katika eneo la Gezaulole, wilaya ya Kigamboni, ambapo alimuua mkewe aitwaye Naomi Marijani.

Itakumbukwa kuwa Oktoba 24, 2022 Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) alimfutia shtaka mshtakiwa huyo na kisha kufungua kesi nyingine yenye shtaka hilo hilo.

Huo ni utaratibu wa kawaida kwa upande wa mashtaka kufuta kesi na kumfungulia nyingine iwapo watabaini kuna kasoro za kisheria katika kesi hiyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live