Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Upelelezi kesi ya Yusufali, wenzake wakamilika, kusomewa maelezo Februari 21

Tue, 19 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imepanga Februari 21, 2019 kumsomea maelezo ya mashahidi na vielelezo, mfanyabiashara maarufu nchini, Mohamed Yusufali na wenzake wawili.

Mbali na Yusufali, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi Namba 8/2019 ni Arifal Paliwalla na Meneja wa Benki ya I&M tawi la  Kariakoo, Sameer Khan.

Yusufali maarufu kwa majina ya Choma, Mohamedali au Mohamed Jamalee na wenzake, wanakabiliwa na mashtaka 506 yakiwamo ya kutakatisha fedha, kukwepa kodi na kuisababishia Serikali hasara ya Sh24 bilioni.

Uamuzi huo umetolewa leo Jumatatu Februari 18, 2019  na Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi baada ya hakimu anayesikiliza shauri hilo kuwa na kazi nyingine.

Awali, Wakili kutoka Takukuru, Leonard Swai alidai mbele ya Hakimu Shaidi kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kutajwa na hakimu anayesikiliza shauri hilo, Augustine Rwizile ana kazi nyingine, hivyo wanaomba ahirisho fupi kwa ajili ya kupanga tarehe ya kuwasomea maelezo ya mashahidi na vielelezo.

“Washtakiwa wote wapo mbele ya mahakama yako na kesi ilikuja kwa ajili ya kutajwa na kupangiwa tarehe kwa ajili ya kuwasomea maelezo ya Mashahidi na vielelezo, washtakiwa hawa,” amedai Swai na kuongeza:

“Lakini hakimu anayesikiliza shauri hili ana kazi nyingine hivyo, tunaomba tarehe fupi kwa ajili ya kupangiwa tarehe ya kuwasomea maelezo  ya washtakiwa,” amedai Swai.

Swai amedai kuwa tayari Takukuru imeshafungua taarifa ya kesi hiyo Mahakama Kuu Kitengo cha Rushwa na Uhujumu Uchumi maarufu Mahakama ya Mafisadi.

Swai baada ya kueleza hayo, Wakili wa utetezi, Jamhuri Johnson akisaidiaa na Hassan Kiangio, walikubaliana na hoja za upande wa mashtaka na kuiomba mahakama hiyo ipange tarehe fupi.

Hakimu Shaidi ameahirisha kesi hiyo hadi Februari 21, 2019 na washtakiwa wamerudishwa mahabusu kutokana na mashtaka yanayowakabili kutokuwa na dhamana.

Hatua ya kuwasomea maelezo ya mashahidi na vielelezo, washtakiwa hao inatokana na upelelezi wa kesi hiyo kukamilika.

Hata hivyo, washtakiwa hao wakishasomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo, wataulizwa kama wana maoni yoyote na kama hawana, kesi hiyo itahamishwa kutoka katika Mahakama ya Kisutu na kwenda  katika mahakama ya Mafisadi kwa ajili ya kuanza kusikilizwa rasmi.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, katika mashtaka hayo 506; mashtaka 64 ni ya utakatishaji fedha; Mashtaka 264 ni ya kughushi; mashtaka 72 ni ya kuwasilisha nyaraka za uongo Mamlaka ya Mapato nchini(TRA).

Mashtaka 103 ni ya kutoa taarifa za uongo; shtaka moja la  kuisababishia Serikali hasara ya Sh24bilioni, shtaka moja la kukwepa kodi na shtaka lingine ni kupanga nyama za kukwepa kodi.

Hata hivyo, Yusufali  pia anakabiliwa na kesi nyingine ya uhujumu uchumi namba 1/2019, yenye mashtaka 39 likiwemo la kusababishia Serikali hasara ya Sh 2bilioni, katika Mahakama ya Kisutu.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanadaiwa kukwepa kodi, kati ya Januari 2008 na Januari 2016 katika jijini la Dar Es Salaam.

Pia inadaiwa kati ya Januari 2008 hadi 2016, katika jiji la Dar Es Salaam, Yusufali akiwa kama  Mkurugenzi wa Kampuni ya Farm Plant Limited, ambayo imesajiliwa kulipa Kodi ya ongezeko la  thamani(Vat) kwa nia ya kukwepa kodi, aliwasilisha makadilio ya kodi ya uongo kwa Kamishna wa Mamlaka ya Mapato nchini(TRA) na hivyo kukwepa kulipa kodi kiasi cha Sh 24, 303, 777, 426( sawa na Sh 24bilioni).

Katika shtaka la kuisababishia Serikali  hasara inayomkabili mshtakiwa Yusufali na Paliwalla, inadaiwa kuwa kati ya Januari 2008 na Januari 2016 katika jiji la  Dar Es Salaam, aliwasilisha nyaraka za uongo, Mamlaka ya Mapato nchini( TRA), kitendo ambacho kiliisababishia Serikali hasara ya Sh 24 bilioni



Chanzo: mwananchi.co.tz