Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Upelelezi kesi ya Maimu wakamilika

60156 Pic+maimu

Thu, 30 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Upelelezi  wa kesi ya kuisababishia Serikali hasara ya Sh1.175 bilioni inayomkabili aliyekuwa mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Dickson Maimu na wenzake watano, umekamilika.

Maimu na wenzake wanakabiliwa na mashtaka 100 katika kesi ya uhujumu uchumi namba 7/2019 iliyopo Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Wakili wa Serikali, Wankyo Simon ameieleza mahakama hiyo leo Jumanne Mei 28, 2019 wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa.

Simon amedai  mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kuwa upelelezi wa shauri hilo umekamilika.

"Upelelezi wa kesi hii umekamilika na upande wa mashtaka tayari tumewasilisha taarifa muhimu Mahakama Kuu,” amedai Simon.

Katika hatua nyingine,  Maimu, Astery Ndege na George Ntalima wameshindwa  kufika mahakamani hapo kwa kile kilichoelezwa kuwa ni wagonjwa.

Pia Soma

Wakili Simon  amedai  kuwa amepewa taarifa na askari magereza kuwa washtakiwa hao ni wagonjwa na hivyo wameshindwa kufika mahakamani kusikiliza kesi yao.

Kutokana na hali hiyo,  Simon ameiomba mahakama hiyo ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Simba baada ya kusikiliza maelezo hayo, aliahirisha kesi hiyo hadi Juni 11, 2019 itakapotajwa.

Mbali na Maimu, washtakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo  ni meneja Biashara wa Nida, Aveln Momburi;  mkurugenzi wa kampuni ya Aste Insurance Brokers,  Astery Ndege; ofisa usafirishaji, George Ntalima; mkurugenzi wa sheria, Sabina Raymond na Xavery Kayombo.

Kati ya mashtaka hayo 100 yanayowakabili washtakiwa hao, 24 ni ya kutakatisha fedha,  23 ya kughushi,  43 ya kutumia nyaraka kwa lengo la  kumdanganya mwajiri, mashtaka matano ni ya  kuisababishia hasara Mamlaka hiyo.

Pia, mashtaka mawili ya kula njama ya kulaghai, mashtaka mawili ya matumizi mabaya ya madaraka, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na matumizi mabaya ya madaraka lipo moja ambalo linamkabili  Maimu na Sabina.

Hata hivyo, katika mashtaka hayo, mshtakiwa  Momburi na Raymond wao hawana mashtaka ya utakatishaji fedha,  hivyo wako nje kwa dhamana baada ya kwenda kuomba dhamana yao Mahakama Kuu.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, kati ya Julai 19, 2011 na Agosti 31,2015, washtakiwa wakiwa maeneo tofauti katika Jiji la Dar es Salaam walikula njama ya kufanya udanganyifu wa Sh1.175bilioni dhidi ya Nida.

Maimu anatuhumiwa kutakatisha fedha haramu Sh1,175,785,600.93  kati Julai 19, 2011 na Agosti 31, 2015  kwa kujihusisha moja kwa moja kuhamisha fedha hizo huku akijua ni zao la kughushi.

Pia, Maimu na Raymond wanatuhumiwa Novemba 7, 2011 wakiwa Makao Makuu ya Nida, Kinondoni walitumia madaraka yao vibaya na kusababisha kampuni ya Gotham International Ltd kupata faida ya Sh.899,935,494.

Novemba 12, 2011 na Mei 12, 2015, Maimu na Momburi wakiwa makao makuu ya Nida, Kinondoni, walishindwa kusimamia ujenzi wa jengo lililopo plonti namba 39A na hivyo, kuisababishia  mamlaka hiyo hasara ya Sh 402,210,885.02.

Chanzo: mwananchi.co.tz