Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Upelelezi kesi ya Maimu haujakamilika

17957 Pic+maimuTanzaniaWeb

Wed, 19 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam.  Upelelezi wa kesi  ya uhujumu uchumi na kusababisha hasara ya Sh1.16 bilioni inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Dickson Maimu na wenzake katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu bado haujakamilika.

Kesi hiyo ilifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Agosti18, 2016, upelelezi wake bado haujakamilika.

Wakili wa Serikali  Patrick Mwita leo Septemba 18, 2018, amedai mbele ya  Hakimu Mkazi Mkuu, Augustina Mmbando wakati kesi hiyo ilipotajwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri anayeisikiliza kesi hiyo yupo likizo.

Baada ya kusikiliza maelezo hayo, Hakimu Mmbando ameiahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 16, 2018 kwa ajili ya kutajwa.

Mbali ya Maimu, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Meneja Biashara wa Nida Avelin Momburi na Mkurugenzi wa Tehama, Joseph Makani.

Wengine ni Kaimu Mhasibu Mkuu wa Nida,  Benjamin Mwakatumbula, Mkurugenzi wa Kampuni ya Aste Insurance Brokers,  Astery Ndege, Ofisa Usafirishaji,  George Ntalima, Mkurugenzi wa Sheria, Sabina Raymond na Xavery Kayombo.

Katika kesi hiyo, washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka ya kutumia madaraka vibaya, kula njama, kutumia nyaraka za uongo kumdanganya mwajiri na kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh1,169,352,931.

Inadaiwa shtaka la kwanza Maimu na Mwakatumbula kati ya Januari 15 hadi 19,  mwaka 2010 katika makao makuu ya Nida  wilayani Kinondoni Mkoa wa Dar es Salaam, wakiwa watumishi wa umma kwa nafasi walizokuwa nazo  walitumia madaraka  vibaya.

Wanadaiwa waliidhinisha malipo kwa Gotham International Limited (GIL) ya Dola za Marekani 2,700,00 bila ya kutumia viwango vya kubadilisha fedha za kigeni vilivyowekwa na  Benki Kuu ya Tanzania, kinyume na kifungu 19.3 cha mkataba kati ya Nida na GIL, hivyo kuifanya GIL kupata faida ya Sh 3,969,000.

Maimu na Mwakatumbula katika shtaka jingine wanadaiwa kati ya Juni 3 na 5, 2013 katika makao makuu hayo walitumia madaraka vibaya kwa kuidhinisha malipo kwa GIL ya Dola za Marekani milioni 1.8, bila ya kuzingatia viwango vya kubadilisha fedha, hivyo kuifanya GIL kupata faida ya Sh 106,346,000.

Washtakiwa hao wawili wanadaiwa Juni 20, 2014 katika makao makuu hayo, waliidhinisha tena malipo ya Dola za Marekani 675,000 kwa GIL bila ya kuzingatia viwango vya kubadilisha fedha, hivyo kuifanya kampuni hiyo kupata faida ya Sh 42,471,000.

Maimu na Mwakatumbula wanadaiwa kutumia madaraka yao vibaya kwa kupitisha malipo mengine ya Sh6 milioni  kwa GIL bila ya kupiga  hesabu kwa kutumia viwango vya kubadilishia fedha hivyo kuifanya kampuni hiyo kupata faida ya Sh 14, 661,676.76.

Maimu na Mwakatumbula wanadaiwa kati ya Januari 15, 2010 na Mei 16, 2015 katika makao makuu hayo ya NIDA kwa kuidhinisha malipo kwa GIL ya Dola za Marekani bila ya kuzingatia viwango vya kubadilisha fedha za kigeni waliisababishia NIDA kupata hasara ya Sh 167,445,676.76.

Chanzo: mwananchi.co.tz