Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Upelelezi kesi ya MC Luvanda wasubiri taarifa za Brela

32160 MRLUVANDAPI Anthony Luvanda ‘MC Luvanda’

Tue, 18 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Upande wa mashtaka katika kesi inayomkabili mshereheshaji maarufu nchini Tanzania, Anthony Luvanda ‘MC Luvanda’ umeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa wanasubiri vielelezo kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) ili kukamilisha upelelezi.

Luvanda anakabiliwa na mashtaka matatu, likiwemo la kutoa maudhui mtandaoni bila ya kuwa na kibali cha Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Wakili wa Serikali mwandamizi, Nassoro Katuga ameeleza hayo leo Jumanne Desemba 18, 2018 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Huruma Shaidi, wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa.

"Tulipeleka barua Brela ili watusaidie kutupatia vielelezo hivyo, lakini bado hawajatujibu. Tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa na kuangalia kama tutakuwa tumepata vielelezo hivyo" alidai Katuga

Katuga baada ya kueleza hayo, wakili wa utetezi, Shirinde Swed, amedai kuwa hana pingamizi juu ya hilo.

Hakimu Shaidi baada ya kusikiliza hoja za pande zote ameahirisha kesi hiyo hadi Januari 21, 2019 itakapotajwa na mshtakiwa yupo nje kwa dhamana.

Mbali na Luvanda mshtakiwa mwingine katika kesi hiyo ni kampuni ya Luvanda ya Home of Company Limited.

MC Luvanda pamoja na kampuni yake wanakabiliwa na mashtaka matatu likiwemo la kutumia kikoa ambacho hakijisajiliwa Tanzania.

Inadaiwa kuwa kati ya Februari 24 na Septemba 2018 katika Jiji la Dar es Salaam, mshtakiwa huyo alianzisha na kutumia mtandao wa www.mcluvanda.com ambao haukuwa na kikoa cha .tz.

Pia inadaiwa kuwa katika kipindi hicho mshtakiwa alianzisha na kutumia mtandao huo ambao haukuwa na kikoa cha .tz.

Pia ,mshtakiwa huyo anadaiwa kuwa alitoa huduma ya online bila ya kuwa na kibali.

Katika shtaka la tatu, Mc Luvanda anadaiwa kuwa katika kipindi hicho alitoa huduma hiyo kupitia online TV ijulikanayo kama MC Luvanda bila kuwa na kibali cha TCRA.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz