Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Upelelezi kesi walioghushi saini ya Makamba haujakamilika

Thu, 14 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es salaam. Upelelezi wa kesi ya  kughushi saini ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Muungano na Mazingira), January Makamba inayowakabili wafanyakazi sita wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) bado haujakamilika.

Mbali na kughushi washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka mengine ikiwemo kula njama, kughushi, kuwasilisha nyaraka za uongo, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kusababisha hasara ya Sh160milioni.

Mwanasheria wa Serikali, Jenipher Masue leo Jumatano Februari 13, 2019 mbele ya hakimu mkazi mwandamizi, Augustina Mmbando  ameeleza upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilia.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni ofisa mazingira NEMC, Deusdith Katwale;  mtaalamu wa Tehama, Luciana Lawi; ofisa mazingira Magori Wambura; katibu muhtasi, Edna Lutanjuka; msaidizi wa  wa ofisa Mwaruka Mwaruka na ofisa mazingira baraza hilo, Lilian Laizer.

Wafanyakazi hao walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu  Oktoba  31, 2018 na kusomewa mashtaka sita ya uhujumu uchumi likiwamo la kughushi saini ya  Makamba katika vyeti vya tathmini ya uharibifu wa mazingira.

Katika kesi hiyo mshtakiwa namba moja ambaye ni Wambura anaendelea kusota rumande baada ya kukosa dhamana na washtakiwa wengine watano wako nje kwa dhamana.

Hakimu Mmbando ameahirisha kesi hiyo hadi Februari 27, 2019 itakapotajwa.

Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka sita ikiwemo kugushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kulisababishia baraza hilo hasara ya Sh160milioni.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz