Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Upelelezi kesi mhasibu bodi ya pamba mbioni kukamilika

Thu, 20 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Upelelezi wa kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili mhasibu mkuu wa Bodi ya Pamba Tanzania (TCB), Simon Maganga upo katika hatua za mwisho kukamilika.

Maganga anayetetewa na wakili Othman Katuli, anakabiliwa na mashtaka sita katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, likiwemo la kuisababishia Serikali hasara ya ShSh55.6 milioni.

Wakili wa Takukuru, Nikson Shayo ameeleza hayo leo Alhamisi Desemba 20, 2018 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Thomas Simba wakati shauri hilo likitajwa.

“Kesi imekuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wa shauri upo katika hatua za mwisho kukamilika. Tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa” amedai Shayo.

Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi  Januari 23, 2019 itakapotajwa na mshtakiwa yupo nje kwa dhamana.

Maganga alifikishwa kwa mara ya kwanza Kisutu Julai 11, 2018 kujibu mashtaka hayo katika kesi ya uhujumu uchumi namba 49/2018.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Maganga anadaiwa Januari 2009, alimdanganya mwajiri wake, kwa kutumia vocha za kuwasilisha mbegu za pamba katika msimu wa mwaka 2009/10 akijaribu kuonyesha Kampuni ya Afrisian Ginning Limited ilinunua mbegu za pamba kilo 25.1milioni.

Pia, mshtakiwa alifanya hivyo kwa kampuni ya Nyanza Cooperative Limited na kuonyesha ilinunua kilo 3.7milioni za mbegu za pamba wakati akijua siyo kweli.

Katika shtaka jingine, mshtakiwa anadaiwa kutumia vocha za kuwasilisha mbegu za pamba msimu wa mwaka 2009/10 akijaribu kuonyesha kampuni ya S&C Ginning Limited, ilinunua kilo 17.1milioni za mbegu za pamba.

Maganga akiwa kama Mhasibu wa TCB, alifanya ufujaji na ubadhirifu wa Sh55.6 milioni mali ya TCB.

 

 



Chanzo: mwananchi.co.tz