Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Upatu nusura uwapeleke jela, faini yawaokoa

36462 Pic+upatu Upatu nusura uwapeleke jela, faini yawaokoa

Sun, 13 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakurugenzi wawili wa kampuni inayodaiwa kuendesha biashara ya upatu ya Rifaro Afrika Ltd wamelipa faini ya Sh 102 milioni kila mmoja, baada ya kukiri makosa yao hivyo kuepuka kifungo cha miaka saba jela kila mmoja.

Washitakiwa hao ni Jones Moshi (42) mkazi wa Mbezi Beach jijini Dar es Salaam na raia wa Kenya, James Gathonjia (35) ambao walikuwa wanakabiliwa na mashtaka mawili.

Mashtaka hayo ni kuendesha biashara ya upatu kwa kukusanya fedha na kutakatisha fedha kiasi cha Sh1 bilioni.

Pia Mahakama imetaifisha Sh.145 milioni ambazo ni fedha zilizokuwa katika akaunti ya washitakiwa hao.

Hukumu hiyo ilitolewa juzi na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Wilbard Mashauri baada ya washtakiwa hao kukiri mashtaka yao wakati shauri hilo lilipofikishwa mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa.

Awali washitakiwa hao walikuwa wakikabiliwa na mashitaka matatu katika kesi ya uhujumu uchumi namba 87/2018, lakini upande wa mashitaka ulibadilisha hati ya mashitaka kwa kuliondoa shitaka la uhujumu uchumi.

Baada ya kuondoa shitaka hilo upande wa mashitaka ukiongozwa na wakili wa Serikali mwandamizi, Shadrack Kimaro akisaidiana na Ester Martine na Neema Mbwana uliwasomewa upya mashtaka mawili katika kesi ya jinai namba 11/2019, ambayo ni kuendesha biashara ya upatu na utakatishaji fedha Sh1 bilioni.

Katika hukumu hiyo, hakimu Mashauri aliamuru washtakiwa hao kwenda jela miaka saba kila mmoja au kulipa faini ya Sh102 milioni kila mmoja ambapo walilipa faini hiyo na kuepuka kifungo cha gerezani.



Chanzo: mwananchi.co.tz