Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Upande wa mashtaka kesi ya Mwanyika waomba msaada wa upelelezi nje ya nchi

39486 Kesipic Upande wa mashtaka kesi ya Mwanyika waomba msaada wa upelelezi nje ya nchi

Mon, 4 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Upande wa mashtaka katika kesi inayomkabili aliyekuwa Rais wa kampuni ya Acacia, Deogratias Mwanyika wameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa wameomba msaada wa upelelezi kutoka nje ya Tanzania.

Wakili wa Serikali, Wankyo Saimon ameeleza hayo leo Februari Mosi, 2019 mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Kelvin Mhina wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa.

Wankyo ameeleza hayo baada ya wakili wa utetezi, Gasper Nyika kudai kuwa walishaomba kupatiwa majibu ya hatua gani ya upelelezi wamefikia na ni msaada gani waliouomba nje ya nchi.

"Tunachotaka kujua ni kama hatua zimeshachukuliwa lakini ni hatua gani za upelelezi mmeshafikia hadi sasa,” amedai Nyika.

Wankyo amedai hatua zimeshachukuliwa lakini majibu hawajayapata hivyo wanaomba tarehe nyingine ya kutajwa ili kujua ni hatua gani  walizofikia.

Baada ya kuelezwa hayo, Hakimu Mhina ameahirisha kesi hiyo hadi Februari 15, mwaka huu.

Mbali na Mwanyika washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni meneja mahusiano wa mgodi wa Bulyanhulu, Alex Lugendo; mkurugenzi mtendaji wa Pangea, North Mara na Bulyanhuku Assa Mwaipopo; kampuni ya mgodi ya Pangea, North Mara, Exploration na Bulyanhulu.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 39, yakiwemo ya utakatishaji na kukwepa kodi zaidi ya Dola  112 milioni.

Washtakiwa hao pia wanakabiliwa na mashtaka matatu ya kula njama, saba ya kughushi, 17 ya utakatishaji fedha, kuwasilisha nyaraka  za uongo kwa TRA shtaka moja, kuongoza uhalifu wa kupangwa, mashtaka nane ya kukwepa kodi na moja la kutoa rushwa.

Washtakiwa wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Aprili 11, 2008 na Juni 30,2007 katika sehemu tofauti jijini Dar es Salaam, Kahama mkoani Shinyanga, Tarime Mara, Biharamulo Kagera, maeneo ambayo yapo katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Maeneo mengine ambayo washtakiwa wanadaiwa kutenda makosa hayo ni katika mji wa Johannesburg, Afrika Kusini, Toronto Canada na Uingereza.

Aidha washtakiwa Mwanyika  na Lugendo wanadaiwa kutoa msaada katika kusimamia mkakati wa kihalifu kwa nia ya kupata faida.

Washtakiwa hao wanadaiwa kutoa tamko la uongo kwa kamishna jenerali wa TRA huko Biharamulo kwa nia ya kukwepa kodi ya Dola 9.3 milioni ambayo ni kodi iliyopaswa kulipwa kwa TRA.

Washtakiwa Mwanyika na Lugendo wanadaiwa kuwa kati ya Desemba 2009 na Desemba 31 2018 katika maeneo tofauti ndani na nje ya Tanzania kwa pamoja na wengine ambao hawapo mahakamani, walisaidia mgodi wa North Mara kuhamisha fedha Dola 374,243,943.45  za Marekani huku wakijua kuwa fedha hizo ni zao la makosa ya kughushi na kukwepa kodi.

Pia,  washtakiwa wanadaiwa kati ya Novemba 2,  2012 na Novemba 27, 2015 huko Shinyanga walitoa rushwa ya Sh718,520,001.76 kwa Hussein Kashindye ambaye  ni mkuu wa upelelezi makosa ya jinai mkoa wa Shinyanga kwa lengo la kumshawishi ili aweze kuachana na uchunguzi wa makosa ya jinai yaliyokuwa yametendwa na Mgodi wa Bulyanhulu.

Katika shtaka la kughushi washtakiwa hao wakiwa na nia ya ulaghai walighushi mkataba wa mkopo wakitaka kuonyesha kwamba Aprili 30, 2014 Kampuni ya Pangea Limited ilikubali kukopa Dola 90,000,000 ikiwa na riba Kutoka Benki ya Kimataifa ya Barrick huku wakijua kuwa si kweli.

Katika shtaka la kutoa nyaraka ya uongo, mshtakiwa Mwanyika anadaiwa Aprili 30, 2018 huko BOT wilaya ya Ilala, kwa makusudi aliwasilisha nyaraka ya uongo ya mkopo baina ya kampuni mgodi wa Bulyanhulu na Barrick International Bank Corp kwa madhumuni ya kuonyesha kuwa, kati ya Juni 2001 na Desemba 13, 2007 Bulyanhulu walijipatia mkopo usio na faida wa Dola 416,100,000 kutoka Barrick.

Soma Zaidi: Mwanyika wa Acacia, wenzake waendelea kusota rumande



Chanzo: mwananchi.co.tz