Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

‘Unatumikisha watoto wetu… Hapana, mnanipakazia tu’

7df396c3ba8d172dda74e5734c4d8760 ‘Unatumikisha watoto wetu… Hapana, mnanipakazia tu’

Mon, 17 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

JOHN Benson, Mkazi wa Mtaa wa Nyamatare, Musoma mjini, ni mfanyabiashara wa vyuma chakavu mwenye mafanikio katika biashara hiyo.

Katika mahojiano na HabariLEO, Benson anakiri kwamba amekuwa akinunua bidhaa hizo kutoka kwa watu mbalimbali wakiwamo watoto.

Hata hivyo, anakana kwa kinywa kipana kuhusika na utoro wa watoto hao shuleni wala kuishi nao nyumbani kwake akiwatumikisha kumkusanyia vyuma chakavu katika mitaa mbalimbali ya mji wa Musoma.

Analalamikia pia hatua ya wazazi kumpakazia kuhusu utoro wa watoto wao, kusababisha polisi kumpekua nyumbani kwake na kumpoteza utulivu ikiwa ni pamoja na tukio la mwezi uliopita, Aprili, ambapo polisi walivamia makazi yake usiku wa manane.

Anasema askari hao walifanya upekuzi lakini hawakupata mtoto hata mmoja asiyekuwa wa familia yake kama ambavyo imekuwa ikidaiwa na watu anaowalalamikia kwa kumpakazia.

“Baada ya kupekuliwa usiku, kesho yake nilitakiwa kuripoti polisi (ilikuwa Aprili 16). Niliwekwa ndani mpaka nilipodhaminiwa Aprili 17 mwaka huu. Nilipangiwa tarehe ya kurudi tena polisi kwenye dawati la jinsia,” analalamika mfanyabiashare huyo.

Wakati Benson akisema hayo, Jane Magesa (siyo jina lake halisi) anadai kwamba mtoto wake wa kiume, Jackson, mwenye umri wa miaka 12 anayesoma darasa la tano, aliacha kwenda shule na kupotea nyumbani tangu Februari 12 mwaka huu kwa kile alichogundua baadaye kwamba alikuwa kwa Benson akimkusanyia vyuma chakavu.

“Nimemtafuta mwanangu tangu Februari hadi alipopatikana Aprili 28 mwaka huu,” anadai Jane.

Anasema mwanae alipopatikana alikuwa na ugonjwa ya ngozi na kwamba kwa sasa anatumia dawa alizopatiwa kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara ambazo kiasi zinamsaidia lakini hali bado.

Anasema kabla ya hapo alipatiwa fomu ya kutibiwa namba tatu (PF3) kupitia dawati la jinsia la polisi mjini Musoma

“Kilio changu nilikifikisha kwa viongozi wote wa mtaa mpaka kwa Ofisa Mtendaji na Kata, kisha nikalamika polisi ambako Askari Agatha wa Dawati la Jinsia, alinipa RB yenye Namba 1733 - Ukatili dhidi ya Mtoto,” anasema.

Anadai kwamba alipoanza kulalamika, mfanyabiashara huyo aliagizwa na uongozi wa shule anayosoma mtoto wake kumrejeshea mama huyo mwanae lakini alikaidi.

Katika mahojiano, mtoto huyo, Jackson (siyo jina lake halisi) anadai kwamba alianza kumuuzia Benson vyuma chakavu akiwa na umri wa miaka 10. Anadai pia alitoroka nyumbani Februari 12 mwaka huu na kwenda kuishi kwa Benson baada ya kunogewa na pesa anazokuwa analipwa.

Jackson anazidi kudai kwamba alipohamia ‘jumla’ kwa Benson aliwakuta watoto wenziye 14 na yeye akawa wa 15, wote kwa ajili ya kazi ya kumkusanyia mfanyabiashara huyo vyuma na plastiki chakavu katika mitaa mbalimbali ya mji wa Musoma na hususani kwenye madampo.

Anadai kwamba kwa kila kilo mfanyabiashara huyo alikuwa anawalipa sh 300.

Kati yao, Jackson anadai kwamba ni mtoto mmoja tu (jina linahifadhiwa) aliyekuwa akienda shule na kwamba watoto wenzake aliokuwa akiishi nao kwa Benson wanatokea maeneo tofauti ya mji wa Musoma, isipokuwa mmoja ambaye asili yake ni Kenya.

Jakson anadai kwamba mtoto mwenye asili ya Kenya alikuja kwa ajili ya kuishi na babu yake lakini alimtoroka na kwenda kuishi kwa Benson.

Mwandishi amemshuhudia Jackson ambaye amejaa upele mwili mzima, huku sehemu zake za siri zikiwa zimevimba na kuwa kubwa mithiri ya tango huku korodani zikiwa mithili ya vikombe. (Picha zinazoonesha hali hiyo zipo lakini kwa ajili ya maadili hatutazichapisha ili kuendana na makala haya).

Jackson anadai kwamba yeye pamoja na wenzake wawili (majina yanahifadhiwa) walipatwa na ugonjwa huo wakiwa nyumbani kwa mfanyabiashara huyo ambaye badala ya kuwashughuli kwa tiba, aliwafukuza.

“Tulikuwa tunalala kwenye uwanja wa nyumba yake, eneo yanakohifadhiwa makorokocho (vyuma na plastiki chakavu). Kila mmoja ana gunia ambalo anaingia ndani yake na kulala humo mpaka asubuhi.

“Kama asingetufukuza huwenda mama asingenipata kwa sababu nilikuwa naogopa kurudi nyumbani na kila nilipomwona mama yangu nilikuwa majificha,” anadai mtoto huyo.

Anazidi kudai kwamba siku ambayo polisi walifanya upekuzi kwenye makazi ya mfanyabiashara huyo, wao walikuwa wameondolewa mapema nyumbani hapo, na kwamba walielekezwa wakalale kwenye pagale lililo jirani na hapo, linalofahamika kama kwa Chigulu.

Kuhusu chakula anasema walikuwa wakisubiri Wanafunzi wa Sekondari ya Mara wamalize kula na wao kuchukua mabaki wakidanganya kuwa yalikuwa ni kwa ajili ya kulisha luku ilhali walipofika nyumbani kwa mfanyabiashara huyo walikuwa wakiyala.

Anadai yeyote miongoni mwa watoto aliyetenda kosa ikiwamo kupeleka mzigo usiyofaa au usiyolingana na uzito aliyoagizwa, aliamriwa kunyanyua mawe juu kama adhabu.

Kaimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nyamatare anayosoma mtoto huyo, Nimrod Mageta, anakiri kufahamu tatizo hilo lake lakini anahisi chanzo ni malezi mabaya ambayo hutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo kufarakana kwa wazazi.

Anasema mahudhurio ya Jackson yalikuwa mabaya tangu akiwa darasa la nne na kwamba kuna wakati ili afike shuleni ilimlazimu mama yake kumpeleka na kumkabidhi kwa walimu.

“Hii biashara ya vyuma chakavu niseme tu kweli inaathiri maendeleo ya wanafunzi kielimu, kiafya hata kimaadili kwa sababu wengi wakiingia huko hatma yao huishia kuwa machokoraa,” anasema Mwalimu Mageta.

Anashauri elimu itolewe kwa wazazi ili wafahamu kuwa wajibu wa kutekeleza majukumu yao kwa watoto wao siyo hiyari wala hisani bali ni matakwa ya kisheria.

Aidha anashauri mamlaka zinazosimamia utekelezaji wa sheria zinazolinda haki za watoto kutobaki maofisini, watoke wafanye kazi mitaani na kuchukua hatua dhidi ya kila anayekiuka sheria hizo.

Mjumbe wa shina Na. 6 (balozi) kuliko na makazi ya mama yake Jackson anakiri kupokea malalamiko kutoka kwa mama huyo na kuyapeleka kwa uongozi wa mtaa wao.

"Nilikuwa naona watoto wengi nyumbani kwa Mama Neema (mfanyabiashara) ingawa sikuweza kufahamu idadi yao lakini tangu alipokamatwa na polisi siwaoni, nasikia aliwafukuza," anadai mjumbe huyo.

Ofisa Mtendaji wa Kata hiyo, Steven Mwara, anakiri kufahamu kuwa mtaa huo una changamoto zinazotokana na uwepo wa biashara ya vyuma chakavu, ambazo zinashughulikiwa kwa ushirikiano wa wazazi na mamlaka nyingine husika.

Anatoa wito kwa wazazi wa watoto wanaotoroka nyumbani, kuwatafuta bila kujali gharama kwa kuwa ni wajibu wa kila mzazi kutimiza majukumu yake kwa mtoto wake, ikiwamo kumhakikishia ulinzi na usalama wa maisha yake.

“Kuna mtoto mwingine (jina linahifadhiwa) alitoroka nyumbani kwao huko Nyegina naye tulimkamatia kwa mfanyabiashara huyo. Tulimtoa na kumkabidhi kwa baba yake lakini cha ajabu, siku chache baadaye alitoroka na kurudi tena… Yaani utadhani wamerogwa,” anasema Mwara.

Anasema kwa sasa sakata hilo linashughulikiwa na mamlaka nyingine, likiwamo Jeshi la polisi.

Akizungumza na HabariLEO kwa njia ya simu, baba mzazi wa mtoto aliyetokea Kijiji cha Nyegina (majina yanahifadhiwa) anasema ni takribani miaka mitatu tangu mwanae atoroke nyumbani na kuacha shule.

“Nyumbani hakuna tatizo lolote naishi na mama yake pamoja na wadogo zake vizuri lakini yeye amekuwa akitoroka na tukimpata na kumrudisha nyumbani, baada ya siku chache anatoroka tena, ametusumbua sana jamani,” anasema.

Anasema mwanae huyo amefikia hatua ya kuiwekea masharti familia yake kwamba, ikitaka asome, imhamishie kwenye shule iliyopo Mtaa wa Nyamatare ili awe anasoma huku akiishi kwa mfanyabiashara huyo lakini walimkatalia.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mara, Daniel Shillah anasema hajafikishwa sakata hilo mezani kwake na kwamba endapo litakifikishwa kwa vile anaamini linaandaliwa na wasaidizi wake atafanya mkutano na vyombo vya habari kulizungumzia.

Ofisa Kazi wa Mkoa wa Mara, Perfect Kimathi, anakiri ofisi yake kuwa na taarifa za malalamiko ya wazazi dhidi ya Benson na kwamba kwa kushirikiana na mamlaka nyingine, wanaendelea kulishughulikia.

Anasema uzoefu unaonesha wafanyabiashara wengi wa chuma chakavu hupenda kuwatumikisha watoto kutokana na urahisi wa kuwalipa ujira mdogo bila kuzingatia kuwa ni kosa la kisheria kutumikisha mtoto kwenye ajira zinazoathiri malezi na makuzi yake.

Sheria Namba 8 ya Mwaka 2006 ya Ajira na Mahusiano Kazini, Sehemu ya II inayohusu Haki za Msingi na Ulinzi, Sehemu Ndogo A – Ajira kwa Watoto, inazuia ajira kwa watoto.

Sheria hiyo inasema katika kifungu 5 (1): Hakuna mtu anayeruhusiwa kumwajiri mtoto mwenye umri chini ya 18.

Sheria hiyo katika 5 (2) inasema mtoto mwenye umri wa miaka 18 anaweza kuajiriwa kufanya kazi nyepesi tu, ambazo haziwezi kuwa na madhara kwa afya na maendelo yake; na hazimzuii kuhudhuria masomo shuleni, kushiriki kwenye ufundi stadi au miradi ya mafunzo iliyothibitishwa na mamlaka yenye madaraka au uwezo wa mtoto kufaidi maelekezo anayoyapata.

Katika 5 (3) sheria inasema mtoto mwenye umri chini ya miaka 18 haruhusiwi kuajiriwa kwenye mgodi, kiwanda au kama kufanya kazi katika meli au katika sehemu nyingine za kazi ikijumuisha ajira isiyo maalumu na kilimo, kwenye mazingira ya kazi ambayo Waziri anaweza kuona ni hatarishi.

Kifungu 10 (4) cha sheria hiyo kinasema: Mtu yeyote haruhusiwi kumwajiri mtoto kwenye ajira: (a) ambayo haifai kwa mtu mwenye umri huo; (b) sehemu ambayo inahatarisha hali nzuri ya mtoto, elimu, afya ya mwili na akili au roho, maadili au maendeleo ya kijamii.

Chanzo: www.habarileo.co.tz