Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Umiliki wa IPTL wazua mjadala nchini

IPTL Mitambo ya IPTL

Wed, 4 Aug 2021 Chanzo: mwananchidigital

Mahakama ya Rufani imebatilisha umiliki wa kampuni ya kufua umeme wa mafuta, Independent Power Tanzania Limited (IPTL) kwa kampuni yake ya Pan Africa Power Solutions (T) Limited (PAP), inayomilikiwa na mfanyabiashara Harbinder Singh Sethi.

Uamuzi huo wakati Seth ameweka mitambo hiyo kama dhamana ya kuachiwa kwake, umetolewa Julai 30, 2021 na jopo la majaji watatu wa mahakama hiyo lilioongozwa na Jaji Agustine Mwarija akishirikiana na Dk Gerald Ndika na Mary Levira, kufuatia maombi ya mapitio yaliyofunguliwa na kampuni ya Mechmar Corporation (Malaysia) dhidi ya hukumu ya Makahama Kuu.

Mechmar iliyokuwa mwanahisa mkuu wa IPTL ikimiliki asilimia 70 ya hisa ilifungua maombi hayo ya mapitio dhidi ya Kampuni ya VIP Engineering and Marketing Limited, inayomilikiwa na mfanyabiashara James Rugemalira, ambayo ilikuwa mwanahisa mdogo ikimiliki asilimia 30 za IPTL.

Wadaiwa wengine walikuwa ni IPTL yenyewe, Kabidhi Wasihi Mkuu, ambaye alikuwa ameteuliwa kuwa mfilisi wa IPTL na PAP.

Katika maombi hayo, Mechmar ilikuwa inapinga uamuzi wa Mahakama Kuu na amri zake, uliotolewa na Jaji John Utamwa, Septemba 5, 2013, ambapo pamoja na mambo mengine, mahakama hiyo ilikabidhi masuala yote ya IPTL mikononi mwa PAP, ambayo pia iliahidi kulipa madeni yote ya IPTL, ambayo yangethibitika.

Miaka takribani miaka minane baadaye, Mahakama ya Rufani katika uamuzi huu mpya imetengua uamuzi huo wa Mahakama Kuu, baada ya kuridhika kwamba ulikuwa na kasoro na kwamba mchakato huo wa kuikabidhi IPTL kwa PAP haukuwa sahihi. Mahakama hiyo imebainisha kwamba Mahakama Kuu ilipaswa kuridhia tu maombi ya VIP kuondoa mahakamani shauri lake la kutaka kufungwa kwa IPTL, na kwamba amri pekee ambayo ilipaswa kuitoa ni VIP kulipa gharama za shauri hilo.

Hivyo, Mahakama ya Rufani imefafanua kuwa amri ya kuhamishia masuala ya IPTL kwa PAP ilikusudia kutamka au kuipa haki PAP kana kwamba, Mahakama Kuu ilikuwa imesikiliza na kuamua shauri katika ustahimilivu wake na mbaya zaidi ni kwamba PAP haikuwa mdaiwa katika shauri hilo.

“Amri zilizofuatia katika shauri hili hazikuwa na miguu ya kusimamia,” imesema Mahakama ya Rufani katika uamuzi wake huo baada ya kusikiliza na kujadili hoja za pande zote na kubainisha kuwa inaona sababu ya pili ya maombi hayo ina ustahimilivu na inatosha kumaliza maombi na haina haja kuendelea na sababu ya tatu.

“Kwa hayo yote tunaona usahihi wa maombi, ambayo tunayakubali. Tunabatilisha na kufuta amri amri zote zilizofuatia zilizotolewa na Mahakama Kuu,” imehitimisha uamuzi wake Mahakama ya Rufani.

Hata hivyo imebainisha kuwa amri ya Mahakama Kuu inayobaki ni ile tu ya kutambua VIP kuliondoa mahakamani shauri lake.

Wakati wa usikilizwaji wa maombi hayo, Mechmar iliwakilishwa na wakili Gaspar Nyika, VIP iliwakilishwa na Michael Ngalo wakati IPTL na PAP ziliwakilishwa na wakili Lutema na Kabidhi Wasihi Mkuu aliwakilishwa na mawakili wa Serikali, Benson Hosea na Samwel Mutabazi.

Uamuzi wa Makama Kuu

Mahakama Kuu ilifikia uamuzi wa kuikabidhi IPTL kwa PAP baada ya kampuni ya VIP kuwasilisha mahakamani maombi ya kuondoa shauri lake la awali la kutaka kufunga shughuli za kampuni hiyo ya IPTL.

VIP ilikuwa imefungua maombi ya kutaka kuifunga IPTL kufuatia mgogoro na mwanahisa mwenzake, Mechmar, lakini Mechmar nayo ilifungua mahakamani hapo maombi mengine ikipinga yale ya VIP. Maombi yote mawili yaliunganishwa katika shauri moja.

Baadaye VIP ndipo ilipowasilisha maombi mapya ya kuliondoa shauri hilo, huku pia ikiwasilisha hati ya makubaliano ya uhamishaji wa hisa zake kutoka IPTL kwenda kwa kampuni ya PAP, inayomilikiwa na mfanyabiashara Harbinder Singh Sethi.

Kulingana na makubaliano hayo ya ununuzi wa hisa za VIP, pia ilidaiwa kuwa tayari PAP ilikuwa imeshanunua hisa asilimia 70 za Mechmar, ambazo ilidai zilikuwa zimenunuliwa na kampuni ya Piper Link ambayo pia inamilikiwa na Sethi.

Mechmar kupitia kwa mawakili wake wawili ambao pia walikuwa na mgogoro wa yupi mwakilishi halali wa kampuni hiyo kati ya Melichisedeck Lutema na Seni Malimi ambao Mahakama Kuu ilipaswa kuutatua kwanza, walikuwa na msimamo tofauti katika maombi hayo ya VIP kuliondoa mahakamani shauri hilo,

Wakati Lutema alkikubaliana na maombi ya VIP kuliondoa shauri hilo na hata VIP kuhamishia hisa zake kwa PAP; Malimi licha ya kutokuwa na pingamizi kwa VIP kuondoa shauri kortini, alipinga mchakato wa kuhamishia hisa za VIP kwa PAP na PAP kupewa umiliki wa IPTL, akisema mchakato huo haukuwa halali.

Hata hivyo, Mahakama Kuu katika uamuzi wake, hata kabla ya kumaliza mgogoro wa wakili, ilikubaliana na maombi ya VIP kuliondoa shauri lake la kutaka kuifunga IPTL.

Mbali na hilo, Jaji Utamwa alitoa amri nyinginezo zikiwemo hisa za VIP kuhamishiwa kwa kampuni ya PAP na masuala yote ya IPTL kuwa chini ya PAP. Mechmar kupitia kwa wakili Malimi haikuridhika na uamuzi huo wa Mahakama Kuu, hivyo mwaka huo huo 2013 ilifungua maombi ya mapitio Mahakama ya Rufani, ikiiomba ipitie uamuzi huo na kujiridhisha na uhalali wake.

Hata hivyo, VIP kupitia kiapo cha mmiliki wake, James Rugemalira ambaye kwa sasa yuko mahabusu akikabiliwa na kesi inayotokana na sakata hilo la IPTL na mali zake, ilipinga maombi hayo ya Mechmar.

Pia IPTL na PAP kupitia kiapo cha wakili Melchisedeck Lutema na kiapo cha nyongoneza cha mmiliki wa kampuni hizo, Seth zilipinga maombi ya Mechmar.

Wakati maombi hayo ya mapitio ya Mechmar yakiwa bado hayajasikilizwi, PAP kufuatia uamuzi huo wa Mahakama Kuu, ilimiliki mali zote za IPTL , ukiwemo mtambo wa kufua umeme na Akaunti Maalumu ya Tegeta Escrow iliyofunguliwa kwa pamoja kati ya IPTL na Shirika la Umeme (Tanesco).

Akaunti hiyo ilifunguliwa kwa ajili ya kuweka pesa za malipo ya uwekezaji, ambazo Tanesco ilipaswa kuzilipa kwa IPTL, ili kusubiri kumalizika kwa mgogoro uliohusu kiwango sahihi ambacho Tanesco ilipaswa kukilipa.

Baada ya PAP kumilikishwa IPTL, ilichukua fedha zote zilizokuwemo ndani ya akaunti hiyo kiasi cha Sh309,461,300,158.27 na USD 22, 198,544.60, na sehemu ya fedha hizo zikachukuliwa na Rugemalira kama malipo ya hisa zake asilimia 30 alizokuwa akizimiliki IPTL (sasa akiziuza kwa PAP).

Chanzo: mwananchidigital