Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ukatili wa kutisha Dar mgambo wa Makonda

15017 Mgambo+pic TanzaniaWeb

Sat, 1 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mgambo wanaosimamia operesheni ya usafi Dar es Salaam, wanadaiwa kuwafanyia ukatili wananchi katika maeneo mbalimbali jijini hapa kwa kuwapiga na kuwajeruhi.

Hayo yamebainika baada ya video kusambaa kwenye mitandao ya kijamii zikiwaonyesha mgambo hao wanaosimamia operesheni hiyo iliyoasisiwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda wakiwapiga wananchi na wengine kulalamika kujeruhiwa.

Moja ya video hizo inamuonyesha mwanamume mmoja akipigwa na mgambo hao kwa rungu kubwa jambo ambalo liliamsha hisia za wananchi.

Taarifa za matukio hayo ziliifikia polisi na jana, kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Jumanne Muliro alisema tayari mgambo watatu wamekamatwa.

Kamanda Muliro alimtaja aliyepigwa na kujeruhiwa kuwa ni mkazi wa Bunju A, Robson Orotho kwa madai ya kutolipa faini ya usafi ya Sh50,000 na mgambo wanaoshikiliwa kwa tukio hilo ni Kelvin Edson, Gudluck Festo na Rehema Nyange.

“Kukamatwa kwa watuhumiwa hao kulitokana na taarifa zilizoonyesha kukiukwa kwa sheria za nchi, kitendo ambacho kilililazimisha jeshi la polisi kufanya ufuatiliaji wa haraka na kufanikiwa kuwatia mbaroni watuhumiwa wote waliohusika na tukio hilo. Jeshi la Polisi linatoa wito vyombo vyote vya umma na vile visivyokuwa vya umma kufanya kazi kwa kufuata misingi ya sheria, taratibu na kanuni za nchi.”

Aidha, taarifa ambazo Mwananchi imezipata zinasema kuwa baadhi ya wakazi wa Kimara jana walikimbia makazi yao kwa muda kuwakwepa mgambo hao.

Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani, Juni 5, Makonda alitangaza kuanzisha operesheni ya usafi wa mazingira akisema itashirikisha askari 400 wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ili kuhakikisha jiji hilo linakuwa safi.

Mbele ya Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, mkuu huyo wa mkoa alisema usafi katika jiji lake bado ni tatizo watu ni wachafu, wanatia aibu.

“Naomba unifikishie salamu hizi kwa Rais John Magufuli, hapa ni askari wa JKT 400. Ziba masikio nataka niendeshe operesheni ili jiji linyooke na liwe safi,” alisema Makonda.

Taarifa za kupigwa kwa wananchi hao zilianza kusambaa jana asubuhi katika mitandao ya kijamii na moja ya video zinamuonyesha mwanamke aliyekuwa akitokwa na damu usoni kutokana na jeraha katika paji lake la uso huku akisikika akisema; “Wamekuja kumkamata yule kaka wanampiga marungu ya kwenye miguu na kichwani, nikawaambia kwa nini mnampiga, nikafika nikamshika yule askari, kumshika askari akachukua rungu lake akanipiga usoni, sasa sheria gani inasema askari ana…”

Hata hivyo, jina la mwanamke huyo na makazi yake havikufahamika.

Mbali na video hiyo, kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wanachi wakidai kutukanwa na kufanyiwa vitendo vya kibabe na mgambo hao ikiwamo kuingia ndani ya vyumba kwa nguvu na kuwakamata wananchi.

Awali, baada ya kusambaa kwa taarifa hizo, Mwananchi liliwatafuta wakuu wa wilaya za Temeke, Kinondoni na Ubungo kuzungumzia operesheni hiyo ambao walisema kesi hizo ni za Wilaya ya Ilala.

“Mimi mgambo wangu wako shwari, mtafute mkuu wa Wilaya ya Ilala maana nasikia, wananchi waliopigwa ni wa Ilala,” alisema mkuu wa Wilaya ya Temeke, Felix Lyaniva.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Daniel Chongolo hajasikia tukio lolote lililoripotiwa kwenye wilaya yake lakini amekuwa akisikia visa hivyo Wilaya ya Ilala.

Alipotafutwa, mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema alisema hana taarifa rasmi juu ya mgambo kuwapiga raia ndani ya wilaya yake licha ya kufahamu kuwapo kwa oparesheni ya usafi inayoongozwa na mkuu wa mkoa.

“Hayo ya mgambo kupiga wananchi siyajui ila taarifa ambazo pia nimezisikia jana (juzi) ni mgambo kuwakimbiza wananchi na kuwaharibia vitu vyao, hizo ndizo ninazozijua lakini hizi za kuwapiga kwa kweli hazijafika ofisini kwangu,” alisema.

“Ninachokifahamu pia ni kwamba kwa sasa kuna operesheni ya usafi inayoongozwa na mkuu wa mkoa ambapo mgambo wa jiji na JKT ndiyo wanaosimamia.”

Mjema alikemea tabia ya mgambo kujichukulia sheria mkononi kwa kuwapiga wananchi akisema wanachotakiwa kufanya ni kuwapa elimu siyo kuwafukuza au kuwapiga, kuharibu mali au kuwakimbiza. Alisema ni vyema wakaongozana na viongozi wa mitaa huku akiwataka wananchi wasiogope kutoa taarifa wanapofanyiwa vitendo vya ukatili.

“Hakuna sheria inayomruhusu mgambo kumpiga mwananchi, kumkimbiza wala kumharibia mali zake, wakifanya hivyo ni kosa tena ni kosa kubwa,” alisema.

Akizungumzia suala hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Salum Hamduni alisema ameziona video zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii na kuagiza maofisa wake kufuatilia kwa karibu kinachotokea mitaani.

Hamduni aliwataka watu wanaopigwa na mgambo hao kuripoti kwenye vituo vya polisi vilivyokaribu yao ili jeshi hilo litoe msaada na kuchukua hatua za kisheria.

“Baada ya kuona clip hizo, nimechukua hatua kama kiongozi mwenye jukumu la kulinda usalama kwa kutuma timu yangu. Maofisa wangu wako field kufuatilia kinachoendelea, wakithibitisha hilo tutatoa taarifa rasmi,” alisema Hamduni.

Chanzo: mwananchi.co.tz