Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ujenzi wa Vituo Jumuishi wa Utoaji Haki waikuna PAC

Pindapo Kutoka Kushoto, Geofrey Pinda, Japhet Hasunga na Prof Elisante ole Gabriel

Thu, 24 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali imeridhishwa na jinsi Mahakama ya Tanzania ilivyotumia fedha katika utekelezaji wa miradi miwili ya Ujenzi wa Vituo Jumuishi wa Utoaji Haki (Integrated Justice Centres-IJCs) za Temeke na Kinondoni.

Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo,Japhet Hasunga wakati wa ziara yao ya siku moja ya kutembelea Mradi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki cha Temeke na Kinondoni.

‘Baada ya mahojiano na ukaguzi wa miradi yote miwili, Kamati imeridhika kuwa thamani ya fedha iliyotumika inalingana na miradi iliyotekelezwa na Mahakama ya Tanzania katika maeneo hayo,” amesema Hasunga.

Hasunga ameongeza kuwa fedha hizo zimetumika kujenga majengo na kuimarisha mifumo ambayo inasaidia katika kuharakisha utoaji haki kwa wananchi katika mazingira rahisi.

Aidha; Kamati imepongeza pia Mahakama kwa kuimarisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano(TEHAMA) katika utoaji haki na uhifadhi wa nyaraka mbalimbali ambapo wananchi wamesogezewa huduma.

Naye, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria,Geophrey Pinda amesema ujenzi wa Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki (IJC) umesaidia kusogeza huduma na kuwafikia wananchi wengi kwa urahisi.

Amesema Serikali iko katika mpango wa kutafuta fedha kwa ajili ya kuiwezesha Mahakama kujenga Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki katika Kanda 12 zilizobaki ili kuwawezesha wananchi kupata huduma kwa karibu.

“Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki vimekuwa kimbilio kubwa kwa wananchi ambapo kwa Temeke pekee kwa siku wanapokea wananchi Zaidi ya 400 ambao wanakwenda kupeleka mashauri mbalimbali,” amesema Pinda.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel amesema wamefanikiwa kujenga Vituo Jumuishi 6 katika Mikoa mitano kwa gharama ya shilingi bilioni 51.5.

Amesema Vituo hivyo viko katika Mkoa wa Dar es Salaam (Temeke na Kinondoni), Arusha, Morogoro, Mwanza na Dodoma.

Prof. Ole Gabriel amesema katika IJC kuna Mahakama ya Mwanzo hadi ya Rufaa na pia zipo Ofisi za wadau mbalimbali kama vile Maafisa wa Magereza, Polisi, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka, Ofisi za Mawakili wa Kujitegemea na wengine ambao wakatika mnyoro wa utoaji haki.

Kamati inatarajia kuendelea na ziara yake ya ukaguzi wa Mradi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki cha Morogoro mwishoni mwa Mwezi huu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live