Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uhamiaji Mtwara yawadaka wahamiaji haramu, wakiwemo watoto 15

Wed, 29 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mtwara. Idara ya Uhamiaji mkoani Mtwara inawashikilia raia 38 wa kigeni, wakiwemo watoto 15 kwa tuhuma za kuishi nchini bila kibali.

Raia hao ni kutoka nchi za Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Uganda.

Akizungumza na MCL Digital leo Jumatano Agosti 29, 2018, ofisa Uhamiaji mkoani Mtwara, James Mwanjotile amesema raia hao wa kigeni walikamatwa jana eneo la Kiangu mjini Mtwara.

Amesema walikamatwa baada ya kupata taarifa kutoka kwa watoa taarifa wa idara hiyo, wanamshikilia mmliki wa nyumba ambayo raia hao walikutwa.

“Wanasema lengo lao ilikuwa ni kwenda Comoro wakishatoka hapo waende Ufaransa, ni tofauti na wengine ambao huwa wanasema wanakwenda Msumbiji,” amesema.

“Wote hawa tumewakuta kwenye nyumba moja wamewekwa katika vyumba tofauti. Asilimia 99 wameingia nchini kihalali lakini vibali vyao vilikuwa vimekwisha muda kasoro mama mmoja Mganda amesema hati yake ya kusafiria imeibiwa.”

Amesema, “tunafanya maandalizi ya kuwachukua maelezo yao na baadaye tutawafikisha mahakamani. Pia kuna watoto wengine ni wadogo sana,  mfano kuna mtoto wa miezi mitatu na mazingira tuliyowakuta nayo ni magumu.”

Mmiliki wa nyumba hiyo, Ally Said amesema watu hao wamekutwa katika nyumba yake baada ya kumpangisha mmoja wa marafiki zake kwa gharama ya Sh500,000.

“Rafiki yangu aliuliza kama nyumba yangu ina mpangaji akaomba nimpangishe kwa muda wa mwezi mmoja lakini wageni wake watakaa kwa wiki mbili kutokana na gharama za nyumba za wageni kuwa kubwa,” amesema.

“Baada ya muda niliwaona wakiwa na wasiwasi nikamuuliza mhusika akasema wana hati za kusafiria na  wataondoka lakini kabla ya kuondoka wamekamatwa.”

Mmoja wa raia hao kutoka Congo, Vivian Nyota amesema, “nilikwenda Kigoma kuchukua watoto lakini kuna dada nilikuwa namdai fedha zangu akaniambia nije Mtwara lakini nilipofika akawa hapatikani na sikuwa na fedha ya gesti ikabidi niombe sehemu ya kulala.”

 

 

 

 

Chanzo: mwananchi.co.tz