Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uhalifu watoto wa kiume tishio jipya

Panya Road Kortini Uhalifu watoto wa kiume tishio jipya

Wed, 26 Jul 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ulawiti, unyang’anyi wa kutumia silaha, mauaji, wizi na matusi ni makosa yanayofanywa na watoto hasa wa kiume, mamlaka zimethibitisha.

Aidha, asilimia kubwa ya watoto wa kiume wanaofikishwa katika Mahakama ya Watoto jijini Dar es Salaam, wanashtakiwa kwa makosa ya ulawiti.

Akizungumza na Nipashe, Meneja wa Mahabusu ya Watoto iliyopo Upanga, jijini Dar es Salaam, Darius Kalijongo, alisema aina hiyo ya uhalifu kwa watoto inachangiwa na malezi duni, makundi rika pamoja na umaskini kwa kipato cha familia.

Alisema watoto wanaotuhumiwa kwa makosa wamethibitika kuyatenda kweli.

Alitoa mfano kwamba katika kipindi cha miaka minne iliyopita (2018/20192021), jumla ya watoto wa kiume 448 walipokewa katika mahabusu hiyo, 150 kati yao walikuwa wamefanya unyang’anyi kwa kutumia silaha na 84 walilawiti wenzao.

Kalijongo alitaja makosa mengine yaliyofanywa na watoto wa kiume na idadi yao kwenye mabano kuwa ni mauaji (10), wizi (76), matusi (4), kujeruhi (6) na kuingia nchini bila kibali (36).

Kwa upande wa watoto wa kike, meneja huyo alisema waliofikishwa katika mahabusu hiyo kwa kipindi hicho ni 17 ambao walikuwa wanakabiliwa na makosa ya mauaji (5), kujeruhi (3), bangi (1) na kuingia nchini bila kibali (8).

Alisema vitendo vya ulawiti vinachangiwa na utandawazi, kwa watoto kuona kwenye televisheni au kwenye simu.

Alisema changamoto inayoikabili jamii kwa sasa ni wazazi pamoja na walezi kushindwa kutoa ushirikiano wakati wa mchakato wa marekebisho ya tabia, pale mtoto anapokuwa ametenda kosa.

Alitoa mfano kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Julai 2021 hadi Juni 2022, mahabusu hiyo ilipokea watoto 123, kati yao 48 walikuwa wamefanya uhalifu wa unyang’anyi wa kutumia silaha.

Makosa mengine na idadi ya watoto waliotenda kwenye mabano ni mauaji (4), wizi (25), ulawiti (6), ubakaji (11), kujeruhi (4) na uhujumu uchumi (1). Makosa mengine kwa mujibu wa meneja huyo ni kuvunja na kuiba (2), kuingiza mifugo shambani (2), kupanga njama ya wizi (6), shambulio la aibu (1), kukutwa na mali ya wizi (1), kuingia nchini bila kibali (12) na kwamba hakuna aliyeshtakiwa kwa kukutwa na bangi wala kuua kwa kutokusudia.

“Changamoto kubwa zinazotukabili kwa sasa ni kuongezeka kwa makosa makubwa ambayo watoto wanashtakiwa nayo, mashauri ya mauaji (PI), kuchukua muda mrefu na kukosekana kwa programu endelevu ya ufuatiliaji hasa kesi inapokwisha,” alisema.

Alisema kwa Jiji la Dar es Salaam, maeneo ambayo watoto wanatoka ni Bunju, Temeke, Mbagala, Kigamboni, Chanika, Kinyerezi, Bagamoyo, Chalinze, Gongo la Mboto, Kigogo Luhanga, Kibaha, Mburahati, Tandika, Manzese, Mbezi Mwisho na Mbezi Juu. Alisema kwa wanaoingia nchini bila kibali wanatoka nchi za Kongo na Burundi.

MAHAKAMA YA WATOTO

Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Watoto iliyopo katika Kituo Jumuishi cha Temeke, Orupa Mtae, aliiambia Nipashe kwamba wanapokea kesi za madai na za jinai, zikiwamo za wizi, ubakaji na ulawiti.

“Kwenye makosa ya jinai, asilimia kubwa ya kesi tunazopokea hivi sasa ni za ukatili wa kingono na kijinsia. Kwa sasa nyingi ni za kulawiti kwa maana ya mtoto kumwingilia mwingine kinyume cha maumbile,” alisema.

Alisema: “Takwimu halisi siwezi kukupa, lakini kesi za ulawiti ni nyingi sana ukilinganisha na hizi nyingine kama wizi, mengi tunayoyapokea ni ulawiti na kubaka; asilimia kubwa ni ulawiti.”

Hakimu Orupa aliongeza: “Makosa ya kubaka yapo, lakini yanayoongoza ni kulawiti. Asilimia kubwa ni watoto wa kiume kuingilia wenzao wa kiume, chache sana za watoto wa kike kuingiliwa kinyume na maumbile.”

Alisema tathmini yake imebaini kwamba watoto wanaojihusisha na makosa hayo kutokana na malezi duni ya wazazi au walezi.

“Natoa rai kwa wazazi kuwa macho zaidi katika malezi, wazazi pia wawajengee uwezo watoto wa kujitambua na kujikinga dhidi ya matendo haya,” alisema.

Hakimu Orupa alisema watoto wengi wanashawishiwa na kurubuniwa kwanza kabla ya kufanyiwa vitendo hivyo na kueleza kuwa mzazi makini anaweza kumsaidia mtoto kabla ya kulawitiwa.

“Yule anayemfanyia tukio (ulawiti), haanzi moja kwa moja bali kuna vishawishi watoto wanafanyiana, kuna wengine wanasema walikuwa wanaangalia picha za ngono na kuambiwa afanye kama alivyoona, wengine wanajifunza kwa wenzao shuleni, kwa hiyo kabla ya tukio lenyewe, kuna vitu vya awali vinafanyika,” alisema Orupa.

Hakimu Orupa alisema baadhi ya watoto wanajifunza na kufanya uhalifu kutokana na wazazi na walezi wao kutowalea ipasavyo kutokana na majukumu ya kutafuta kipato.

Alisema wazazi na walezi wengi, wanaondoka nyumbani alfajiri wakati ambao watoto nao wanajiandaa kwenda shule, na wanarudi wakiwa wamechoka kiasi cha kushindwa kuongea na watoto.

Hakimu huyo anawashauri wazazi kuweka utaratibu wa kuzungumza na watoto kila siku. “Inawezekana siku unayoongea naye ndiyo siku ambayo ameanza kushawishiwa, ukiongea naye utazuia tukio la ulawiti au ubakaji,” alisema.

MIPANGO YA BAADAYE

Meneja wa mahabusu hiyo alisema wanakusudia kuanzisha programu endelevu zitakazowezesha watoto kujifunza stadi za maisha ikiwamo uchoraji, ufugaji wa kuku na samaki.

Alisema wanaimarisha eneo hilo kwa kutoa ujuzi wa ufundi, kilimo na ufugaji ikiwamo ushonaji, ususi, kilimo cha bustani, kompyuta na ufundi wa aina mbalimbali.

Alisema baadhi ya watoto wamepewa mitaji na vitendea kazi.

“Watoto watatu wamepewa vyerehani na sasa wanaendelea na shughuli za ushonaji, wanne wamewezeshwa kuanzisha biashara ndogondogo, wawili wanashiriki katika shughuli za kilimo na mmoja amejiunga na Chuo cha Uchungaji,” alisema Kalijongo.

Aliongeza kuwa: “Watoto watano wameajiriwa na wengine wamejiajiri wenyewe na wanne wamerudi shule baada ya kesi zao kumalizika.”

Alisema programu ya uchepushaji na kudhaminiwa na kuimarika kwa ushirikiano kati ya mahabusu hiyo na maofisa ustawi wa jamii, polisi na mahakama, kumepunguza idadi ya watoto katika mahabusu hiyo.

Ripoti za mamlaka hizo mbili zinakuja takribani miezi miwili tangu Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania (LRCT), ianze utafiti na mapitio ya sheria zinazosimamia makosa dhidi ya maadili nchini.

Mei 12, mwaka huu, LRCT iliwakutanisha wakuu wa upelelezi wa jinai Tanzania Bara na Zanzibar na waendesha mashtaka wa mikoa ya Tanzania bara ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Bunge na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kuiagiza Wizara ya Katiba na Sheria, kufanya utafiti huo kutokana na ongezeko la vitendo vya mmomonyoko wa maadili nchini.

Kikao hicho kilichohudhuriwa na Katibu Mtendaji wa LRCT, Griffin Mwakapeje, kililenga kupata taarifa na takwimu za makosa hayo nchini na changamoto za kisheria wanazokabiliana nazo katika ukamataji, upelelezi na uendeshaji wa mashauri hayo mahakamani.

Makosa dhidi ya maadili ni pamoja na kubaka, genge la ubakaji, kujaribu kubaka, kuteka, udhalilishaji wa kingono, kuwaingilia kingono watu wenye ugonjwa wa afya ya akili, kumwingilia mtu asiye mke mwenye umri chini ya miaka 18 bila ridhaa yake na kuwatweza watoto kingono.

Makosa mengine ni udhalilishaji mkubwa wa kingono, uwakala wa ukahaba, kumiliki madanguro, kuingilia kinyume na maumbile (ushoga), kuzini na maharimu, kusambaza picha za ngono, ponografia kwa watoto na kwa njia ya mtandao na usagaji.

Katika kikao hicho, Mkurugenzi Tishio ongezeko makosa uhalifu watoto wa kiume wa Mashtaka (DPP), Sylvester Mwakitula, alisema asilimia 40 ya mashtaka katika Wilaya ya Kigamboni ni ya mmomonyoko wa maadili, yakihusisha vitendo vya ulawiti na ubakaji.

Alisema kumekuwa na ongezeko la makosa ya ulawiti, ubakaji na ukatili wa kijinsia nchini. “Makosa haya yapo nchi nzima, japo kuna mikoa na sehemu chache yanaonekana yapo zaidi, lakini ni tatizo kubwa kwa taifa letu…katika Wilaya ya Kigamboni mashtaka ambayo yapo mahakamani karibu asilimia 40 ni ya namna hii, kwa hiyo mnaweza kuona namna ambavyo tatizo ni kubwa,” alisema.

Taarifa ya DPP iliungwa mkono na Hakimu Orupa aliyesema kesi nyingi za ulawiti wanazopokea katika mahakama yake zinatoka Wilaya ya Kigamboni.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live