Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uhalifu wapungua 16%, udhalilishaji bado changamoto

Abe0ebdc8f540a6a87dff7e1007b6676 Uhalifu wapungua 16%, udhalilishaji bado changamoto

Thu, 21 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

MKUU wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP), Simon Sirro, amesema uhalifu nchini umepungua kwa asilimia 15.5 kutoka matukio ya uhalifu 58,590 yaliyofanyika katika mwaka 2019 hadi matukio 50,689 yaliyofanyika mwaka jana (2020).

Sirro alitoa taarifa hiyo jana kwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Khamis Hamza Chilo aliyefanya ziara ya kikazi kwenye Makao Makuu ya Jeshi la Polisi yaliyopo jijini hapa.

"...hali ya ulinzi na usalama nchini ni shwari kwani uhalifu umepungua kwa asilimia 15.5 japo kuna changamoto ya kuwepo kwa vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia pamoja na uhalifu unaovuka mipaka. Jeshi la Polisi bado linaendelea kuyashughulikia kwa kufanya operesheni mbalimbali za kuzuia uhalifu,"alisema jijini Dodoma.

IGP Sirro alisema Polisi wanaendelea kutoa elimu ya ushirikishwaji wa jamii kwa wananchi na aliwataka wananchi hao kujihadhari na kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu kwa jeshi hilo ili wakamatwe na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Alisema katika kutoa elimu jeshi hilo pia linawatumia viongozi wa dini kuwahubiria waumini wao kujihadhari na vitendo vya uhalifu na wanasiasa mbalimbali kuelimisha wananchi wao kuepuka vitendo hivyo vya kihalifu.

Chilo alilitaka Jeshi la Polisi liendelee kutoa elimu kwa jamii juu ya dhana ya ushirikishwaji wa jamii kwani ndio muarubaini wa kupunguza uhalifu nchini.

Pia alilitaka jeshi hilo kuendelea kujenga ushirikiano na jamii kwani ubia huo una matokeo chanya katika kuzuia uhalifu.

Akikagua jengo jipya la Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, ameliahidi kuhakikisha anashirikiana bega kwa bega na Jeshi la Polisi katika kuboresha vitendea kazi ikiwa ni pamoja na kuhakikisha jengo hilo linakamilika ili watendaji wake waweze kutekeleza majukumu yao katika mazingira mazuri yatakayo wawezesha kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi.

Chilo ameagiza Jeshi la Polisi kuhakikisha kwamba, wanaendelea kudhibiti vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia katika jamii kwa kuendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya namna ya kuzuia vitendo hivyo pamoja na kuhakikisha hatua thabiti za kisheria zinachukuliwa dhidi ya watuhumiwa wa vitendo vya ubakaji na ulawiti.

Aidha, aliwataka wananchi kuacha tabia ya kumaliza kesi za udhalilishaji wa kijinsia kinyume na utaratibu badala yake washirikiane na jeshi hilo kwa kutoa taarifa ili wahusika waweze kushughulikiwa kisheria.

Chanzo: habarileo.co.tz