Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ugonjwa wa shahidi waahirisha kesi ya Sabaya

Df74f888b88d30ccce20a399ae24f135.jpeg Ugonjwa wa shahidi waahirisha kesi ya Sabaya

Sat, 23 Oct 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SHAHIDI wa saba katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita, bado anaumwa tumbo na kusababisha kushindwa kuendelea kwa kesi hiyo na kuahirishwa hadi Oktoba 27, mwaka huu.

Kesi hiyo iliahirishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha baada ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Felix Kwetukia kuiomba mahakama kuiahirisha kesi hiyo hadi wiki ijayo kwa kuwa shahidi huyo, Ramadhani Juma bado ni mgonjwa na hakukuwa na shahidi mwingine.

Juzi mchana, Juma alishikwa ghafla na ugonjwa wa tumbo na kuiomba

mahakama kuwa hatakuwa tayari kutoa ushahidi siku hiyo hadi jana.

Kwetukia alidai mbele ya Hakimu Mkazi, Mkoa wa Arusha, Patricia Kisinda anayesikiliza kesi hiyo kuwa shahidi Juma ambaye ni mfanyakazi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Arusha bado hali yake si nzuri.

Alidai upande wa Jamhuri unachukulia kwa uzito na kipaumbele kikubwa kesi hiyo na ndio maana inasikilizwa kwa wiki nzima mfululizo ili mashahidi wote 20 ambao wanapaswa kutoa ushahidi watoe ushahidi kwa muda muafaka bila kuwepo ucheleweshaji wa aina yoyote. Adai ugonjwa wa shahidi wa saba uko nje ya uwezo wao.

Mawakili wa utetezi wakiongozwa na Mosses Mahuna, walipinga kua-

hirishwa na kudai ni ucheleweshaji wa makusudi wa kesi hiyo kwa upande wa Jamhuri.

Waliomba mahakama kutokubali ombi hilo. Waliomba aiamuru Jamhuri kumwita shahidi mwingine kesi iweze kuendelea kwani muda unaruhusu kufanya hivyo.

Kutokana na malumbano hayo, Hakimu Kisinda alitoa uamuzi mdogo na kukubaliana na upande wa Jamhuri wa kuahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 27 mwaka huu.

Alisema itasikilizwa mfululizo na aliwataka waendesha mashitaka wa serikali kujiandaa ikiwa ni pamoja na kuleta mashahidi wengine iwapo Juma ataendelea kuwa mgonjwa.

Mbali ya Sabaya washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni pamoja na Enock Mnkeni (41), Watson Mwahomange (27) maarufu kwa

jina la Malingumu, John Aweyo (45), Syliverster Nyengu (26) maarufu kwa jina la Kicheche ambaye pia ni Msaidizi wa Sabaya, Jackson Macha (29) na Nathan Msuya (31).

Katika kesi hiyo, Sabaya na wenzake, shitaka la kwanza ni la uhujumu uchumi la pili linamkabili Sabaya mwenyewe kuwa akiwa mtumishi wa umma alishiriki kushawishi rushwa ya Sh milioni 90 kutoka kwa mfanyabiashara jijini Arusha, Francis Mrosso.

Shitaka la tatu linalomkabili Sabaya ni kuwa Januari 20 mwaka huu ndani ya Jiji la Arusha na Mkoa wa Arusha aliomba rushwa ya Sh milioni 90 kutoka kwa Mrosso aweze kumsaidia katika kesi iliyokuwa ikimkabili ya ukwepaji kodi. Shitaka la nne ni la utakatishaji fedha lililokuwa likiwakabili washitakiwa wote saba.

Chanzo: www.habarileo.co.tz