Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Udhuru ya Mbowe yakwamisha kesi

86299 Mbowepic Udhuru ya Mbowe yakwamisha kesi

Fri, 29 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeshindwa kuendelea na kesi ya uchochezi inayowakabili viongozi tisa wa Chadema kutokana mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe kuwa na ahadi ya kuonana na daktari wake.

Mbowe kupitia wakili wake, Peter Kibatala ameieleza mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Alhamisi Novemba 28, 2019 wakati shauri hilo lilipoitwa kwa ajili kuendelea na usikilizwaji.

Kibatala amedai  Mbowe alikuwa ana ahadi na daktari wake saa 4 asubuhi lakini kutokana na umuhimu wa kesi hii aliona aje mwenyewe kutoa taarifa mahakamani.

Amedai Mbowe anakwenda kuangaliwa afya yake na kutokana na sababu hizo wanaomba mahakama hiyo iahirishe kesi.

" Kutokana hali hii upande wa utetezi tunaomba mahakama imruhusu mteja wangu aende kuonana na daktari wake kama alivyoshauriwa. Tunaomba kesi hii iahirishwe hadi Desemba 2, 2019," amedai Kibatala.

Baada ya maelezo hayo, upande wa mashtaka ukiongozwa na mkurugenzi msaidizi wa mashtaka, Joseph Pande umepinga ombi hilo kwa kuwa halina msingi na kuiomba mahakama iendelee na usikilizwaji wa shauri hilo kama ilivyopangwa.

Pande amesema ombi hilo halijabainisha kama mshtakiwa huyo hayupo katika hali ya kutoendelea na kesi kwa hiyo haliifungi mahakama kuendelea na kesi hiyo.

Baada ya kupitia hoja za pande zote, hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba ameahirisha kesi hiyo hadi kesho Ijumaa saa 4:30 asubuhi.

“Kwa kuwa kesi hii ni ya muda mrefu naiahirisha hadi kesho itakapoendelea na sio Desemba 2, 2019 kama upande wa utetezi walivyoomba,” amesema Hakimu Simba.

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine  ni  Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vicent  Mashinji; naibu makatibu wakuu, John Mnyika (Bara) na Salum Mwalimu (Zanzibar).

Mbunge wa  Tarime Vijijini,  John Heche; Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini); Esther Matiko (Tarime Mjini); Halima Mdee (Kawe); Ester Bulaya (Bunda).

Mbowe na wenzake wanakabiliwa na mashtaka 13 yakiwemo ya uchochezi, kufanya mkusanyiko usio halali na kukaidi amri ya jeshi la polisi.

Chanzo: mwananchi.co.tz