Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uchunguzi kijana anayedaiwa kufia mahabusu sura mpya

Mutafungwa.webp Uchunguzi kijana anayedaiwa kufia mahabusu sura mpya

Wed, 20 May 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

JESHI la Polisi mkoani Morogoro limeanza kufanya uchunguzi kubaini mazingira tatanishi ya kifo cha Kelvin Mapondela (22), ambaye mwili wake bado umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti Hospitali ya Mt. Francis, mjini Ifakara kwa takribani wiki tatu kutokana na mvutano baina ya vyombo vya..

dola na ndugu wa marehemu.

Kelvin alifariki Aprili 28, mwaka huu na ndugu wa marehemu wanadai kifo chake kimetokana na kipigo cha polisi wakati akiwa mahabusu.

Kamanda wa Polisi Mkoa Morogoro, Wilbroad Mutafungwa, akizungumza na waandishi wa habari kutokana na sakata hilo, alisema ofisi yake imefungua jalada na kuanzisha uchunguzi unaoogozwa na Mkuu wa wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (RCO) wa mkoa huo.

Mutafungwa, alisema licha ya majibu ya kitabibu kutolewa, ameamua kuongeza nguvu kuwa suala hilo litashughulikiwa na RCO wa mkoa huo kwa kina zaidi.

Alisema, katika uchunguzi huo hawatamwonea mtu yeyote na hata ikibainika kuwa askari wake wamehusika na sheria zitachukua mkondo wake.

Akielezea tukio lilivyotokea, Mutafungwa alisema baada ya kupata malalamiko mengi juu ya tukio hilo, ameamua kwenda mjini Ifakara ili kuonana na ndugu wa marehemu licha ya suala hilo kuwa katika uchunguzi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, alisema Aprili 26, mwaka huu, mjini Ifakara zilipokelewa taarifa kuwa kijana mmoja alikamatwa na vijana wawili kwa tuhuma za kuwaibia waya wa kopa katika ofisi yao ya kununua vyuma chakavu.

Mutafungwa alisema baada ya kutuhumiwa alikamatwa na wenzie na kupelekwa umbali wa kilomita kadhaa na walipofika huko walimshambulia na baadaye kumvua nguo kwa madai ya kutaka kumlawiti.

Alisema siku iliyofuata April 27, kijana aliyeshambuliwa alitoa taarifa katika kituo cha polisi kwa madai ya kushambuliwa na vijana wawili na alipofika nyumbani alikutana na vijana hao wawili akiwamo marehemu kwa nia ya kuomba msamaha kwa kitendo walichokifanya siku ya nyuma.

Wakati wakiendelea kuomba msamaha walishangaa askari mgambo wakiwakamata na kudai wanahitajika polisi kwa makosa waliyoyafanya siku moja nyuma na kuchukuliwa na kupelekwa kituo cha polisi wilaya.

Kamanda Mutafungwa alisema siku iliyofuata ya Aprili 28, vijana wote wawili waliombewa dhamana na walifanikiwa kupata, lakini ilipofika usiku siku hiyo hiyo, walipata taarifa kuwa mmoja kati ya watuhumiwa amefariki dunia.

Alisema katika taarifa ya kifo hicho ndugu wa marehemu walidai kuwa ndugu yao amefariki baada ya kupigwa na polisi wakati akiwa mahabusu.

Kamanda huyo alibainisha kuwa, baada ya kuenea kwa taarifa hizo, jeshi la polisi liliamua kufungua jalada la uchunguzi ili kufahamu pale marehemu na mwenzake walipomchukua mtuhumiwa walienda kufanya nini na pia kujua marehemu na mwenzake walipokamatwa kuletwa kituoni walifanywa nini.

Alisema wanachunguza watuhumiwa wote wawili kipi kimewatokea wakati wakiwa mahabusu huku pia wakichunguza tabia za marehemu na ilikuwaje baada ya kutolewa kwa dhamana.

Kamanda huyo aliwaomba ndugu wa marehemu kama wana ushahidi wowote wapeleke kwa RCO na ataufanyia kazi na kuomba kuuchukua mwili kwaajili ya mazishi kwa kuwa uchunguzi wa kidaktari umeshafanyika na majibu yamepatikana na kinachosubiriwa sasa ni kubainika wahusika baada ya uchunguzi.

Kwa upande wa ndugu wa marehemu, Steven Marios ambae amejitambulisha kuwa babu wa marehemu, alidai mjukuu wao aliibiwa waya huo akiwa kazini na siku ya pili walikuja kuchukuliwa na mgambo na kupelekwa kituo cha polisi na siku ya tatu walipoenda kupeleka chai waliambiwa watuhumiwa hao wawili walipigwa sana wakati walipokuwa mahabusu.

Marios, alidai hata baba wa marehemu alipoenda kushughulikia suala la dhamana kwa mwanawe, alidai alipigwa na polisi na walipofanikiwa kumtoa Kelvin alikuwa anashindwa kutembea kutokana na kipigo

Babu huyo wa marehemu, alidai walimchukua Kelvin na kumpeleka hospitali ya Mt. Francis na alipofika alikimbizwa chumba cha uangalizi maalum (ICU), baada ya hali yake kuwa mbaya na ilipofika usiku alifariki dunia wakati akihangaikiwa kuongezewa damu.

Ndugu mwingine wa marehemu, aliyejitambulisha jina la Focus Mapondela, alidai kinachowashangaza ndugu yao alikuwa mzima wa afya wakati anakamatwa lakini alipotoka mahabusu alikuwa katika hali mbaya.

Mapondela, alisema wamepokea ushauri wa Kamanda huyo wa polisi kwa kumleta Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wana imani haki itatendeka na suala la kumzika marehemu watakaa kama familia kisha kutoa majibu na kutangaza siku ya maziko.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live