Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uchapaji wa jalada kesi ya Wayne Lotter wakwamisha kesi kuendelea

44067 Pic+kesi Uchapaji wa jalada kesi ya Wayne Lotter wakwamisha kesi kuendelea

Wed, 27 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Upande wa utetezi wa kesi ya mauaji ya mwanaharakati wa kupambana na ujangili, Wayne Lotter (52), inayowakabili washtakiwa 17, umehoji  uchapwaji wa jalada hilo umefikiwa hatua gani.

Hatua hiyo inatokana na upelelezi wa shauri hilo kukamilika na upande wa mashtaka, Februari 13, mwaka huu waliiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kuwa unasubiri jalada hilo lichapishwe kwa ajili ya taarifa muhimu.

Wakili wa Utetezi, Benedict Ishabakaki ameieleza Mahakama hiyo leo, Februari 27, 2019, mbele ya Hakimu Mfawidhi, Kelvin Mhina wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa na kuangalia kama upande wa mashtaka umekwisha kamilisha kazi ya uchapaji.

“Februari 13, mwaka huu upande wa mashtaka uliieleza mahakama hii kuwa upelelezi wa shauri hilo umekamilika unasubiri jalada hili lichapishwe kwa ajili ya taarifa muhimu, sasa leo nilitegemea waje waiambie Mahakama wamefikia hatua gani.

“Tunaomba kujua upande wa mashtaka wamefikia hatua gani katika uchapishaji wa jalada hili" alihoji Wakili wa utetezi.

Akijibu hoja hizo, Wakili wa Serikali, Wankyo Simon alidai kuwa wanasubiri  taarifa ya uchapaji wa kesi hiyo.

Simon alidai jalada lipo katika hatua za uchapaji na baada ya kumaliza Mahakama itapewa taarifa iweze kupanga tarehe kwa ajili ya kuwasomea washtakiwa maelezo ya mashahidi na vielelezo.

“Naomba niseme tu, nitafuatilia na tarehe ijayo nitakuja na majibu juu ya jalada hili kama limeshakamilika,” alidai Simon.

Hakimu Mhina baada ya kusikiliza hoja za pande zote,  aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 27, mwaka huu itakapotajwa.

Washtakiwa katika kesi hiyo ya mauaji Namba 19/2017 ni raia wawili wa  Burundi, ambao ni Nduimana Jonas (40) maarufu Mchungaji na bonimana Nyandwi.

Wengine ni Godfrey Salamba (42) mkazi wa Kinondoni Msisiri A, Inocent Kimaro (23) mkazi wa Temeke Mikoroshini, Chambie Ally (32) mkazi wa Kia/Boma na Ofisa wa benki ya NBC, Robert Mwaipyana (31) mkazi wa Temeke Mikoroshini.

Pia, washtakiwa wengine ni Meneja wa Benki ya Backlays, Khalid Mwinyi (33) mkazi wa Mikocheni B; Rahma Almas (37) mkazi wa Mbagala B;  Mohammed Maganga (61) ambaye ni mchimba makaburi;  Allan Mafue, Ismail Mohammed, Leornad Makoye, Amino Sham, Ayoub Selemani, Joseph Lukoa, Gaudence Matemu na Abuu Mkingie.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka mawili ambayo ni kula njama na kumuua mwanaharakati wa kupambana na ujangili.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kati ya Julai Mosi na Agosti 16, 2017 walikula njama ya kufanya mauaji ya Mkurugenzi na Mwanzilishi-Mwenza wa Shirika lisilo la kiserikali la PALMS Foundation, Wayne Lotter (52).

Katika shtaka la pili, washtakiwa hao wanadaiwa Agosti 16, 2017 katika makutano ya barabara za Chole na Haile Selasie iliyopo wilaya ya Kinondoni , wanadaiwa kumuua  Lotter, ambaye  alikuwa mwanaharakati wa kupambana na mauaji ya Tembo.



Chanzo: mwananchi.co.tz