Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ubovu wa basi wakwamisha kesi ya Maimu wa Nida

Tue, 30 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam.  Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Dickson Maimu na wenzake watano hawajafika  Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kusikiliza shauri linalowakabili ikielezwa kuwa basi la Magereza limeharibika.

Hayo yameelezwa leo Jumanne Aprili 30 katika Mahakama hiyo na upande wa mashtaka.

Maimu na wenzake wanakabiliwa na mashtaka 100, likiwamo la kuisababishia Serikali hasara ya Sh1.175 bilioni katika kesi ya uhujumu uchumi namba 7/2019.

Wakili  kutoka Takukuru, Leonard Swai  leo mbele ya Hakimu Mkazi, Salum Ally ameeleza kuwa, wamepewa taarifa na askari magereza kuwa basi linalowabeba washtakiwa hao kutoka gereza la Segerea kuelekea mahakamani hapo ni bovu.

Kutokana na hali hiyo Swai aliiomba Mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kesi hiyo kutajwa.

Hakimu Ally baada ya kusikiliza maelezo ya upande wa mashtaka aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 14 itakapotajwa tena.

Mbali na Maimu Washtakiwa wengine katika kesi hiyo  ni meneja biashara wa Nida, Aveln Momburi, mkurugenzi wa kampuni ya Aste Insurance Brokers,  Astery Ndege, ofisa usafirishaji, George Ntalima, mkurugenzi wa sheria, Sabina Raymond na Xavery Kayombo.

Kati ya mashtaka  yanayowakabili, 24 ni ya kutakatisha fedha,  23 ya kughushi,  43 ya kutumia nyaraka kwa lengo la  kumdanganya mwajiri na matano ya  kuisababishia hasara mamlaka hiyo.

Mengine ni mawili ya kula njama ya kulaghai, mawili ya matumizi mabaya ya madaraka na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na matumizi mabaya ya madaraka.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, kati ya Julai 19, 2011 na Agosti 31,2015 washtakiwa wakiwa maeneo tofauti jijini Dar es Salaam walikula njama ya kufanya udanganyifu wa Sh1.175 bilioni dhidi ya Nida.

Maimu na Raymond wanatuhumiwa Novemba 7, 2011 wakiwa makao makuu ya Nida Kinondoni,  walitumia madaraka yao vibaya na kusababisha  kampuni ya Gotham International Ltd kupata faida ya Sh899,935,494 isivyo halali.

Novemba 12, 2011 na Mei 12, 2015, Maimu na Momburi wakiwa makao makuu ya Nida, Kinondoni wanadaiwa walishindwa kusimamia ujenzi wa jengo lililopo ploti  namba 39A na hivyo kuisababishia  mamlaka hiyo hasara ya Sh 402,210,885.02.



Chanzo: mwananchi.co.tz