Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uandaaji taarifa kesi ya Nida uko hatua za mwisho

Wed, 3 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es salaam.Upande wa mashtaka katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili mkurugenzi mkuu wa zamani wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Dickson Maimu na wenzake, umeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa wako hatua za mwisho za uandaaji taarifa kwa ajili ya kuwasilisha Mahakama Kuu kitengo cha uhujumu uchumi.

Maimu na wenzake wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 7/2019 ya kuisababishia Serikali hasara ya Sh1.16 bilioni.

Wakili wa serikali Wankyo Saimon amedai leo Aprili 2, 2019 mbele ya Hakimu Mkazi, Salim Ally kuwa kesi hiyo imekuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi umekamilika, kinachofanyika ni mchakato wa ukamilishwaji wa taarifa kwa ajili ya kuwasilisha Mahakama Kuu.

Wakili wa utetezi, Joseph Ndunguru alidai upande wa mashtaka unatakiwa kueleza ni hatua gani hadi sasa wameshafikia na ni taratibu zipi zinazokwamisha ukamilishwaji wa taarifa hiyo.

Wakili Wankyo alidai kutokana na idadi ya makosa wanayoshtakiwa nayo ni vigumu kueleza ni muda gani watakamilisha taarifa hiyo ila inahitaji muda kutokana na wingi wa nyaraka zinazoandaliwa.

Baada ya maelezo hayo, Hakimu Ally aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 16, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni meneja biashara wa Nida, Aveln Momburi, mkurugenzi wa kampuni ya Aste Insurance Brokers, Astery Ndege, ofisa usafirishaji, George Ntalima, mkurugenzi wa sheria, Sabina Raymond.

Hata hivyo mshtakiwa wa kwanza Dickson Maimu, mshtakiwa wa pili Aveln Momburi na mshtakiwa wanne George Ntalima hawakufika mahakamani kutokana na taarifa iliyotolewa kuwa ni wagonjwa.

Awali washitakiwa hao walikuwa wakikabiliwa na mashtaka 26 likiwemo la uhujumu uchumi, ila Januari 28, 2019 waliachiwa huru na mahakama hiyo baada ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kusema hana nia ya kuendeleza mashtaka dhidi yao.

Hata hivyo baada ya washitakiwa kuondolewa mashtaka hayo na kuachiwa huru walikamatwa tena na walifikishwa katika mahakama hiyo kisha kusomewa mashtaka mapya 100 yakiwemo 25 ya utakatishaji fedha.  

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka 22 ya kughushi, mashtaka 43 ya kutumia nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri, mashtaka mawili ya kula njama, mashtaka 25 ya kutakatisha fedha na mashtaka matano ya kuisababishia hasara Nida.

Pia washitakiwa wanakabiliwa na mashitaka mawili ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na shtaka moja la matumizi mabaya ya madara lipo moja ambalo linamkabili  Maimu na Sabina. 

Katika mashitaka ya kwanza ya kula njama, Maimu, Ndege na Ntalima wanadaiwa, kati ya Julai 19, 2011 na Agosti 31, 2015 wakiwa maeneo tofauti tofauti ndani ya Jiji la Dar es Salaam walikula njama ya kufanya udanganyifu wa Sh 1.175 bilioni dhidi ya Nida.

Pia Maimu anadaiwa kutakatisha fedha kiasi cha Sh1,175,785,600.93 kati ya Julai 19, 2011 na Agosti 31, 2015 ambapo anadaiwa kujihusisha moja kwa moja kuhamisha fedha hizo huku akijua ni zao la kosa la kughushi.

Katika mashitaka mengine, Maimu na Raymond wanadaiwa Novemba 7, 2011 wakiwa makao makuu ya Nida, Kinondoni jijini Dar es Salama walitumia madaraka yao vibaya na kusababisha Chuo cha Sheria  (Law School) Dar es Salaam na Kampuni ya Gotham International Ltd kupata faida ya Sh899,935,494.

Inadaiwa kati ya Novemba 12, 2011 na Mei 12, 2015, Maimu na Momburi wakiwa makao makuu ya Nida, Kinondoni wakiwa ni mkurugenzi na meneja wa biashara walishindwa kusimamia ujenzi wa jengo lililopo ploti namba 39A na kuisababishia mamlaka hiyo hasara ya Sh402,210,885.02.

Katika kesi hiyo washtakiwa, Momburi na Raymond hawakupatikana na kosa la kutakatisha fedha hivyo mashtaka yao yanadhaminika, ila hadi Mahakama Kuu.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz