Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uamuzi mapingamizi kesi ya kina Mbowe Jumatatu

Mbowepic Uamuzi mapingamizi kesi ya kina Mbowe Jumatatu

Thu, 18 Nov 2021 Chanzo: mwananchidigital

Uamuzi wa mapingamizi katika kesi ya ugaidi inayomkabili mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu utatolewa Jumatatu Novemba 22, 2021.

Mapingamizi hayo matatu yaliwasilishwa jana Jumatano Novemba 17,2021 na jopo la mawakili wa upande wa utetezi likiongozwa na Peter Kibatala baada ya mahakama kutupilia mbali pingamizi waliotaka ushahidi wa shahidi wa Jamhuri aliyekutwa na diary ufutwe.

Mawakili hao wamepinga tena kitabu cha kumbukumbu ya mahabusu (DR) kutoka Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam kisipokewe mahakamani kama ushahidi.

Akitoa uamuzi leo Alhamisi Novemba 18, 2021 Jaji Joachim Tiganga amesema Jumatatu atatoa uamuzi wa mapingamizi hayo na kesi hiyo kuahirisha.

“Nimefanya tathimini na uwezekano wa kusema mpaka kesho asubuhi utakuwa ni mgumu. Badala yake tuje Jumatatu Novemba 22, 2021. Shahidi unaombwa kurudi Mahakamani. Washitakiwa wataendelea kuwa chini ya Magereza," amesema.

Ifuatayo ni sehemu ya mambo yaliyojili mahakamani hapo leo;

Wakili wa Serikali, Robert Kidando: Mheshimiwa Jaji, shauri limekuja kwa ajili ya kusikilizwa na jana tulikuwa tunajibu hoja za pingamizi na tupo tayari kuendelea na majibu ya hoja.

Wakili Peter Kibatala naye anasema wapo tayari kwa ruhusa ya Jaji.

Jaji: Bwana Hilla Karibu.

Wakili wa Serikali: Nizungumzie kidogo kuhusiana na hiyo Disposal Order (hii ni amri ya kukiachia kielelezo (kilichokwishapokewa Mahakamani), kutoka katika himaya/mikono ya mahakama. Kwamba hakuna another getaway ambapo kielelezo kinaweza kutoka.

Wakili Hilla: Mheshimiwa Jaji submission yetu ni kwamba kwa kuwa Mwendelezo wa kesi ni uleule economic namba 16, na kwa kuwa bado tuko kwenye proceeding na kwa kuwa kulikuwa hakuna maombi au sababu ya disposal.

Wakili Hilla: Hoja ya kwamba bado tupo kwenye kesi ile ile moja. Kinachotakiwa ni kuonyesha kwa Mahakama ni kwa namna gani kielelezo kilimfikia shahidi. Na zile sheria au kanuni zimefuatwa. Mheshimiwa Jaji, Chain of Custody imeelezwa vizuri kwenye ushahidi, Foundation ya namna kielelezo hiki kimemfikia shahidi kimelezwa vizuri Mheshimiwa Jaji.

Wakili Hilla: Nguvu za Naibu Msajili hasa kwenye mazingira ya kesi hii ambapo ndio kielelezo kinapotunzwa

Wakili Hilla: Mazingira ya kesi yetu yalivyo ni sahihi Msajili wa Mahakama kushughulika movement ya kielelezo. Deputy Registrar (Naibu Msajili) ndiye mtekelezaji wa amri za Mahakama. Kwa hivyo ni Mamlaka yake na jukumu lake kushughulika kielelezo kama alivyofanya. Ni wasilisho letu kwamba kama wenzetu wanakubaliana document ni authentic basi suala lingine halina nafasi.

Wakili Hilla: Naibu Msajili ndio mtelelezaji wa amri na ni mamlaka yake kutoa kielelezo kwa shahidi, bado kitabu cha kumbukumbu ya mahabusu (DR) ni muhimu kutumiwa.

Wakili Hilla: Tunaomba mapingamizi yatupiliwe mbali, kielelezo kiendelee na tuendelee na usikilizwaji wa shauri hili. Asante Mheshimiwa Jaji.

Jaji: Mmemaliza?

Wakili wa Serikali, Robert Kidando: Tumemaliza Mheshimiwa Jaji.

Anaamka Wakili Mtobesya.

Wakili Mtobesya: Naomba nisema vitu vinne ambavyo vitakuwa ni submission.

Mtobesya: Kwanza Mheshimiwa Jaji, ili kufanya Trial Within Trial ni lazima mahakama husika kwa muda isitishe proceedings za main Trial iingie kwenye zoezi la kufanya kesi ndogo.

Mtobesya: Halafu baadaye regardless ya matokeo ya kesi hiyo ndogo, mahakama husika itarejea kuendelea na kesi ya msingi. Kwa hiyo huo ni msingi wa kwanza.

Mtobesya: La pili Mheshimiwa Jaji, Trial within Trial. Proceedings za Trial within Trial, it's a factual exercise ambayo inalenga ku- achieve kitu kimoja tu, Ku- prove hoja ya mshitakiwa ambaye anakuwa under trial kwa kipindi hicho.

Mtobesya: La tatu kama ilivyo kwenye main Trial, mwenye jukumu la kutaka kuthibitisha kama yule aliteswa au la ni prosecutions, na kama ndiyo hivyo Mheshimiwa Jaji watatakiwa ku- lead evidence ku- prove na equally kwa mashitakiwa naye atatakiwa ku- lead evidence kama alitoa maelezo kwa hiari ama la. Kwa hiyo ni proceedings zinazojitegemea mheshimiwa Jaji.

Mtobesya: Nne Mheshimiwa Jaji, katika Economic Case ya 16 ya Mwaka 2021, mahakama hii ilishaingia ku- prove voluntariness ya mshitakiwa wa pili, Adam Kasekwa, na mahakama ikaja na maamuzi ya kinachotakiwa kufanywa kwenye statement ya mshitakiwa namba mbili.

Mtobesya: Nirudi sasa kwenye submission ya kuwajibu kaka zangu wasomi ni kwanini sisi tulidhani kwamba kwenye kesi hii kielelezo hiki ambacho mshitakiwa anaomba kukitoa kiliiingia kwenye kesi ya Trial Within Trial na kwamba kielelezo hiki kiliingia na mahakama ikafanya uamuzi wake.

Mtobesya: Kwanini sisi tulirejea kwenye kifungu namba 353(3) of CPA cap 20, tofauti na kaka yangu Chavula alivyokuwa anatafsiri. Kinasema kwamba Mahakama ikisharidhika, ni vyema ikatoa amri kwa kielelezo hicho kutoka, itafanya hivyo baada au wakati Mahakama ikiendelea. Labda nisome.

Mtobesya: Kwa hiyo sisi tulienda kwenye kifungu hiki tukijua kwamba kwa kuwa kielelezo hiki kilishatumika kwa kesi ya Adam Kasekwa, kwa kuwa kilishatumika kwenye different court proceedings, na kwamba kwa kuwa kilishaamriwa kwenye suala la hiari ya maelezo ya mshitakiwa wa pili, basi wao walipaswa wa- move Mahakama iweze kutoa kielelezo hicho.

Mtobesya: Sasa wenzetu hawakufanya hivyo Mheshimiwa Jaji. Sisi tuna- submit kwamba kuna hatua za kisheria wameziruka. Kwenye sehemu E sehemu CAP 20 ndiyo inahusu Disposal of Exhibit. Mheshimiwa Jaji haihitaji kuzunguka sana kuhusu hoja hiyo. Kitu kikishaingia mahakamani procedure yake ya kukitoa ni ile ile kama ilivyokiingiza. Hiyo ni 'court order.'

Mtobesya: Pia Mheshimiwa Jaji, kama kweli proceedings hizi ni sawa, kwanini wanaomba Mahakama ipokee tena kwa mara ya pili kwenye shauri hili kama proceedings zote ni sawa na kesi ni ile ile? Na kitendo cha wao kuomba ipokelewe tena na Mahakama ni ushahidi tosha kwamba hili ni shauri tofauti.

Mtobesya: Mheshimiwa Jaji, kwenye hilo naomba kuishia hapo. Atakuja kumalizia kaka yangu Kibatala kama kuna kitu sijataja. Sababu walizotoa kupinga mapingamizi yetu zinakosa mashiko. Hivyo tunaomba isizigatie kabisa hoja zao zisizo na mashiko.

Mtobesya: Kwa sababu hiyo naomba nimalizie hapo na nimuachie kaka yangu Peter Kibatala. Asante Mheshimiwa Jaji.

Anaamka Peter Kibatala.

Kibatala: Mheshimiwa Jaji kwa ruhusa yako naomba niendelee hapo ambapo kaka yangu Mtobesya amemalizia. Kwa kweli ni mazingira tofauti kabisa na kesi hii.

Kibatala: Mheshimiwa Jaji, nirudi kule kwenye Disposal Order kama nilimuelewa Mr Chavula kama sijamuelewa atanisamehe. Anasema hatujashambulia kielelezo (DR). Sasa kama hatujashambulia kielelezo tunafanya nini hapa?

Kibatala: Kwenye kifungu cha 353 hakuna kitu kinachofanyika kwenye Judiciary bila Order

Kibatala: Kama tulivyowasilisha, walikuwa na nafasi tangu mara ya kwanza, kwamba kama watakitumia walipaswa kuomba _Disposal Order._Wanajiwekea sheria zao wenyewe na kurekebisha vifungu.

Kibatala: Kama palikuwa na maamuzi ya Mahakama, ambapo maamuzi yakapelekea kupatikana kwa barua, hiyo haihalalishi kielelezo ambacho kimefika mahakamani bila Disposal Order. Hakuna sehemu hata moja Wakili wa Serikali ametoa sheria wala sheria kesi kwamba Naibu Msajili anaweza kumkabidhi mtu yoyote yule kielelezo cha Mahakama.

Kibatala: Wenzangu wanatumia uamuzi wako kwamba uliwafanya wafanye walichofanya. Hapana hakuna sehemu umesema Naibu Msajili aandike barua. Tunachojua mahakama ilitupilia mbali kielelezo. Na sasa wanacho bila kufuata sheria na Chain of Custody.

Kibatala: Hakuna mahala popote ambapo mahakama hii ilifanya Disposal Order na kwamba wao wanasema kwamba ni suala la utawala. Ni sheria ipi imesema kwamba Disposal Order ni suala la kiutawala? Mheshimiwa Jaji, pia wametaja kesi ya Gede Kondo yam waka 2017 kuhusiana na competence ya shahidi. Sasa shahidi mwenyewe hajafikia hata kwenye cross examination.

Kibatala: Na wamesema kwamba kwenye kesi ya Issa Tojo Mahakama haikutumia despite walitaja tu. Nani kasema?

(Peter Kibatala anasoma uamuzi wa kesi anayoirejea).

Kibatala: Kwamba Kanuni ya Estoppel inatajwa. Kama unazungumzia specific issues basi kanuni hii lazima itumike. Na kwamba tunawasilisha kwamba kesi hii ipo sahihi. Msomi Pius Hilla alisema kwamba admission ni kitu kimoja na disposal ni kitu kingine. Sisi tunasema pamoja na kanuni tatu za Relevance, Competence na Veracity lakini hakuna 'Paper Trade'.

Kibatala: Mheshimiwa Jaji, tunawasilisha kwamba kama hawakuomba Disposal Order hawawezi kupata exhibit. Wakiomba wanapata wala hakuna njia ya mkato hapo. Tunakazia mapingamizi yetu. Asante Mheshimiwa Jaji.

Jaji: Nimesikia hoja zenu. Ninajaribu kutafakari kabla sijaamua kupanga maamuzi yawe lini na saa ngapi. Ningeomba dakika kumi nifanye tathimini kisha nitarejea kusema uamuzi ni lini.

Jaji amerejea Mahakamani. Kesi namba 16 ya mwaka 2021 yA Jamhuri dhidi ya Khalfani Bwire, Adam Kasekwa, Mohammed Ling'wenya na Freeman Mbowe inatajwa tena.

Wakili wa Serikali: (Robert Kidando) Mheshimiwa Jaji upande wa mashtaka tupo wote isipokuwa Mr Pius Hilla alitoka kidogo.

Wakili Peter Kibatala: Mheshimiwa Jaji sisi quorum yetu ipo kama awali tupo tayari kusikiliza maamuzi.

Jaji: Nimefanya tathimini na uwezekano wa kusema mpaka kesho asubuhi utakuwa ni mgumu. Badala yake tuje Jumatatu ya tarehe 22 Novemba 2021. Shahidi unaombwa kurudi Mahakamani. Washitakiwa wataendelea kuwa Chini ya Magereza mpaka tarehe 22 Novemba 2021 Jumatatu saa tatu ssubuhi.

Chanzo: mwananchidigital