Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tumieni ofisi za kanda TLS kupeleka migogoro’

Ac227471270585de7ba5c2df33665891.jpeg Tumieni ofisi za kanda TLS kupeleka migogoro’

Fri, 4 Feb 2022 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Kanda ya Mzizima Dar es Salaam kimewataka Watanzania watumie ofisi za kanda zilizopo mikoa 21 kupeleka migogoro inayowakabili ili kupatiwa ufumbuzi kabla ya kuipeleka mahakamani au kwa viongozi wa serikali.

Mwenyekiti wa TLS kanda hiyo, Wakili James Malenga alitoa wito huo wakati wa kufungua mwaka mpya wa mahakama Dar es Salaam juzi.

Alisema kumekuwa na tabia ya wananchi kupeleka malalamiko kwa wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya kuhusu migogoro ya ardhi, mirathi na mikataba wakati changamoto hizo zinatatuliwa kisheria.

''Tumeanzisha chombo cha utatuzi wa migogoro kwenye jamii chenye hadhi ya kimataifa ili kutatua migogoro mbalimbali ikiwamo ya uwekezaji kusaidia nchi yetu kufikia uchumi wa kati kama inavyoelekezwa katika Dira ya Maendeleo ya Mwaka 2025,'' alisema Wakili Malenga na kuongeza:

''Tuna ofisi 21 mikoani ambazo hutoa huduma za usaidizi wa kisheria bure kwa watu ambao wana kesi mbalimbali mahakamani, kusaidia utatuzi wa migogoro na namna ya kufungua mashauri mahakamani.''

Alisema TLS wana mbinu za kutatua mashauri kwa kutumia njia mbadala, hivyo wananchi waitumie fursa hiyo kupata msaada wa kisheria.

Aidha, Wakili Malenga aliiomba serikali itumie mawakili wa ndani katika kusimamia kesi zinazofunguliwa dhidi yake, badala ya kutumia gharama kubwa kulipa mawakili wa nje.

Alisema TLS ina mawakili wenye utaalamu na ujuzi ambao serikali ikiwahitaji itapunguza gharama za uendeshaji wa kesi.

''Tunaomba serikali iweze kuunganisha kada hizi mbili za mawakili wa serikali na wa kujitegemea na kuwa kada moja ya wanasheria ili kusaidia katika ukuaji wa uchumi wa viwanda,'' alisema.

Wakili huyo alisema matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) yatasaidia kupunguza muda wa kusikiliza mashauri na yataongeza fursa katika uwekezaji baada ya mashauri hayo kumalizika kwa wakati.

Chanzo: www.habarileo.co.tz