Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tukio la kutekwa lilivyobadili ratiba yake ya maisha

68338 Pic+kutekwa

Fri, 26 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mei 25, mwaka huu saa 9 usiku katika eneo la Sedeko, mfanyabiashara wa nguo katika soko la Mugumu wilayani Serengeti Juma Siki (34), alitekwa na watu wasiojulikana na kumpora Sh5.09, wakachukua simu na kadi za benki kisha wakamshikilia eneo la siri wakishinikiza ndugu zake kutuma Sh15 milioni ndipo wamuachie.

Siku mbili baadae (Mei 27) usiku walimuachia kwa kumtelekeza eneo la machinjioni wilayani Bunda ambapo alisaidiwa na waendesha pikipiki (bodaboda) hadi Polisi ambako baadae alichukuliwa na polisi kutoka Serengeti kwa ajili ya uchunguzi.

Ikiwa imepita miezi miwili tangu alipotekwa, amezungumza na Mwananchi kuhusiana na maisha yake kwa sasa hasa baada ya tukio hilo lililokuwa gumzo katika mji wa Mugumu anakoishi.

Anasema kwanza haamini kama alibahatika kuachiwa huru akiwa salama katika tukio hilo kutokana na mazingira aliyopitia katika utekaji huo.

“Sijahama ninapoishi lakini tukio lile limenifanya kuwa na ratiba tofauti. Nimeongeza umakini, nalazimika kurudi nyumbani mapema na sasa simuamini yeyote kirahisi,” anasema na kuongeza;

“Nalazimika kuchukua hatua kwa ajili ya kujihami kwa kuwa mpaka sasa sifahamu ni watu gani walioniteka, ingawa miezi miwili imepita lakini sijaelezwa jambo lolote na polisi hivyo ni lazima nichukue tahadhari.”

Pia Soma

Kwa mujibu wa Siki, tangu alipotokewa na tukio hilo anahakikisha anamaliza shughuli zake mapema na kurejea nyumbani kujumuia na familia yake huku akisema kwa wageni wanaofika nyumbani kwake usiku ni lazima ajiridhishe kwelikweli kabla ya kufungua mlango na kumruhusu mtu kuingia ndani.

“Sasa tunamaliza miezi miwili sijaelezwa chochote, awali polisi waliahidi kuniita na kunijulisha walichobaini na kinachoendelea, nawasubiri wanieleze wamebaini nini,” anasema huku akisema amelazimika hata kuacha nyendo za usiku.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Juma Ndaki anasema hawana taarifa mpya kuhusiana na utekaji huo, ”hilo tukio lilikuwa na mambo mengi ndani yake, kwa kifupi hatujapata kitu chochote”.

Hata hivyo, alipoulizwa anamaanisha nini kuhusiana na taarifa yake alisema ”nilikuwa sijalifuatilia suala hilo kwa karibu ngoja nitawafuatilia wapelelezi kujua wamefikia wapi”.

Siki anasema “Katika maisha yangu nilijua wanaotekwa ni wenye fedha nyingi, wanasiasa na wanaharakati tena katika miji mikubwa sio kama hapa Mugumu”.

“Katika mazingira niliyotekwa nilijua sitapona maana kila mmoja alionyesha hatanii na watekaji walionekana kujipanga kufanya lolote, walisema wasipopata fedha walizotaka maisha yangu ni halali yao,” anasema.

Jinsi ilivyokuwa

Mei 25, mwaka huu majira ya mchana alipokea simu kutoka kwa mtu asiyemfahamu akimuuliza alipo na kumjibu yuko dukani, ”aliniliuliza wewe ndiye Juma nikakubali, hakuwa tayari kujitambulisha nami sikutilia shaka.”

Anasema jioni akapigiwa tena simu kwa namba nyingine tofauti na ile ya awali na kuulizwa maswali yale yale, hapo ilimfanya aingiwe na wasiwasi kutafutwa na mtu asiyemjua kwa namba tofauti.

Siki maarufu kama ‘Mzee wa Kubeti’ anadai jioni aliaga anakwenda kwenye sherehe akiwa na gari lake aina ya Toyota Noah, hata hivyo aliishia Wanyancha Pub kuangalia mechi ya mpira wa miguu kati ya Barcelona na Valencia huku akiendelea na vinywaji.

Alivyotekwa

“Nilitoka Pub saa 9 alfajiri katika mitaa yetu nilikuta Noah nyeusi namba zimefunikwa kwa kitambaa, nilistuka sana, nikaongeza mwendo kwenye kona nikakuta mawe mawili na chuma, nikalazimika kusimama ili nigeuze gari,” anasema.

Wakati anajaribu kukwepa mtego huo alijitokeza mtu mwenye bastola na kumtaka awe mtulivu, ghafla akajitokeza mwingine akiwa na panga aliyeingia garini na kumkaba, wakachukua kiasi hicho cha fedha alizotarajia kufuata mzigo jijini Mwanza.

“Walionyesha hawatanii, walidai ili kunusuru uhai wangu niwape fedha, niliposema sina nilipigwa ubapa wa panga, wakachukua kitabu cha benki, simu wakaanza kutuma ujumbe kwa watu ninaofahamiana nao wakitaka watumiwe fedha ndipo niachiwe.

“Baada ya kuhakikisha wanamiliki taarifa zangu za fedha walinihamishia kwenye gari lao akaongezeka mtu mwingine, katika purukushani hizo mmoja kofia iliyokuwa imeficha uso wake ilianguka nikamtambua lakini sijui kazi yake na anaishi wapi,” anasema.

Anasema alipigwa tena ubapa wa panga kichwani na kumchanganya kisha wakamfunga kitambaa usoni na kuondoka, njiani watu hao hakuwasikia kuzungumza zaidi ya kuwasiliana kwa ujumbe wa simu na baadae akapoteza fahamu.

Kufichwa na kuachiwa

Anasema alipopata fahamu alijikuta yuko kwenye chumba kidogo ambacho si rahisi hata kujigeuza, ndani kukiwa na mabati, nje kulikuwa na mtu ambaye alikuwa akimfuatilia na alipohitaji kujisaidia alimletea kopo.

Mei 27, usiku alitolewa katika chumba hicho akiwa amefungwa kitambaa na kuingizwa ndani ya gari bila kuongea na kuondoka mwendo wa zaidi ya saa moja ambapo baadae gari liliegeshwa, akatolewa, kutupwa chini na kumwacha mtu mmoja kama mlinzi.

“Gari liliondoka kwa kasi aliyebaki akanitaka nikae hivyo hivyo bila ya kugeuka. Baadae ilikuja bodaboda ikiwa imewasha taa kisha ikazima, nikamsikia akisema nikigeuka ananimaliza, kisha ikaondoka kwa kasi, nilikaa kwa muda ukimya ukatawala nikatoa kitambaa, nikabaini hakuna mtu,” anasema.

Anasema alisogea barabarani na kwa bahati akapita bodaboda akamsimamisha na kuomba msaada wa kupelekwa polisi Bunda ambako alijieleza na walipofuatilia waliambiwa ninatafutwa Serengeti.

Ingawa baadhi ya watu wanalihusisha tukio hilo na baadhi ya mambo ikiwamo masuala ya kimapenzi, lakini Siki anasema hana uhasama na wala kudaiwa na mtu yeyote.

Sisikwa Chacha aliyedai ni rafiki wa karibu wa Siki, anadai baada ya kupokea ujumbe kupitia simu yake kutakiwa atume Sh15 milioni ili rafiki yake aachiwe na kwamba ni mzima, alichanganyikiwa hasa alipokuwa akijaribu kupiga simu iliyomtumia ujumbe lakini ikawa haipatikani.

Chausiku Siki anadai kukata tamaa ya kukutana na mume wake akiwa hai kutokana na mazingira waliyokuta ndani ya gari lao, damu, kisu na kukosa mawasiliano naye.

Matukio mengine

Mwenyekiti wa Mtaa wa Sedeko Charles Chacha, anasema hilo ni tukio la tatu katika eneo hilo, kwanza mwaka jana mfanyabiashara maarufu Nyanswi Marwa alitekwa na watu wasiojulikana alipokuwa akiingia nyumbani kwake, wakamchoma visu na kusababisha kifo bila kuchukua kitu.

“Mwaka huu mwanzoni katika mji huo huo, Mahende Bahili alishambuliwa na watu wasiojulikana waliomvamia mjane wa Marwa muda baada ya kushuka ndani ya gari na kuanza kumkata kata kwa mapanga,” anadai.

Mwenyekiti huyo alisema Bahili alipojaribu kumsaidia mjane huyo ambaye mume wake aliuawa, ndipo alipogeuziwa kibao na yeye kushambuliwa.

Mganga mkuu wa hospitali ya Bunda DDH, Pendo Tafna anasema Siki alifikishwa hospitalini hapo na kupumzishwa akipatiwa matibabu, lakini baadae aliruhusiwa baada ya majeraha aliyoyapata kuonekana anaweza kwenda kujiuguza nyumbani.

Chanzo: mwananchi.co.tz