Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tuhuma rushwa ya ngono kwa mwanafunzi zamfikisha kortini mwalimu

89758 Ngono+pic Tuhuma rushwa ya ngono kwa mwanafunzi zamfikisha kortini mwalimu

Tue, 24 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) nchini Tanzania leo Jumatatu Desemba 23, 2019 imemfika mahakamani, mwalimu Baraka Sabi kwa kosa la kuomba rushwa ya ngono kwa mwanafunzi wake aliyemaliza kidato cha sita.

Sabi (41) ni Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Serengeti iliyopo wilayani Serengeti Mkoa wa Mara ambaye alikamatwa na Takukuru mwanzoni mwa Desemba 2019 mkoani Dodoma alipokuja kuhudhuria kikao cha wakuu wa shule na ilidaiwa alimtaka mlalamikaji aje Dodoma ili ampatie cheti cha kuhitimu masomo yake.

Mwendesha mashtaka wa Takukuru, Clarence Kimaro amedai mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Dodoma, Pascal Mayumba kwamba mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo Desemba 12, 2019 katika Hotel ya Pahi Jijini hapa.

Kimaro amedai mshtakiwa huyo alitenda kosa kinyume na kifungu cha sheria namba 15 cha makosa ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007.

“Mshtakiwa anashitakiwa chini ya kifungu namba 15 cha sheria namba 11 ya kuzuia na kupambana na rushwa nchini baada ya kuomba rushwa ya ngono kwa (Jina linahifadhiwa) ili ampatie cheti cha matokeo yake ya mtihani wa kidato cha sita,” amedai Kimaro.

Hata hivyo, mshtakiwa huyo alikana mashtaka yanayomkabili na alipewa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana. Alitakiwa kuwa na wadhamini wawili watakaosaini fungu la dhamana la Sh500,000 kila mmoja pia wawe ni wakazi wa Mkoa wa Dodoma.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Januari 10 mwakani baada ya  upande wa mashtaka kudai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

Mwanzoni mwa Desemba 2019, Mkuu wa Takukuru mkoa wa Dodoma, Sosthenes Kibwengo alisema  Desemba 12, 2019 walipokea taarifa kutoka kwa msichana (Jina limehifadhiwa) mkazi wa Dodoma aliyehitimu kidato cha sita katika shule hiyo.

Alisema baada ya kupokea taarifa hiyo walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo Sabi wakati akihudhuria kikao cha wakuu wa shule jijini hapa.

Kibwengo alisema mtoa taarifa aliwaambia kuwa baada ya kufika Dodoma ili kuchukua cheti chake mwalimu huyo alihitaji kupewa rushwa ya ngono ili atoe cheti ambapo mtoa taarifa aliomba udhuru na kuahidi kurejea siku iliyofuata

Chanzo: mwananchi.co.tz