Watu tisa wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza kwa tuhuma za mauaji ya Yumen Elias (54), mlinzi na mkazi wa Nyashishi.
Washtakiwa hao wamesomewa shtaka hilo katika kesi namba 2665/2024, leo Jumatatu, Februari 5, 2024, mbela ya Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Juma Mpuya.
Mwendesha mashtaka wa Serikali, George Ngemela amewataja washtakiwa hao ni Julias Joseph (22) mkazi wa Igoma, Paul John (23) mkazi wa Mwananchi, Leonidas Juma 9) mkazi wa Buhongwa na Abdallah Hassan (31) mkazi wa Nundu.
Wengine ni, Edward Bonface (19) mkazi wa Mahina, Mussa Robert (22) mkazi wa Ilemela Kanisan, Steven Emmanuel (18) mkazi wa Nyakato Sokoni, George Koloso (50) mfanyabiashara, mkazi wa Nyegezi, Charles Chacha (27) mkazi wa Mahina kati.
Ngemela amedai washtakiwa hao walitenda kosa hilo Januari 15, 2024 eneo la Mwananchi, Kata ya Mahina jijini Mwanza kwa kumuua Yumen Elias, kitendo ambacho ni kinyume na kifungu na 196 na 197 cha sheria ya kanuni na adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2022.
Washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama haina mamlaka kisheria ya kusikiliza kesi ya mauaji.
Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Juma Mpuya amesema kulingana na kosa hilo watuhumiwa hao hawatakiwi kupewa dhamana, hivyo kuahirsha kesi hadi Februari 20, 2024 itakapotajwa.