Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Timu ya DCI yatua Siha, utafiti sakata la mauaji

Timuupiiiccc Timu ya DCI yatua Siha, utafiti sakata la mauaji

Wed, 5 Oct 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati Jeshi la Polisi likianza uchunguzi, Sylvia Lyimo, mke wa mtuhumiwa wa mauaji, amesimulia namna nyumba yao ilivyoshika moto baada ya kulipuliwa na kitu kinachodaiwa ni bomu lililorushwa na Polisi wilayani Siha.

Lyimo alisema kuwa wakiwa ndani na mumewe saa 3 usiku wa kuamkia Septemba 27, 2022, alishtushwa na kishindo na alipokwenda sebuleni kuangalia alikutana na moshi unaowasha uliokuwa ukitoka katika kitu kama bomu.

Kabla ya nyumba yao kulipuka, Lyimo alidai kusikia milio ya risasi zilizokuwa zikifyatuliwa kutoka nje ya nyumba yao huku akidai alisikia pia milipuko ya mabomu manne yaliyorushwa ndani ya nyumba yao.

Katika purukushani hizo, inadaiwa koplo Wilfred Kavishe wa kituo cha Polisi Sanyajuu wilayani Siha mkoani Kilimanjaro, alijeruhiwa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali kinachodhaniwa kuwa ni panga.

Simulizi za mwanamke huyo ambaye ni mke wa mshukiwa wa mauaji ambaye polisi wamemtaja kuwa ni Pankrasi Shirima, imekuja wakati Jeshi la Polisi nchini limetuma timu ya makachero na wataalamu kuchunguza tukio hilo.

Taarifa iliyotolewa juzi jioni na msemaji wa jeshi hilo, David Misime ilisema tayari Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Camilius Wambura amemtuma mkurugenzi wa upelelezi wa makosa ya jinai (DCI), Ramadhani Kingai kuunda timu hiyo.

Katika taarifa hiyo, Misime alisema koplo Wilfred aliyejeruhiwa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali amelazwa hospitali na kushonwa nyuzi 12 huku mshukiwa huyo wa mauaji akifanikiwa kutoroka baada ya kumjeruhi askari.

“Mkurugenzi wa upelelezi wa makosa ya jinai atafanya uchunguzi wa nini kilichotokea na ukweli ukoje kutoka kwa waliokuwepo eneo la tukio,” alisema Misime na taarifa zilizopatikana jana, zilisema timu hiyo imetua Kilimanjaro.

DCI Kingai amethibitisha kutuma timu ya wataalamu ambayo tayari iko eneo la tukio kufanya uchunguzi wa kina na itafanya kazi kulingana na mazingira ya kazi yatakavyoelekeza.

“Tumetuma timu ya wataalamu kuchunguza tukio hilo na tayari ipo field (eneo la tukio), imeanza kazi kufuatilia jambo hilo na itafanya kazi kadri mazingira yatakavyoelekeza,” alisema Kingai bila kuingia kwa undani juu ya tukio hilo.

Pankrasi na watuhumiwa wengine katika kijiji hicho, wanadaiwa kuhusika na mauaji ya Serafini Mrama (39), aliyeuawa Septemba 15, 2022 kwa kushambuliwa na wananchi wakimtuhumu kumkata ng’ombe wa jirani yake mguu wa nyuma na kuondoka nao kwa ajili ya kitoweo.

Mke asimulia mwanzo mwisho

Akisimulia tukio hilo, Silvia Lyimo ambaye ni mke wa mtuhumiwa alieleza saa tatu usiku akiwa amelala na mumewe, alisikia vishindo na aliposhtuka kwenda dirishani alimuona mwenyekiti wa kijiji na askari saba.

“Nilishtuka nikanyanyuka nikaenda kuchungulia dirishani, nilionao askari saba na mwenyekiti wa kijiji, nikafungua pazia nikamuuliza mwenyekiti kulikoni akajibu ni msako wa yule kijana (aliyeuawa) kwa uhalifu wake.

“Mume wangu alitoka akaenda sebuleni mlangoni. Sasa nikaanza kusikia vishindo, mume wangu naye akarudi chumbani akikimbia na hakunisemesha chochote,” alieleza mwanamke huyo

“Nami nikaenda sebuleni kuchungulia ndipo nikaona moshi mkali unaowasha, nikamwambia mwenyekiti umekuja kushuhudia tufe, nikamsukumiza mtoto dirishani apate hewa maana moshi ulizidi,” alisema na kuongeza:

“Nikamwambia mwenyekiti kama mmeshindwa kunisaidia mimi na mume wangu acheni tufe, msaidieni huyu mtoto,” alisema na baada ya maneno hayo askari mmoja alipaza sauti akiwataka watoke ndani ya nyumba vinginevyo watakufa.

“Nikachungulia sebuleni moto umepamba na nikasikia milio kama ya bunduki na baadaye nikagundua kuwa ni mabomu na vishindo hivyo vilikuwa vinasikika sebuleni na walitupa mabomu matatu na moto ndio ukalipuka”

Hapo ndipo alimwambia mume wake watoke nje na alipofika nje hakumuona mumewe, ila anakumbuka kuona askari wa kike alimshika na mtoto moja kwa moja kwenye gari na hakujua kilichotokea wala hakujua mumewe alipita wapi.

“Sikuelewa kilichoendekea nyuma baada ya kuchukuliwa na yuke askari, ila nikiwa kituoni nilipata taarifa askari kajeruhuwa na tukiwa kwenye gari yule askari aliniuliza umeolewa na gaidi, nikamwambia hapana.

“Nimeachwa kama nilivyo, sina chochote vitu vyote vimeungulia ndani, fedha ya kikundi Sh1.3 milioni nilikopa nikanunue mahindi na vyote vimeungulia ndani. Huu ni ukatili, Serikali inisaidie maana watoto bado wanasoma,” alidai mama huyo.

Walichosema viongozi wa vijiji

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Naibili, Sabastiani Shirima ambaye ni ndugu wa mshukiwa aliyekuwa anasakwa, alisema alipigiwa simu na wananchi na kujulishwa kuna askari na viongozi wa kijiji wameenda kumkamata Pankras.

“Lakini ikatokea sintofahamu katika ukamataji na mdogo wangu alimjeruhi polisi kwa panga na kukimbia, huku mabomu ya machozi yakirushwa katika nyumba hiyo na vitu vya ndani viliungua ikiwamo magodoro, kitanda na tv,” alisema.

Mtendaji wa kijiji hicho, Melikiao Patrick alieleza alipigiwa simu na polisi saa 2 usiku kwamba walikuwa wanakwenda kijijini hapo, ndipo naye alimpigia mwenyekiti wa kijiji kumjulisha.

“Baada ya hapo tukiongona nao kwa baadhi ya nyumba na watuhumiwa walikamatwa, lakini tulipofika kwa Pankras, viongozi wa kijiji walijitambulisha na kutaka afungue mlango aligoma, ndipo askari alisukuma mlango na alikatwa na kitu chenye ncha kali kichwani na damu nyingi kutoka,” alisema.

Mtendaji hiyo alidai baada ya kuona damu nyingi zikimtoka askari huyo, yeye alikimbilia kwenye gari ya polisi na baada ya muda akaona moshi ukifuka kwenye nyumba hiyo, lakini hata hivyo mtuhumiwa alifanikiwa kutoroka.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live