Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Takururu na janga la rushwa ya ngono vyuoni

07c40e31a90f5ca256c7c121efd535b3 Takururu na janga la rushwa ya ngono vyuoni

Mon, 12 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

“KUNA mwanafunzi alimwandikia mhadhiri wa somo barua pepe na kumuomba amsaidie katika somo lake atamlipa chochote lakini sio pesa. Mhadhiri aliamua kuwashirikisha wanafunzi wengine na baadhi ya wahadhiri idarani… Aliwaasa wanafunzi wasome kwa bidii na kuzingatia maadili…”

Haya ni maneno ya baadhi ya ushuhuda wa rushwa ya ngono ulionukuliwa katika ripoti ya utafiti uliofanywa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru) katika vyuo vikuu viwili vya umma, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) mapema mwaka huu.

Malengo ya utafiti

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Takukuru ilifanya utafiti kwa lengo la kuwezesha upatikanaji wa taarifa za kisayansi zitakazosaidia kukabiliana na vitendo vya rushwa ya ngono katika taasisi za elimu ya juu nchini.

Taasisi hiyo imeeleza kuwa utafiti huo umefanyika katika vyuo vikuu kwa sababu Dira ya Taifa inadhamiria ifikapo mwaka 2025, Tanzania itakuwa ni nchi ya taifa la wasomi na wenye kupenda kujielimisha. Hivyo, tatizo au changamoto yoyote inayogusa sekta ya elimu itaathiri ufikiwaji wa moja ya malengo ya dira hii.

“Elimu ya juu ni kiwanda cha kuzalisha nguvu kazi ya taifa hivyo husaidia kukuza uchumi na kuwezesha nchi kufikia malengo yake ikiwa ni pamoja na kufikia uchumi wa viwanda.

“Hivi karibuni kumekuweko na malalamiko mengi kuhusu uwepo wa matukio ya rushwa za ngono kwenye taasisi za elimu ya juu, na hivyo utafiti huu utawezesha kubainisha kina cha tatizo, kwa nini hali hii, nini kifanyike na namna ya kulishughulikia suala hili,” inaeleza ripoti ya Takukuru.

Tafiti ililenga pia kupata taarifa za kina kuhusu kuwepo kwa tatizo la rushwa ya ngono; kuchunguza sababu za kuwepo vitendo vya rushwa ya ngono; kutathmini uwepo na ufanisi wa mifumo ya udhibiti wa ndani ya maadili juu ya vitendo vya rushwa ya ngono; na kutoa mapendekezo yatakayowezesha taasisi na serikali kwa jumla kupambana na kuzuia rushwa ya ngono kwenye taasisi za elimu ya juu.

Kwa nini UDSM na Udom?

Takukuru inasema imetumia vyuo hivyo, UDSM na Udom kwa sababu ni miongoni mwa vyuo vinavyomilikiwa na umma nchini na kudahili watu wemgi, hivyo kinadharia ni vyuo vinavyohitajika au vinavyotarajiwa kuwa mfano katika utawala bora.

“Aidha, kutokana na ukubwa wake na idadi kubwa ya wanafunzi nchini, utafiti uliona kuwa ni sehemu sahihi ya kuweza kuchunguza na kujenga msingi wa kisayansi kuhusu rushwa ya ngono nchini,” ilieleza ripoti.

Rushwa ya ngono ni nini

Rushwa ya ngono katika utafiti huo, inamaanisha matumizi mabaya ya madaraka ili kujinufaisha kingono isivyo halali. Rushwa ya ngono hugeuza haki na stahiki kuwa upendeleo. Aina hii ya rushwa haitumii fedha au vitu kushawishi ila hutumia nguvu ya kisaikolojia kumshawishi mhanga kutoa mwili wake kingono ili kufanya udanganyifu wa kitaaluma.

“Aidha, mhusika anayedai aina hii ya rushwa ni lazima awe na madaraka au mamlaka ambayo anaamua kuyatumia vibaya kwa kudai ngono ili atoe upendeleo kwa asiyestahili, au kumnyima haki anayestahili kwa kitendo cha kukataa rushwa ya ngono,” inaeleza sehemu ya ripoti ya utafiti wa Takukuru.

Rushwa ya ngono ipo

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kwa ujumla, utafiti umebaini kwamba tatizo la rushwa ya ngono kwenye vyuo vilivyoshiriki lipo na kwamba tatizo hili ni kubwa na si la kupuuzwa. Shuhuda za kutosha za waathiriwa wa rushwa ya ngono pamoja na shuhuda za uwepo wa watuhumiwa ambao hawajachukuliwa hatua zilitolewa.

Matokeo ya utafiti huo yameonesha zaidi ya asilimia 50 ya wahojiwa (wenye uelewa) walieleza uwepo wa rushwa ya ngono katika vyuo hivyo, hivyo kumaanisha kuwa rushwa ya ngono ni tatizo katika vyuo vikuu nchini.

Sababu ya kuwepo rushwa ya ngono

Sababu tano zimeelezwa kuwa chanzo ambazo ni ukosefu wa maadili, ushawishi wa mtu mwenye mamlaka, mfumo wa utoaji taarifa kutokuwa rafiki, mifumo dhaifu ya kushughulikia rushwa ya ngono na mamlaka ya kutoa alama za mitihani kuachwa chini ya walimu pekee.

Aidha, utafiti huo umebainisha kuwa vitendo vya rushwa ya ngono vinasababishwa ama na wanafunzi kulazimisha mapenzi ili wafaulu au wahadhiri huomba rushwa ya ngono ili kuwasaidia wanafunzi wafaulu.

Maombi mengine yanayochangia rushwa hii ni ya kupatiwa hosteli, kupatiwa ufadhili wa ndani na nje ya nchi na kupatiwa ajira.

Athari za rushwa ya ngono

Ripoti hiyo imeeleza kuwa kuna athari nyingi zinazotokana na rushwa ya ngono katika taasisi za elimu ya juu zikiwemo vyuo kuzalisha watendaji wenye uwezo mdogo kifikra; kuathiri utendaji wa taasisi; kudhalilisha utu wa mtu na kusababisha mtu kushindwa kujiamini na kuathiri saikolojia ya waathiriwa wa vitendo vya rushwa ya ngono.

Nyingine ni magonjwa ya kuambukiza kama Ukimwi; mimba zisizotarajiwa; kushusha morali ya utendaji kazi kwa watumishi; upendeleo kwa baadhi ya wanafunzi wanaotoa rushwa ya ngono; kuporomoka kwa maadili ya wanafunzi, wahadhiri na watumishi wasio wahadhiri na kuharibu taswira ya vyuo ndani na nje ya nchi.

Kwa upande mwingine, taarifa ikinukuu utafiti uliofanywa na Mukama (2017), rushwa ya ngono huvunja heshima ya mtu binafsi na taasisi.

Baadhi ya matukiona shuhuda

“Mwalimu alimtongoza mwanafunzi wa kigeni katika programu ya postgraduate, wakati wanafanya majadiliano ya Tasnifu (dissertation) yake. Mwalimu alianza kumshikashika, mwanafunzi alipiga kelele, baada ya taarifa kuenea, mwalimu huyo alipelekwa mafichoni kwa muda wa miaka mitatu na baadaye kurudishwa chuoni hapo,” ilieleza ripoti ya utafiti huo wa Takukuru.

Ripoti hiyo inabainisha kuwa pamoja na kuwepo kwa shuhuda za vitisho kwa watoa taarifa ambao ni waathiriwa au wahadhiri/watumishi wa vyuo husika pia zipo shuhuda zinazoonesha wanafunzi waliopendelewa na kupewa aidha ajira au kupewa udhamini wa masomo bila kustahili baada ya kutoa rushwa ya ngono.

Ushuhuda mwingine ulionukuliwa kwenye ripoti iyo ya utafiti ni huu: “Mwanafunzi alitakwa kingono na mhadhiri, akamkatalia. Baada ya kumkatalia mwanafunzi alianza kuona madhara yake kwa kuwekewa alama za chini…”

Nukuu nyingine: “Mhadhiri aliomba rushwa ya ngono kwa mwanafunzi aliyekuwa amefaulu mtihani wa majaribio (test) alikuwa amepata alama 84 lakini mhadhiri hakumrudishia karatasi yake ya mtihani na kumweleza kuwa amefeli mtihani na hivyo yuko tayari kumwongezea alama hadi zifike 84 iwapo atampa rushwa ya ngono.”

Kwa mujibu wa utafiti huo, mwanafunzi huyo alipoenda ofisini kwa mhadhiri alimkuta yuko na mhadhiri mwingine na alipoomba karatasi yake alikataliwa kwa madai kwamba yupo kwenye mazungumzo.

“Kwa bahati mhadhiri mwenzake bila kujua kinachoendelea alimshauri mhadhiri huyo amsikilize mwanafunzi, ndipo alipatiwa karatasi yake na kubaini kuwa alikuwa amefaulu kwa kupata alama 84,” inabainisha ripoti hiyo.

Ushuhuda mwingine uliobainishwa kwenye ripoti hiyo ni pamoja na kuwepo tabia ya baadhi ya wahadhiri kuwatongoza wanafunzi mapema wanapofika kuanza masomo chuoni kwa njia mbalimbali zikiwemo kuwapigia simu na kuwatumia ujumbe mfupi wa maneno kupitia simu za kiganjani.

“Wanafunzi wanapokataa wahadhiri hao huwatishia kuwa watahakikisha hawafaulu katika masomo wanayofundisha... Kuna wanafunzi walilalamika kwa uongozi wa chuo kutokana na kukataa kutoa rushwa ya ngono kwa mtuhumiwa na uongozi wa chuo ulielekeza usahihishaji wa somo hilo ufanyike upya na matokeo yalionesha kuwa wanafunzi hao walifaulu. Uongozi ulichukua hatua za kiutawala dhidi ya mtuhumiwa,” inasema ripoti.

Mbinu zinazotumiwa

Utafiti huo umebainisha kuwa mbinu inayoongoza kutumiwa na baadhi ya wahadhiri kushawishi wanafunzi watoe rushwa ya ngono ni tishio la kuwapa alama za chini kwenye mitihani, na vitisho vya kutofaulu kabisa masomo husika.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, watumishi 65 sawa na asilimia 29.9 na wanafunzi 174 sawa na asilimia 18.7, walieleza kuwepo kwa ushawishi wa makusudi ili kujipatia huduma kutoka kwa wenye mamlaka.

Takwimu za utafiti huo zinabainisha kuwa mbinu ya vitisho vya alama za chini kwa UDSM iliongoza kwa asilimia 40.5 na UDOM asilimia 38.6, vitisho vya kufeli mitihani ilifuatia kwa asilimia 28 UDSM na 31.1 UDOM.

Kwa mujibu wa utafiti huo, mbinu nyingine zinazotumika ni pamoja na ahadi ikiwemo ya kuolewa, cheo, chumba chuoni na nafasi ya uongozi.

Aidha, imebainika kuwa ushawishi wa makusudi kufanya ngono kufanyika ni asilimia 26.5 UDSM na 22.4 UDOM.

Aidha, utafiti huo ulibainisha mbinu nyingine zinazowaingiza mtegoni wanafunzi kwenye vyuo hivyo kuwa ni wahadhiri kuwaita wanafunzi kwenye mazingira yasiyo rasmi kwa ajili ya kukagua utafiti (research) inayofanyika kwa asilimia 3.9 UDSM na 7.5 UDOM.

Mbinu nyingine wanayotumia wahadhiri ni kujiunga kundi moja la whatsapp na wanafunzi, na imefahamika kuwa hilo kufanyika kwa 1.1% UDSM na asilimia 0.6 UDOM.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo utafiti unaeleza kuwa wahadhiri wanafahamu kwamba mwanafunzi anakuja chuoni kwa lengo kuu la kupata tuzo za kitaaluma hivyo hutumia mwanya huo kwa kuwapa alama ndogo za masomo, kubadilisha alama za ufaulu, kuwafelisha au kuzuia matokeo yao ili kuandaa mazingira ya kuwashawishi kingono.

Mapendekezo

Utafiti huo umetoa mapendekezo ili kupambana na tatizo la rushwa ya ngono ndani ya vyuo vya elimu ya juu na taasisi nyingine za umma na za sekta binafsi.

Kwa upande wa serikali, ripoti inapendekeza iuwajibishe uongozi wa vyuo vikuu kwenye kujenga mazingira wezeshi na salama kwa wanafunzi na wafanyakazi katika ngazi zote ili kuwezesha wanafunzi wa kike na kiume kupata haki ya elimu katika ngazi hii.

Pia iimarishe mifumo ya ajira ya wafanyakazi wote hususani wakufunzi na viongozi kwa kuwapa mafunzo ya ualimu na uongozi, uwajibikaji wa kuzingatia maadili ya kufundisha.

Huduma za utoaji wa elimu ikiwa ni pamoja na huduma za malazi kwa wanafunzi ziboreshwe ili kupunguza mianya inayotumiwa na wasimamizi na watoa huduma hizi kwa kuweka sharti la ngono kwa wanafunzi.

“Serikali isimamie uwajibikaji wa uongozi wa chuo kuhusu masuala ya jinsia na hususan rushwa ya ngono kwa kuwawajibisha viongozi ili waimarishe Kamati za Maadili ndani ya vyuo.”

Mapendekezio mengine ni kuijengea uwezo Takukuru katika kuchunguza na kumfikisha mtuhumiwa mahakamani bila kuhitaji kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka.

Serikali pia inashauriwa ifanye mapitio ya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11/2007 ili kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa ya ngono.

Kwa uongozi wa vyuo, ripoti imependekeza uboreshe mifumo ya udhibiti na uwajibikaji kwenye kuimarisha mifumo ya kusimamia maadili, mifumo ya utahini, mifumo ya kutoa taarifa na kulinda watoa taarifa pamoja na kuwajibisha watuhumiwa wa vitendo hivyo.

“Uimarishe taasisi na kamati zinazoshughulikia masuala ya maadili ya watumishi wake ikiwa ni pamoja na kamati za maadili, vitengo vya jinsia, ofisi ya mshauri wa wanafunzi kwa kuwapatia nyenzo, vitendea kazi na mafunzo ya kuwawezesha kushughulikia masuala ya rushwa ya ngono pamoja na unyanyasaji wa kijinsia kwenye vyuo,” anasema tarifa.

Vyuo pia vinashauriwa kuimarisha mahusiano na Takukuru kwenye kutoa elimu, kupeleleza na kuchukua hatua stahiki kwa watuhumiwa wa vitendo vya rushwa ya ngono.

Vyuo vijijengee uwezo na uelewa wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11/2007 kuhusu rushwa ya ngono ili wasimamie utekelezaji wake vyuoni; na kuwajengea wanafunzi na jamii yote ya chuo uelewa wa suala la rushwa ya ngono ili wajitetee na kupambana nalo.

Kwa asasi za kiraia, ripoti imependekeza kutumia taarifa hiyo ya utafiti kuimarisha vita dhidi ya rushwa ya ngono; kuendeleza na kuimarisha ubia kati yake na Takukuru kwenye vita dhidi ya rushwa ya ngono, hasa kwenye utafiti na elimu ya umma; na kujijengea uelewa wa pamoja wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa hususani vipengele vinavyoelezea rushwa ya ngono ili kuendeleza mapambano dhidi ya rushwa ya ngono.

Kwa wanafunzi wa vyuo, imependekezwa waongeze jitihada katika masomo, wazingatie maadili, wasikubali kurubuniwa, wavunje ukimya na kupaza sauti kunapotokea viashiria vya kuwanyima haki zao, na wachukue hatua stahiki pale wanapopokonywa hizo haki.

“Wadai kuimarishwa kwa mikakati iliyobainishwa katika miongozo na sheria ndogondogo za kuzuia na kudhibiti rushwa ya ngono; wafikishe malalamiko yao Takukuru kwa kupitia kamati zao, taasisi za kiraia na hata wao wenyewe; na waungane na kushiriki zaidi kwenye kampeni za kupambana na rushwa ya ngono,” inaeleza ripoti hiyo.

Chanzo: habarileo.co.tz