Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Takukuru yawakamata viongozi wawili kwa rushwa ya Sh20,000

74413 Takukuru+pic

Thu, 5 Sep 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kiteto. Mwenyekiti wa Baraza la ardhi Kata ya Bwawani wilayani Kiteto Mkoa wa Manyara, Steven Tollya na Katibu wake, Maiko Lemabi wanashikiliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa wakidaiwa kuomba rushwa ya Sh20,000 ya kufungua shauri.

Mkuu wa Takukuru wa mkoa wa Manyara, Fidelis Kalungura aliyasema hayo jana Jumatano Septemba 4, 2019 wakati akizungumzia kukamatwa kwa viongozi hao wawili.

Kalungura alisema viongozi hao walikamatwa kwenye kijiji hicho kwa nyakati tofauti baada ya kuomba rushwa kwa mwananchi ambaye jina lake linahifadhiwa.

Alisema watuhumiwa hao walimuagiza mwananchi huyo awape kiasi hicho baada ya Julai 22, 2019 kuwaeleza anataka kufungua shauri la ardhi kwenye baraza la ardhi la kata ya Bwawani.

Alisema watuhumiwa hao walimuomba mwananchi huyo Sh10,000 ya gharama halali ya kufungua shauri na Sh20,000 ili waweze kumfungulia shauri hilo.

"Baada ya kuambiwa hivyo Julai 24, 2019, mwananchi huyo alifika ofisi za Takukuru na kutoa taarifa ya kuombwa rushwa na watuhumiwa hao wawili ambao ni viongozi wa baraza la ardhi la kata hiyo," alisema Kalungura.

Pia Soma

Advertisement
Alisema baada ya kutoa taarifa hiyo waliandaa mtego kwa kuwatumia fedha hizo kwa njia ya Airtel Money ndipo wakamfungulia mwananchi huyo shauri hilo.

Alisema baada ya kufungua shauri hilo waliwakamata kwa nyakati tofauti na kuhojiwa kwenye ofisi za Takukuru kisha wakawapatia dhamana.

"Watuhumiwa hao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote taratibu za kisheria zitakapokamilika," alisema.

Alitoa wito kwa viongozi wa umma na wananchi wote wa Kiteto wajiepushe na vitendo vya rushwa na kufanya kazi kwa kuzingatia taratibu, kanuni na maadili ya kazi zao vinginevyo watakumbana na mkono wa sheria. 

 

Chanzo: mwananchi.co.tz