Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Takukuru yawachunguza Meya Moshi, Sabaya

7a11052209a11479475d49ac518c1d26.jpeg Takukuru yawachunguza Meya Moshi, Sabaya

Wed, 16 Jun 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Kilimanjaro imethibitisha kupokea tuhuma saba za kihalifu zinazowakabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai ole Sabaya na Meya wa Manispaa ya Moshi, Juma Raibu.

Akitoa taarifa hiyo kwa vyombo vya habari jana mjini Moshi, Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Kilimanjaro, Frida Wikes alisema uchunguzi wa tuhuma zilizoibuliwa dhidi ya Sabaya na Raibu zinaendelea kuchunguzwa.

“Kuna tuhuma mbalimbali za kihalifu zilizoibuliwa kuhusiana na Sabaya na Meya wa Manispaa ya Moshi Juma Raibu, uchunguzi unaendeleaj na ikithibitika tutawafikisha mahakamani,” alisema Wikes.

Alisema Sabaya alikwishafikishwa mahakamani mkoani Arusha kutokana na makosa aliyoyafanya akiwa mkoani humo na kulingana na uchunguzi unaoendelea mkoani Kilimanjaro ikithibitika atapandishwa mahakamani Kilimanjaro.

Aidha, alisema katika tuhuma saba zinazomkabili Sabaya na baadhi ya watu alioshirikiana nao katika kutenda uhalifu kwa wananchi ni Meya wa Manispaa ya Moshi.

“Kwenye tuhuma hizi wapo wengine wengi wanaotajwa kama Meya wa Manispaa ya Moshi kwamba walishirikiana naye kwenye uhalifu uchunguzi pia unaendelea dhidi yao ili haki iweze kutendeka na ikithibitika dhahiri bila shaka na wao watafikishwa mahakamani” alisema Kamanda wa Takukuru.

Aidha, alisema mpaka sasa taasisi hiyo inawashikiliwa watu kadhaa na kupokea baadhi ya ushahidi kutokana na tuhuma hizo na kwamba taarifa zaidi zitaendelea kutolewa.

Katika hatua nyingine, amewataka wananchi wa mkoa huo kujitokeza na kutoa malalamiko yao, ushauri na maoni juu ya taasisi hiyo ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha Wiki ya Utumishi wa Umma inayoanza leo hadi Juni 23, mwaka huu.

Chanzo: www.habarileo.co.tz