Dar es Salaam. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) leo Jumatatu Juni 10, 2019 imewataja askari polisi wawili na mtumishi mmoja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) waliohusika na ukamataji pamoja na uzuiaji wa mizigo wa mfanyabiashara Ramadhani Ntunzwe.
Takukuru imewataja watumishi hao ni Charity Ngalawa ambaye ni mwajiriwa wa TRA makao makuu, askari Polisi PC Simon Sungu pamoja na askari polisi PC Ramadhani Uweza wote wakitokea kituo cha Polisi Oysterbay jijini Dar es Salaam.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi mkuu wa Takukuru, Athuman Diwani imesema watumishi hao wanatuhumiwa kwa kosa la kuomba rushwa ya Sh2 milioni kutoka kwa mfanyabiashara huyo kinyume cha kifungu cha 15(1)(a) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na.11 ya 2007.
“Uchunguzi wa Takukuru umebaini kwamba, watuhumiwa hao waliomba kiasi hicho cha fedha kama kishawishi ili waweze kuachia mzigo wa mfanyabiashara huyo ambao waliukamata kwa madai ya kufanya udanganyifu wa kiwango cha bidhaa na hivyo kuathiri ukadiriaji wa kodi,” imesema CP Diwani.
Taarifa hiyo pia imesema kuna watuhumiwa wengine waliohusika kwa namna moja au nyingine katika suala hilo bado wanachunguzwa.
Mbali na watuhumiwa hao, Takukuru pia inawashikilia watumishi wanne wa TRA Mkoa wa Ilala Dar es Salaam wakichunguzwa kwa ukaguzi na ukadiriaji wa kodi walioufanya kwa bidhaa za mfanyabiashara Dilesh Solank ambaye ni mmiliki wa kampuni ya Sanaa ya Steps Entertainment.
Habari zinazohusiana na hii
- VIDEO: Mfanyabiashara aliyetajwa na Majaliwa adai hasara Sh800mil
- VIDEO: Hivi ndivyo mfanyabiashara aliyetajwa na Magufuli alivyowazungusha TRA, kugoma kuwapa rushwa
- VIDEO: Mfanyabiashara aliyegoma kuwapa rushwa TRA afunguka
- Rais Magufuli apigilia msumari wa mwisho ujenzi Bandari ya Bagamoyo
Kamishna Diwani pia amezungumzia madai ya unyanyaswaji na madai ya rushwa kwa wafanyakazi wa kiwanda cha Tumbaku Morogoro (Tanzania Leaf Tobacco Company) yanayodaiwa kufanywa na Polisi mkoani Morogoro.
“Tayari Takukuru makao makuu imeiongezea nguvu timu ya uchunguzi mkoani Morogoro ambayo ilikuwa imeshaanza kazi chini ya usimamizi wa ofisi ya mkuu wa Takukuru Mkoa. Uchunguzi dhidi ya tuhuma hii utakapokamilika tutatoa taarifa kamili,” amesema Diwani
Diwani amewataka wananchi kuunga mkono Rais John Magufuli katika mapambano ya rushwa na kuwa tayari kutoa ushahidi mahakamani katika kesi zinazochunguzwa na Takukuru.