Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Takukuru yarejesha nyumba iliyopokwa na mikopo umiza

Bd2f3280a8bd08c1d6f0f8d14e6d60d0 Takukuru yarejesha nyumba iliyopokwa na mikopo umiza

Sun, 17 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ( Takukuru) wilayani Kahama mkoani Shinyanga imerejesha nyumba ya familia ya Edward Mpolosi iliyokuwa imechukuliwa kinyume cha utaratibu na mfanyabiashara wa mkopo umiza, Masero Nyamhanga.

Kaimu mkuu wa Takukuru wilaya ya Kahama, Frank Masilamba aliwaambia waandishi wa habari jana kwamba utaratibu uliotumika kujimilikisha nyumba hiyo iliyokuwa katika kitalu J 165 mtaa wa Nyihogo haukuzingatia sheria.

Masilamba alisema kuwa nyumba hiyo inarejeshwa kwa familia ya marehemu Edward Mpolosi aliyechukua mkopo wa Sh 300,000 lakini alipochelewesha kulipa deni hilo liliongezeka riba hadi kufikia Sh milioni 10.5.

"Mkataba uliofanyika, sisi Takukuru tumechunguza na kuona ni batili kwa mauziano ya nyumba hiyo huku mkopeshaji akijua wazi kuwa alikuwa anatenda kosa kinyume na sheria za ukopaji "alisema Masilamba.

Masilimba alisema kuwa watoto wa marehemu walifika katika ofisi za Takukuru kueleza namna ya mkopo ulivyofanyika dhidi ya marehemu baba yao na mfanyabiashara huyo na kuona namna alivyodhulumiwa nyumba lakini walianza uchunguzi na kubaini kuwa makubaliano ya mauziano ya nyumba hiyo yalikuwa ni batili.

Mkuu wa wilaya ya Kahama, Anamringi Macha alisema kuwa serikali imeamua kuikabidhi nyumba hiyo kwa watoto wa marehemu ambao ni Rose na George waendelee kuimiliki baada ya mfanyabiashara ambaye alimkopesha fedha baba yao kukosa uhalali wa umiliki.

"Hatuta wavumilia wafanyabiashara wanaotumia fedha zao kunyanyasa wananchi wanyonge kwa kuwakopesha mikopo umiza ambayo imekuwa ikiendelea kupoka haki za watu wengine na tutaendelea kuwakamata nakuwachukulia hatua pindi tukiwabaini"alisema Macha.

Rose Edward ambaye alikabidhiwa nyumba hiyo na mkuu wa wilaya alishukuru serikali kwa hatua hiyo.

Chanzo: habarileo.co.tz