Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Takukuru yarejesha mil 125/- vyama vya akiba na mikopo

Aa10cfcc279cbb4441bc5add1ee02bc8 Fedha

Fri, 17 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

TUME ya Maendeleo Ushirika Tanzania (TCDC) imepongeza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kurejesha Sh milioni 125.3 katika vyama vya Akiba na Mikopo (SACCOS) zilizokusanywa kwa wadaiwa sugu katika vyama hivyo.

Kati ya fedha hizo, Sh milioni 73.4 zilirudishwa kwenye akaunti ya Saccos ya Mipango na Sh milioni 51.9 zilirudishwa katika akaunti ya Saccos ya Majengo za jijini Dodoma.

Akizungumza katika kikao cha pamoja kati ya TCDC na Takukuru, Mrajisi wa Vyama vya Ushirika, Dk Benson Ndiege aliipongeza Takukuru kwa kurejesha fedha zilizochukuliwa bila kufuata sheria na kuzirudisha kwenye akaunti za Saccos husika kwa maelekezo ya Mrajisi Msaizidi wa Mkoa wa Dodoma.

“Kazi iliyofanywa na Takukuru katika urejeshaji wa fedha kwenye vyama vya ushirika zilizokuwa zimechukuliwa bila kufuata utaratibu imewezesha kutoa ujumbe mahususi kuwa fedha na mali za wanaushirika hazitakiwi kuchezewa,”alisema.

Katika kikao hicho, Takukuru iliwasilisha taarifa ya uchunguzi na fedha zilizokusanywa na taasisi hiyo kwa niaba ya vyama vya ushirika nchi nzima baada ya kukabidhiwa kazi hiyo na Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga. Dk Ndiege alisema TCDC wataendelea kushirikiana na Takukuru katika kuhakikisha kuwa mali za wanachama wa vyama vya ushirika zinalindwa na kuwanufaisha wananchi.

Pia alisema warajis wasaidizi wa vyama vya ushirika wa mikoa na maofisa ushirika wa wilaya wataendelea kushirikiana na maofisa wa Takukuru katika maeneo yao ili kulinda mali za wanaushirika.

Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, John Mbungo alipongeza ushirikiano uliotolewa na TCDC kwa taasisi hiyo wakati wakitekeleza maagizo ya viongozi serikali katika urejeshaji wa fedha kwenye vyama vya ushirika zilizokuwa zimechukuliwa bila kufuata utaratibu.

“Tuleteeni matatizo na changamoto zinazohusu ubadhirifu unaofanywa na baadhi ya watu wanaoviibia vyama vya ushirika ili tushughulike nao na kuhakisha kuwa mali za wanaushirika zinakuwa salama,” alisema.

Katika kikao hicho TCDC ilikutana na Takukuru kwa lengo la kuimarisha usimamizi na maendeleo ya vyama vya ushirika nchini.

Chanzo: habarileo.co.tz