Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Takukuru yaondoa tisa ardhi Dodoma

94687 Takukuru+pic Takukuru yaondoa tisa ardhi Dodoma

Thu, 6 Feb 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa nchini (Takukuru) mkoa wa Dodoma, imesema mapambano ya rushwa kwenye sekta ya ardhi mkoani hapa imesababisha vigogo tisa wa idara ya ardhi kuchukuliwa hatua za nidhamu.

Akizungumza na Mwananchi jana mkuu wa uelimishaji Takukuru mkoa wa Dodoma, Faustine Malecha alisema idara ya ardhi ilikuwa imejaa rushwa kutokana na wananchi kutokuwa na hati miliki ya ardhi kwa sababu ardhi yote ilimilikiwa na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA).

Malecha alisema kukosekana kwa hati miliki za ardhi kwa wenyeji kulisababisha wenyeviti wa serikali za vijiji, mitaa na watendaji kata kuuza ardhi holela baada ya CDA kuvunjwa.

“Sekta ya ardhi ilikuwa imejaa rushwa kutokana na baadhi ya watumishi wa sekta hiyo kushirikiana na baadhi ya viongozi wa kata, mitaa na vijiji kuuza ardhi ya wenyeji bila kufuata utaratibu,” alisema Malecha na kuongeza:

“Hilo limesababisha watumishi tisa wa sekta ya ardhi Jiji la Dodoma kuchukuliwa hatua za nidhamu ikiwamo kushushwa vyeo, kufukuzwa kazi na wengine kupangiwa vituo vingine vya kazi ili kuhakikisha mapambano dhidi ya rushwa yanaendelea hata huko walikopelekwa.”

Alisema kulikuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi dhidi ya watumishi hao, hivyo japo hawakukutwa na ushahidi wa moja kwa moja lakini walionekana kuhusika na kuwatapeli wa ardhi ndiyo maana wakachukuliwa hatua za nidhamu.

Pia Soma

Advertisement
Alisema mbali na hilo, Takukuru imeanzisha dawati la kuzuia rushwa (Utafiti) ambalo lina jukumu la kugundua na kuzuia mianya mipya ya rushwa, namna ya kuziba mianya hiyo kwenye idara ya ardhi ili kuboresha huduma na kuondoa malalamiko ya vitendo vya rushwa kwa kuongeza uwazi kwenye utendaji wao.

Mkazi wa mjini hapa, Fausta Cyril alisema kuna mila na desturi ambazo huchochea vitendo vya rushwa hasa kwenye mikoa yenye viwango vikubwa vya rushwa ikiwamo Dodoma, Mwanza na Shinyanga.

Fausta alisema wenyeji wa mikoa hiyo wana desturi ya kutoa zawadi wanapopewa huduma nzuri hata kama ni hospitali bila kuombwa.

“Ni utamaduni wao kwamba kama wanaumwa wakatibiwa vizuri na kupona huwa wanatoa zawadi kwa nesi au daktari aliyewahudumia bila kujua abia hiyo ikizoeleka kwa watoa huduma huwa hawatimizi wajibu wao mpaka wapewe zawadi, hiyo nayo ni rushwa japo inaonekana kama ni zawadi kwa walengwa,” alisema.

Chanzo: mwananchi.co.tz