Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Takukuru yaokoa mil 23/- Temeke, Kigamboni

8147d57e8028a094c1dea1f56fa66dbe.jpeg Takukuru yaokoa mil 23/- Temeke, Kigamboni

Thu, 21 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Temeke imeokoa zaidi ya Sh milioni 23 kutokana na uchunguzi ilioufanya katika wilaya za Temeke na Kigamboni kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia Oktoba hadi Desemba mwaka jana.

Taasisi hiyo pia imepokea taarifa 137 zinazohusu vitendo vya rushwa huku idara za ardhi za halmashauri ya Manispaa ya Temeke na Kigamboni pamoja na taasisi binafsi zikiongoza kwa kulalamikiwa kwa kutenda makosa hayo.

Akizunguza jijini Dar es Salaam jana, Mkuu wa Takukuru wa mkoa huo, Donasian Kessy, alisema makosa yanayohusiana na rushwa katika mkoa huo yameendelea kupungua ikilinganishwa na kipindi cha miezi mitatu nyuma.

Alisema katika kipindi hicho cha Oktoba hadi Desemba, Takukuru Mkoa huo pia imeweza kufungua kesi mpya nne katika mahakama za Temeke na Kigamboni ikiwemo ya ubadhirifu wa fedha kiasi cha Sh Milioni 37.6 iliyomuhusu Anna Michael aliyekuwa mweka hazina wa kikundi cha Ebeneza.

Alisema miongoni mwa kesi hizo nne mpya, wameshinda kesi mbili ikiwemo kesi Na CC/4/2019 iliyofunguliwa Mahakama ya Wilaya ya Temeke inayowahusu Yusuph Aruna, Daniel Julius na Denis Palike ambao ni maafisa mazingira wa kujitolea wa manispaa ya Ilala na kesi Na CC/80/2020 inayomhusu Mwajuma Fadhil Mohamed mshauri wa mahakama ya Mwanzo Kigamboni.

“Mbali na hilo, kupitia dawati la kuzuia rushwa chini ya Takukuru tumefanya chambuzi za mifumo miwili kwa lengo la kubainisha mianya ya rushwa kisha kuidhibiti kwa kutoa ushauri na mapendekezo kwa mamlaka zinazohusika ili kuongeza uwajibikaji” alisema Kessy

Aidha Mkuu huyo wa Takukuru Mkoa wa Temeke alizungumzia mikakati ya taasisi hiyo katika kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu kuwa ni pamoja na kudhibiti vitendo vya rushwa katika mkoa huo ikiwa ni pamoja na kuangalia njia bora ya kuweza kutokomeza rushwa katika miradi mbalimbali ikiwemo ya ujenzi wa miundombinu.

Chanzo: habarileo.co.tz