Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Takukuru ‘yanusa madudu’ ujenzi jengo la X-Ray

6048e13453be5b807699ed37c7d67f46 Takukuru ‘yanusa madudu’ ujenzi jengo la X-Ray

Thu, 22 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, imesimamisha ujenzi wa jengo la X Ray katika Kituo cha Afya cha Bugarama kilichopo katika Halmashauri ya Msalala, mkoani humo, baada ya kubaini uwepo wa matofali zaidi ya 3,000 yasiyo na ubora.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Takukuru wilayani Kahama, matofali hayo yalipelekwa kwa ajili ya ujenzi wa jengo hilo na mzabuni aliyejulikana kwa jina la Block Traders.

Taarifa hiyo ilisema Aprili 4, mwaka katika kutekeleza majukumu yake, Takukuru ilitembelea mradi wa ujenzi wa jengo la X Ray katika Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama ambapo mpaka litakapokamilika jingo hilo litagharimu Sh milioni 53.

Kwa mujibu wa taasisi hiyo, ujenzi huo ni mwendelezo wa majengo yaliyojengwa katika kituo hicho cha afya tangu mwaka 2016 kwa ufadhili wa Mgodi wa Bulynhulu chini ya utaratibu wa urejeshaji kwa jamii unaofanywa na mgodi huo.

“Takukuru katika kufuatilia ilishirikiana na Mhandishi wa Ujenzi wa Halmashauri ya Msalala na kubaini uwepo wa matofali zaidi ya 3,000 yasiyo na ubora yaliyopelekwa na Mzabuni anayejulikana kwa jina la Block Traders,” ilibainisha taarifa hiyo.

Ilisema baada ya maofisa wa Takukuru na Mhandisi wa ujenzi kufanya ukaguzi na kujiridhisha kuwa matofali hayo hayana ubora, Mkuu wa Takukuru Wilaya ya Kahama Abdullah Urari alitoa maelekezo ya kusitshwa kwa ujenzi uliokuwa unaendelea na kusimamisha malipo kwa mzabuni huyo.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa mahojiano ya mafundi yaliyofanyika katika eneo hilo, pia yalithibitisha kutokuwepo kwa ubora wa matofali hayo kwani mafundi hao walieleza kuwa hata wao walihoji ubora wa matofali hayo ingawa walipewa maelekezo ya kuendelea kujenga.

“Kutokana na kubaini kuwa matofali haya yaliyoletwa na mzabuni kutokuwa na ubora, naelekeza kuwa ujenzi huu usimame mpaka pale maelekezo mengine yatakapotolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Msalala,” alisisitiza Urari kupitia taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo ya Msalala, Simon Berege baada ya kupewa taarifa ya tukio hilo kwa njia ya simu na Ofisa wa Takukuru, alitoa maelekezo mzabuni husika aondoe matofali hayo haraka na taratibu nyingine za manunuzi zifanyike ili kumpata mzabuni mwingine.

Chanzo: www.habarileo.co.tz