Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Takukuru yamnasa Hanspoppe Uwanja wa Ndege Dar

22427 Takukuru+pic TanzaniaWeb

Tue, 16 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Baada ya kumsaka kwa muda mrefu, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imemkamata mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya klabu ya Simba, Zacharia Hanspoppe.

Takukuru imemkamata Hanspoppe baada ya kumtangaza katika vyombo vya habari na kumtaka aripoti katika ofisi zake ili kujibu tuhuma zinazomkabili.

Hanspoppe alikamatwa juzi baada ya kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), saa 8.59 mchana akitokea Dubai.

Akizungumzia kukamatwa kwa mfanyabiashara huyo maarufu, naibu mkurugenzi mkuu wa Takukuru, Brigedia Jenerali John Mbungo alisema, “Ni kweli amekamatwa, alikamatiwa uwanja wa ndege mara tu alipowasili.”

Alisema walipata taarifa kwamba Hanspoppe anakuja nchini na wakawasiliana na watendaji wa Idara ya Uhamiaji.

“Na vijana wetu wakawepo pale wanamsubiri na alipofika tu wakamkamata. Hanspoppe ataunganishwa moja kwa moja mahakamani kesho (leo).”

Pamoja na Hanspoppe mwingine aliyekuwa anatafutwa na Takukuru ni Franklin Lauwo ambaye naibu mkurugenzi huyo wa Takukuru alilieleza Mwananchi kuwa amekwishawasiliana nao na kudai atajisalimisha mwenyewe mara baada ya kurejea nchini akitokea Pakistan.

Hanspoppe ataunganishwa katika kesi inayomkabili rais wa Simba, Evans Aveva na makamu wake, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ ya madai ya kughushi na utakatishaji fedha ambayo inaendelea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.

Hanspoppe amekamatwa zikiwa zimepita siku 30 tangu Takukuru ilipojitokeza mbele ya waandishi wa habari kumtaka yeye na Lauwo wajisalimishe huku wakitangaza dau kwa yeyote ambaye atafanikisha kukamatwa kwao.

Septemba 14, Mbungo akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya taasisi hiyo Upanga, alisema Hanspoppe alitoa taarifa za uongo kuhusu malipo ya kodi.

Alisema mfanyabiashara huyo kwa kushirikiana na Aveva na Kaburu walitoa maelezo ya uongo kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambazo zilihusu klabu ya Simba kwamba imenunua nyasi bandia kutoka Kampuni ya Ninah Guangzhou Trading zenye thamani ya Dola 40,577 za Marekani, maelezo ambayo alidai kuwa yalikuwa ya uongo kwani nyasi hizo zilinunuliwa kwa Dola 109,499.

Kuhusu Lauwo, Mbungo alisema alifanya kazi ya ukandarasi wa ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu wa Simba uliopo Bunju, Kinondoni jijini Dar es Salaam kwa Sh249, 929,704 wakati akiwa hajasajiliwa katika Bodi ya Makandarasi Tanzania.

“Tumewatafuta kwa njia za siri na uwazi bila mafanikio. Tunawataka kuripoti kituo cha Takukuru au polisi,” alisema siku hiyo alipotangaza zawadi nono kwa yeyote ambaye angefanikisha kupatikana kwao.

Oktoba 3, katika kesi inayoendelea ya Aveva na Kaburu, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilisema si muda muafaka wa kuifuta kwa sababu ilishafikia hatua ya kusomwa maelezo ya awali.

Uamuzi huo ulitolewa na Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Thomas Simba baada ya mawakili wa washtakiwa hao wakiongozwa na Nehemia Nkoko kuitaka ifute kesi hiyo kwa sababu upande wa mashtaka wameshindwa kuiendesha.

Hakimu Simba alisema mbali na kutoifuta, mahakama hiyo ilitoa siku 14 kwa upande wa mashtaka kutekeleza amri iliyoitoa ya kuutaka upande huo aidha wawafutie mashtaka Hanspoppe na Lauwo au wabadilishe hati ya mashtaka kwa kuwaondoa washtakiwa hao ili kesi isikilizwe.

“Nimepitia hoja zote zilizotolewa na pande zote na kuona kuwa sio muda muafaka wa kufuta kesi hiyo kwa sababu tayari ilikuwa katika hatua ya washtakiwa kusomewa maelezo ya awali (PH) na pia ilishatoa amri na bado haijatekelezwa” alisema.

Hakimu alisema upande wa mashtaka wanatakiwa watekeleze amri iliyotolewa Mei 12, 20018.

“Hivyo, mahakama haiwezi kufuta kesi hiyo kwa sababu itafuta hadi amri ambayo tayari alishaitoa na haijatekelezeka.”

Alisema kutokana na sababu hiyo anatoa siku 14 kuanzia Oktoba 4 kwa upande wa mashtaka ili waweze kufanya mabadiliko na kama hawatafanya hivyo, mahakama inaweza kuamua vingine itakavyoona inafaa.

Hakimu Simba alitaka amri hiyo itekelezeke kwa sababu hawajui ni lini Hanspoppe na Lauwo watakamatwa wakati Aveva na Kaburu wakiendelea kusota mahabusu.

Baada ya kueleza hayo, hakimu alisema washtakiwa watasomewa maelezo ya awali Oktoba 16, ambayo ni leo.

Hii ina maana kuwa Hanpoppe anaweza kuonekana mahakamani hapo leo na kuunganishwa na wenzake katika kesi hiyo.

Chanzo: mwananchi.co.tz