Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Takukuru yamhoji DED, yawashirikia watumishi wawili Mara

89413 TAKUKURU+PIC Takukuru yamhoji DED, yawashirikia watumishi wawili Mara

Fri, 20 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Musoma.  Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Mara nchini Tanzania inawashikilia watumishi wawili wa halmashauri ya wilaya ya Bunda vijijini mkoani Mara huku ikiendelea kumuhoji mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo (DED), Amos Kusaja kwa tuhuma za upotevu wa zaidi ya Sh500 milioni zilizotolewa kwaajili ya ujenzi wa hospitali ya halmashauri.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Desemba 20, 2019, mkuu wa Takukuru mkoa wa Mara, Alex Kuhanda amewataja watumishi wanaoshikiliwa ni Mweka hazina, Castro Maokola na Ofisa Ugavi, Emmanuel Mboje.

Kuhanda amesema watu hao wanashikiliwa na taasisi yake kufuatia uchunguzi ulioanza kufanywa juu ya matumizi ya Sh1.5 bilioni zilizotolewa kwaajili ya ujenzi wa hospitali ya halmashauri hiyo.

Amesema baada ya kuanza uchunguzi wamegundua tayari halmashauri hiyo imekwisha tumia zaidi ya Sh1.2 bilioni na kwamba nyaraka zilizowasilishwa zinaonyesha matumizi ya Sh700 milioni huku zikikosekana nyaraka za matumizi ya Sh500 milioni.

Amesema wamebaini kuwapo kwa matumizi ya Sh4.2 milioni zilizolipwa na mkurugenzi wa  halmashauri hiyo kwa mhandisi ambaye alitakiwa kusimamia ujenzi wa hospitali hiyo ingawa hakuwahi kusimamia ujenzi huo.

Kutokana na hali hiyo, Kuhanda amesema amemtaka mkurugenzi pamoja na mhandisi huyo kurejesha fedha hizo ofisini kwake Desemba 23, 2019.

 Amesema kufuatia uchunguzi walioufanya pia wamebaini licha ya kuwapo kwa nyaraka zinazoonyesha matumizi ya Sh700 milioni lakini kazi iliyofanyika kwenye mradi huo hailingani na thamani ya fedha iliyokwishatumika huku akiongeza fedha iliyobaki haiwezi kukamilisha kazi iliyobaki.

Desemba 17, 2019 Mkuu wa mkoa wa Mara, Adam Malima aliitisha kikao cha dharura cha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya kuijadili halmashauri ya wilaya ya Bunda kwa madai ya kushindwa kukamilisha hospitali hiyo kwa wakati.

Malima alisema hospitali hiyo iliyoanza kujengwa Februari 2019 ilitarajiwa kukamilika Juni 2019 lakini hadi sasa haijakamilika kutokana na madai ya kuwa Mkurugenzi amekuwa akikwamisha ujenzi huo kutokana na kutotoa fedha kwaajili  ya manunuzi ya vifaa pamoja na malipo ya mafundi kwa wakati.

Chanzo: mwananchi.co.tz