Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Takukuru yajitosa rushwa ya trafiki

7ae39def4a5e980f1439b9f49b9883f2.jpeg Takukuru yajitosa rushwa ya trafiki

Mon, 26 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MKURUGENZI Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), John Mbungo amesema wameunganisha nguvu kupambana na rushwa kwa askari Polisi kwa kuanzisha ushirikiano wa utatu kuwabaini waomba rushwa na kuchukulia hatua.

Mbungo alisema hayo jana wakati akifafanua hatua zinazochukuliwa dhidi ya baadhi askari wa barabarani wanaomba rushwa ya kati ya Sh 2,000 hadi Sh 10,000 kutoka kwa madereva, makondakta wa vyombo vya usafiri hususan mabasi ya abiria maarufu kama daladala na bajaji mkoani Dar es Salaam.

Hatua hiyo imekuja baada ya HabariLEO kufanya

uchunguzi na kubainika kuwa, imekuwa kawaida kwa baadhi ya askari hao kuchukua rushwa kwa kila gari la abiria na bajaj kila siku kwa nyakati tofauti.

“Ni kweli kuna rushwa ndogondogo zinachukuliwa na baadhi ya askari wa usalama barabarani, tunalifahamu na kusema kweli kulidhibiti ni ngumu, ila tulichofanya ni kuanzisha aplikasheni iitwayo utatu inayoshirikisha Takukuru, Jeshi la Polisi na wadau

wengine kwenye masuala ya usafiri na askari wanaomba rushwa wanaripotiwa kupitia mtandao na Jeshi la Polisi wanachukua hatua kwa mujibu wa sheria,” alisema Mbungo.

Alisema rushwa ndogondogo imekuwa ngumu kuidhibiti na kwamba njia sahihi inayotumika kwa sasa na taasisi hiyo na vyombo vingine vyenye mamlaka ni kuendelea kuelimisha na kuchukua hatua kwa wale wanaobainika kukuika

sheria kama kuwashusha vyeo, kuwapa onyo na pia kuwafukuza kazi pale inapobidi kufanya hivyo kwa sababu vitendo vya rushwa havikubaliki na ni kosa kisheria.

“Ipo mifano mingi ya askari wa usalama barabarani ambao wameshaadhibiwa kwa makosa ya rushwa, kuna askari kule Arusha alimuomba mama mmoja dereva rushwa ya ngono na uchunguzi ukafanywa na ikathibitika ni kweli kaomba, jeshi la polisi kwa kuwa ni chombo cha weledi na nidhamu kilimuwajibisha kwa kumfukuza kazi askari huyo,” alisema Mbungo.

Alisema makosa ya rushwa kwa askari wa usalama barabarani yamekuwa sugu kwa sababu wanapokea rushwa hiyo ndogondogo na kwamba kuidhibiti ni ngumu bila kuwashirikisha wadau wote.

“Kuna usemi unasema kama huwezi kupambana nae basi ungana nae na ndivyo tulivyofanya, tumeamua kuunganisha nguvu ya mapambano kwa kuwashirikisha na wao na wadau wengine na elimu ndio jambo la msingi, lakini pia tunawaambia wanaoombwa rushwa watoe taarifa kwenye aplikesheni hiyo ili tuwakamate waombaji na iwe fundisho, tumeanza kuona matokeo ila bado tunahitaji nguvu ya pamoja,” alisema Mbungo.

Chanzo: www.habarileo.co.tz