Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Takukuru yaeleza sababu ya kuchelewa kumchunguza aliyekuwa Mkurugenzi Mji Geita

Michuzi Ded Geita.png Takukuru yaeleza sababu ya kuchelewa kumchunguza aliyekuwa Mkurugenzi Mji Geita

Wed, 31 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Geita inaendelea kuchunguza safari ya China aliyokwenda aliyekuwa Mkurugenzi wa Mji wa Geita, Zahara Michuzi ambaye Desemba mwaka jana alihamishiwa Halmashauri ya Mji wa Ifakara.

Uchunguzi huo ulioanza mwanzoni mwa Novemba 2023 ulitokana na agizo la Mkuu wa Wilaya ya Geita, Cornel Magembe aliyelitoa mwishoni mwa Oktoba, 2023 la kuitaka taasisi hiyo kuchunguza safari ya Mkurugenzi aliyekwenda nchini China kama ilikuwa kwa masilahi ya halmashauri au binafsi.

Pia aliitaka taasisi hiyo kubaini kama matumizi ya safari hiyo yalitokana na fedha za halmashauri au binafsi na endapo watabaini alitumia fedha za Halmashauri zirejeshwe na zielekezwe kutekeleza miradi ya maendeleo.

Akizungumza Januari 30, 2024 Naibu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Geita, Azza Mtaita amesema uchunguzi huo umechukua muda mrefu kwa kuwa ni wa mtu mkubwa kwenye taasisi, lakini pia fedha zilizochukuliwa ni nyingi.

Kuhusu uhamisho wake kama unaathiri uchunguzi Mtaita amesema kuhamishwa kwake ni faida kwa timu ya uchunguzi kwa kuwa imewapa uhuru watumishi wanaopaswa kutoa ushahidi, na kuifanya Takukuru kufanya kazi kwa kina zaidi.

“Ni kweli uchunguzi umechukua muda mrefu kwa kuwa naye ni mkubwa na fedha alizochukua ni nyingi na kuna mambo ambayo tunatakiwa tuyahakikishe, ni bora kuchukua muda mrefu kupata matokeo chanya.

“Hata chakula kilichopikwa muda mrefu ladha yake ni tofauti na ile ya haraka unapoandaa kitu muda mrefu kinakuwa na matokeo mazuri,” amesema Mtaita.

Hata hivyo, amesema uchunguzi utakapokamilika utatolewa kama wanavyotoa taarifa nyingine walizozifanyia kazi.

Wakati huohuo, Takukuru mkoani hapa imebaini miradi minne ya maendeleo yenye thamani ya Sh1.5 bilioni ikiwa na viashiria vya ubadhilifu.

Miradi hiyo ni miongoni mwa 14 ya maendeleo yenye thamani ya Sh6.4 bilioni iliyokaguliwa na taasisi hiyo kwa kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2023.

Mtaita ametaja miradi iliyobainika kuwa na harufu ya ubadhilifu kuwa ni wa Shule ya Sekondari na Msingi za Nyantorotoro zinazojengwa kwa thamani ya zaidi ya Sh699 milioni.

Mradi mwingine ni ujenzi wa Shule ya Msingi Museveni iliyopo wilayani Chato inayojengwa kwa gharama ya Sh705 milioni pamoja na ujenzi wa kituo kikuu cha mabasi wilayani Nyang’hwale inayojengwa kwa gharama ya Sh114.7 milioni, ambayo ujenzi wake ni hafifu ikilinganishwa na orodha ya mahitaji na vifaa vya mradi (BOQ).

Katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2023 taasisi hiyo imepokea malalamiko 81 na kati ya hayo 53 sawa na asilimia 65.5 yalihusu makosa ya rushwa na tayari uchunguzi umeanza.

Amesema Serikali za Mitaa zinaongoza kwa malalamiko ambapo kati ya 81 yaliyopokelewa 34 ni kutoka Serikali za mitaa huku idara ya elimu ikifuatia kwa kuwa na malalamiko 14,afya 6,madini 6,ardhi matatu na taasisi nyingine zikiripotiwa mawili.

Mtaita amewatahadharisha wanasiasa wenye nia ya kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika mwaka huu na ule mkuu utakaofanyika 2025, kuacha kujipitisha kwa wananchi kwa kuwarubuni kwa rushwa ili wawaunge mkono.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live