Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Takukuru wamdaka aliyekuwa DED Rombo, kupanda kortini

37956 Pic+DED Takukuru wamdaka aliyekuwa DED Rombo, kupanda kortini

Wed, 23 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), inamshikilia aliyekuwa mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo, Judethadeus Mboya kwa tuhuma za matumizi mabaya ya ofisi.

Mkuu wa Takukuru mkoani Kilimanjaro, Holle Makungu alisema jana kuwa Mboya anatuhumiwa kutumia madaraka yake vibaya na kuisababishia hasara halmashauri hiyo ya Sh226.6 milioni.

Taarifa ya Takukuru iliyomkariri Makungu, inasema mkurugenzi huyo wa zamani anadaiwa kuwalipa fidia wananchi 25 waliotoa ardhi yao kwa mwekezaji.

Takukuru inadai kuwa fedha hizo za fidia zilipaswa kulipwa na kampuni ya uwekezaji ya China, Jun Yu Investment International iliyojenga kiwanda cha saruji cha Moshi eneo la Holili.

Makungu alisema katika taarifa yake kuwa mtuhumiwa huyo pamoja na wengine wanaochunguzwa, wanatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote kuanzia leo.

Ingawa Makungu hakueleza kwa kina, Februari 19, 2016, aliyekuwa mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Amos Makala aliiagiza Takukuru kuchunguza ulipaji huo wa fidia.

Angellah Kairuki, aliyekuwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi wakati huo, alinusa harufu ya ufisadi katika malipo hayo na kuagiza uchunguzi ufanyike.

Kairuki aliagiza uchunguzi huo baada ya kuelezwa katika kikao na watendaji wa mkoa kuwa Sh500 milioni zilizotolewa na mwekezaji kulipa fidia hiyo zilikuwa zimeingia katika mifuko ya watu binafsi.

Pia, Waziri Kivuli wa Ardhi wakati huo, Halima Mdee alilizungumzia suala hilo bungeni akimtuhumu aliyekuwa mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama kuwa na hisa 20,000 katika kiwanda hicho. Gama kwa sasa ni marehemu.

Hata hivyo, mkuu huyo wa mkoa aliwahi kuwaambia wanahabari kuwa hamiliki hisa, bali mwanaye anayeitwa Muyanga Gama ndiye mwenye hisa katika kiwanda hicho.

“Aliyetafuta eneo, aliyelipa fidia ni Halmashauri ya Rombo. Mimi kama RC sikuhusika na sina hata senti tano niliyopata katika shughuli hiyo,” alisema Gama katika mkutano aliouitisha wa waandishi wa habari kuzungumzia tuhuma hizo wakati wa uhai wake.

Alisema mtoto wake ni mtu mzima na hivyo ana haki ya kumiliki hisa kwa mujibu wa sheria.



Chanzo: mwananchi.co.tz