Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Takukuru kuwafikisha mahakamani wafanyabiashara, askari tuhuma za rushwa

89653 Takukuru+pic Takukuru kuwafikisha mahakamani wafanyabiashara, askari tuhuma za rushwa

Mon, 23 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) nchini Tanzania itawafikisha mahakamani watuhumiwa wanaokabiliwa na makosa mbalimbali leo Jumatatu Desemba 23, 2019 wakiwamo wafanyabiashara na askari polisi.

Mkuu wa Takukuru mkoa wa Arusha, Frida Wikesi amesema miongoni mwa watuhumiwa hao ni mfanyabiashara Shabir Mohamed Virjee, Mkenzi Mussa Pazi ambaye mfanyakazi wa kituo cha mafuta cha Oryx kilichopo eneo la Clock Tower jijini Arusha.

Mtuhumiwa mwingine ni aliyekua askari polisi wa usalama barabarani mwenye namba F8683 PC Paulo Edward Erasmo kwa kosa la kushawishi na kutaka kumhonga askari mwenzake Sh10 milioni kinyume na kifungu cha 15 cha Sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007.

"Takukuru ilipokea taarifa kutoka kwa askari polisi aliyeshawishiwa ikieleza kuwa Shabir Virjee ambaye ni baba wa mtuhumiwa ambaye suala lake linaendelea na uchunguzi wa polisi kuhusiana na uuzwaji wa  mafuta kinyume na matakwa ya leseni yao ya biashara na maelekezo ya Ewura alishawishi apokee rushwa ili amsaidie mwanaye," amesema Frida.

Amesema baada ya kupata taarifa hizo ilianzisha uchunguzi na kubaini Virjee alimtumia askari Paul Erasmo kumshawishi askari mwenzake apokee rushwa ili mtuhumiwa aliyekua mahabusu adhaminiwe na asiendelee kufuatilia tena suala lake hivyo kuandaa mtego uliofanikisha kuwanasa watuhumiwa wakiwa tayari wamekabidhi fedha hizo.

"Takukuru mkoa wa Arusha inatumia fursa hii kumpongeza sana askari huyo kwa kitendo chake cha kizalendo na ujasiri cha kukataa hongo hiyo na kulinda heshima ya Jeshi la Polisi," amesema Frida

Katika hatua nyingine, Takukuru itawafikisha mahakamani wafanyakazi wanne wa kampuni ya majengo ya uwakala wa utunzaji  mazingira ambao ni Oliver Shui, Abdul Hamisi, Rehema Adamu na Prosper Kahemele kwa tuhuma za kuomba rushwa ya Sh20,000.

Amesema mtoa taarifa ambaye walimtuhumu kwamba amechafua mazingira kwa kumwaga maji machafu mtaroni alipe kiasi hicho ili asiandikiwe faini ya Sh50,000 na baada ya kuwaona Takukuru walikataa kupokea fedha hizo.

Wakati huohuo, Takukuru wilaya ya Karatu itamfikisha mahakamani Daniel Gwandu Mathiya  aliyekua mtumishi wa kituo cha afya Karatu kwa kughushi nyaraka za ajira kwa kutumia vyeti vya Daniel Mathias Kirway na kupeleka kupata ajira kama Mtakwimu wakati hana sifa hizo.

Chanzo: mwananchi.co.tz