Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Takukuru ilivyotaifisha mabilioni ya shilingi, magari na nyumba

48675 Takukurupic

Tue, 26 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imerejesha zaidi ya Sh14.9 bilioni, kutaifisha nyumba saba na magari manne kutoka kwa mafisadi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne Machi 26, 2019  makao makuu ya taasisi hiyo,  Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Kamishna Diwani Athuman amesema kwa mujibu wa sheria mbalimbali, taasisi hiyo inaweza kutaifisha mali zilizopatikana kwa njia haramu ikiwamo ya rushwa.

“Kuanzia mwaka 2016 hadi sasa, Takukuru imefanikiwa kurejesha zaidi ya Sh14.9 bilioni na kutaifisha nyumba saba na magari manne kutoka kwa mafisadi,” amesema.

“Tumeweka zuio la mali ikiwamo akaunti za fedha zaidi ya Sh20 bilioni, nyumba 26, viwanja 47, magari 61 na mashamba 13.”

Amesema Takukuru ina mamlaka ya kufuata sheria ya kutafuta, kushikilia na kutaifisha mali kupitia tangazo la kutafutwa.

Mkurugenzi huyo amesema jana Jumatatu Machi 25, walitoa tangazo la kutafutwa kwa Magreth Kobelo Gonzaga katika vyombo na majukwaa mbalimbali ikiwamo gazeti la Mwananchi akituhumiwa kutakatisha fedha.

Amesema Magreth ni mkazi wa Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam ambaye anatuhumiwa kutakatisha fedha na kujipatia mali kupitia moja ya kampuni aliyokuwa akifanya kazi.

Diwani amesema wakati uchunguzi ukiendelea, Magreth alitoweka na kwamba kwa sasa wanamuhitaji mtuhumiwa huyo.

“Kutokana na sababu hiyo, Takukuru inapaswa kutangaza kutafutwa kwake, kabla ya kutaifisha mali zake,” amesema Diwani

Amesema katika uchunguzi walioufanya wamebainisha Magreth alitumia fedha hizo haramu kununua viwanja katika ufukwe wa Bahari ya Hindi pamoja na nyumba mbalimbali.

Mara baada ya kumaliza kuzungumza, Kamishna Diwani aliwapeleka waandishi wa habari kuwaonyesha moja ya nyumba ambazo zinamilikiwa na Magreth ambazo ziko hatarini kutaifishwa.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz