Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tabibu Msaidizi kortini kwa kupokea rushwa

C73937a3a4837b1e093d0d474e36b632 Tabibu Msaidizi kortini kwa kupokea rushwa

Tue, 28 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoa wa Rukwa imemshtaki Tabibu Msaidizi, Eliud Humbo wa Kituo cha Afya Matai wilayani Kalambo akidaiwa kuomba na kupokea rushwa ya Sh 100,000 kutoka mgonjwa aliyemfanyia upasuaji 'feki'.

Tabibu Msaidizi huyo ambaye hana utaalamu wa upasuaji kwa binadamu alimpasua tumbo mgonjwa huyo na kuuacha utumbo wake nje na kumsababishia maumivu makali mwilini.

Mgonjwa huyo alikuwa na rufaa kwenda Hospitali ya Mkoa Mjini Sumbawanga.

Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Rukwa, Hamza Mwenda aliwaeleza hayo waandishi wa habari mjini hapa wakati akitoa taarifa ya utendaji wa kazi wa Aprili hadi Juni 2020 wa taasisi hiyo.

Alisema kesi hiyo namba 66/2020 imefunguliwa Juni 26 Mahakama ya Wilaya ya Kalambo.

"Awali mgonjwa huyo alibainika kusumbuliwa na ugonjwa wa ngiri na madaktari walimpatia rufaa kwenda kutibiwa Hospitali ya Mkoa wa Rukwa iliyopo katika Mji wa Sumbawanga...

Wakati akijiandaa kutoka Kituo cha Afya Matai ili akatibiwe mjini Sumbawanga alikutana na Tabibu Msaidizi huyo (Humbo) aliyesema ana uwezo kumfanyia upasuaji na atapona na akamwomba ampatie Sh 100,000 kwa kazi hiyo, lakini siku hiyo hakuwa zamu kituoni,"alieleza.

Baada ya mtuhumiwa kupokea fedha hizo, inadaiwa alienda kwa Msimamizi wa Kitengo cha Tohara kwa wanaume akidai kuwa mgonjwa huyo alikuwa akihitaji kutahiriwa.

"Mtuhumiwa huyo alikabidhiwa vifaa vilivyohitajika kwa kumfanyia tohara mgonjwa wake lakini alimfanyia upasuaji wa ngiri kwa kumpasua tumbo lake akiwa hana utaalamu wa kumfanyia mgonjwa upasuaji wa aina yoyote.

Baada ya kufanyiwa upasuaji huo alilazwa wodini ambapo siku iliyofuata kidonda kilianza kuoza huku utumbo wake ukiwa nje na hali yake ilibadilika ghafla,"alieleza Mwenda.

Ilidaiwa daktari wa zamu alipomhoji ugonjwa unaomsumbua ndipo siri ilipofichuka na taarifa zake kufikishiwa Takukuru. “Tumemkamata mtuhumiwa na tumemfikisha mahakamani kwa kuomba na kupokea rushwa,"alisisitiza.

Aliongeza kuwa mgonjwa huyo alikimbizwa kwa matibabu Hospitali ya Mkoa wa Rukwa mjini hapa ambapo amefanyiwa marekebisho ya upasuaji 'feki' na amepona na kuruhusiwa.

Chanzo: habarileo.co.tz