Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TTCL yashinda kesi, ikiamriwa kumlipa mpangaji wake MMU

HUKUMU TTCL yashinda kesi, ikiamriwa kumlipa mpangaji wake MMU

Mon, 19 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mahakama Kuu Kanda ya Arusha imekiamuru Chuo Kikuu cha Mount Meru (MMU) kuilipa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) zaidi ya Sh362 milioni ambazo ni malimbikizo ya deni la kodi ya pango.

Hata hivyo, TTCL imeamriwa na Mahakama kukilipa chuo hicho fidia ya Sh10 milioni kama hasara ya jumla kutokana na kosa la kukifungia ofisi bila kukipatia taarifa ya siku 60 kwanza kama mkataba wa upangaji unavyoeleza.

Mahakama katika uamuzi wa Januari 29, mwaka huu imefikia uamuzi huo baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote, katika kesi ya msingi iliyofunguliwa na TTCL dhidi ya chuo hicho, pamoja na ushahidi wa madai kinzani ya chuo hicho dhidi ya TTCL kuhusu mgogoro huo kodi ya pango.

Chuo hicho kilikiuka mkataba wa upangaji ulioingiwa kati yao mwaka 2011, kwa kushindwa kulipa kodi ya pango ya majengo yake TTCL, ambayo chuo kiliyatumia kama ofisi na miundombinu ya kutolea huduma ya elimu ya juu, hususani kwa kwa wanafunzi wa Shahada ya Uzamili.

Majengo hayo ya TTCL yapo kiwanja namba 61 kitalu E Boma Road katikati ya jiji la Arusha.

Kwa mujibu wa mikataba iliyokuwa ikihuishwa kila baada ya miaka miwili, chuo kilipaswa kulipa kodi ya pango ya Dola za Marekani 78,960 kila mwaka bila Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).

Septemba Mosi, 2017, TTCL ilikitimua chuo hicho katika majengo yake kwa kufunga ofisi kutokana na kushindwa kulipa malimbikizo ya kodi ya pango kwa kipindi cha miaka mitano.

TTCL ilifungua kesi ya ardhi namba 25/2021, kwa kuvunja mkataba na kudai malipo ya deni la kodi ya pango pamoja na fidia.

Chuo kiliibua madai kinzani kikidai TTCL ilikiuka masharti ya makubaliano kwa kukifungia bila kuzingatia mkataba na kukisababishia hasara na kiliiomba Mahakama iamuru kilipwe fidia kwa hasara hiyo na gharama za kesi.

Kwa mujibu wa ushahidi uliowasilishwa mahakamani, TTCL ilikuwa ikikidai chuo hicho Dola 285,321.13 (Sh638.808 milioni wakati huo) ikiwa ni malimbikizo ya kodi kuanzia mwaka 2011 mpaka 2017.

Chuo katika ushahidi kupitia kwa mwenyekiti wake wa Bodi, Boniface Mwabukusi kilidai kuwa TTCL iliwafungia ofisi hizo bila kuwapatia taarifa na kwamba walipewa taarifa hiyo miezi tisa baadaye, Aprili 5, 2018.

Mwabukusi alidai kulingana na mkataba, mpangaji akishindwa kulipa kodi, mpangishaji alipaswa kutoa taarifa ya siku 60 lakini TTCL iliwafungia na bila kutoa taarifa hiyo na walikataa kujadiliana kupata upatanisho kuhusu deni halisi kwa kuwa kulikuwa na mkanganyiko wa kiasi halisi walichokuwa wanadaiwa.

"Mali zikiwemo samani na vifaa vya kielektroniki kama kompyuta, maktaba iliyokuwa ikitumiwa na wanafunzi na walimu na vifaa vingine na kuendelea kuvishikilia kwa takribani miaka mitano, hadi 2021 vilipoachiliwa," alidai Mwabukusi na kuongeza:

"Wakati tunakabidhiwa vitu hivyo, vitabu vilikuwa havifai tena kwa matumizi kwa kuwa vilikuwa vimeharibiwa kwa maji, kuliwa na panya, na vifaa vya kidijitali havikuwa vikifanya kazi tena kwa kuwa havikuweza kutoa taarifa zozote."

Alidai thamani ya uharibifu wa mali hizo ulikuwa si chini ya Sh100 milioni na hasara ya nyaraka muhimu kwa matumizi ya kiutawala, kuvuruga taratibu za uendeshaji chuo, na kutokana na kushindwa kuendesha chuo, Tume ya Vyuo Vikuu ilisimamisha kozi zote.

Alidai wakati wanafukuzwa katika majengo hayo walikuwa na wanafunzi 120 na kila mwanafunzi alikuwa analipa ada ya Sh5.6 milioni na kwamba wengi waliomba na kurejeshewa ada zao na hivyo walipoteza mapato ya ada za wanafunzi takribani Sh2.8 bilioni, kwa mwaka.

Mahakama katika uamuzi uliotolewa na Jaji Devotha Kamuzora, aliyeisikiliza, imeamua deni linalodaiwa na TTCL ni Sh362.594 milioni na si Sh638.898 milioni iliyodaiwa na TTCL.

Amesema kutokana na hakuna kiwango cha ubadilishaji fedha (Dola kuwa Shilingi) kwa kodi iliyolipwa au iliyotakiwa kulipwa kuanzia Januari 2015 mpaka Desemba 31, 2016, hivyo anakubaliana na mdaiwa (Chuo) kuwa madai ya TTCL si bayana, hivyo yanahitaji suluhisho la pamoja kwa pande zote.

Jaji Kamuzora alisema kifungu cha 4(iii) cha makubaliano ya upangaji, kinaeleza matokeo ya kutokutekeleza wajibu wa kimkataba, mpangaji akishindwa kulipa kodi kwa siku 30 mpangishaji atakuwa na haki ya kumuondoa.

Hivyo alisema kutokana na ushahidi uliowasilishwa na TTCL, amejiridhisha kuwa chuo kilikiuka mkataba kwa kushindwa kulipa kodi ya pango kwa wakati.

Hata hivyo, Jaji Kamuzora alisema kifungu cha 6 cha mkataba huo wa upangaji, kinaruhusu upande wowote kuvunja mkataba lakini pamoja na mambo mengine, baada ya kutoa taarifa ya miezi miwili.

Alisema ushahidi unaonyesha TTCL ilikifungia nje chuo hicho kabla ya kukipatia taarifa hiyo kwani ilikifungia Septemba Mosi, 2017 na taarifa ilitolewa Aprili 5, 2018 na mpangaji aliipata Aprili 12, 2018.

Hivyo alisema pande zote zilikiuka mkataba, chuo kwa kushindwa kulipa kodi kwa wakati, na TTCL kwa kukifungia nje isivyo halali bila kwanza kutoa taarifa kama ilivyoelezwa katika mkataba wa upangaji.

Alisema hakuna shaka kuwa TTCL ina madai halisi dhidi ya chuo, lakini haikuweza kuonyesha madhara iliyoyapata kama matokeo ya kuchelewa malipo ya kodi ya pango.

Alisema TTCL haiwezi kulipwa fidia ya madhara ya jumla kwa kuwa nayo ilikiuka mkataba upangaji kwa kushindwa kutoa taarifa kabla ya kumfungia nje mpangaji.

Licha ya TTCL kukiuka mkataba, chuo kimeshindwa kuthibitisha hasara halisi ya uharibifu wa vifaa vilivyokuwa vimefungiwa.

Alibainisha hakuna kumbukumbu kuonyesha wakati kinarejeshewa mali zake zilizokuwa zimefungiwa ndani, mwaka 2021, vitabu na nyaraka vilikuwa havifai kutumika kwa kuharibiwa na maji na kuliwa na panya na kompyuta kutotumika tena.

Jaji Kamuzora alisema chuo hicho hakikuweza kuthibitisha madai ya hasara ya kukosa mapato, kwani hakikuthibitisha idadi ya wanafunzi waliokuwepo, kama walikuwa wameshalipa ada, wala waliorejeshewa ada zao na kiasi kilichorejeshwa.

Hata hivyo, alisema anakubali kuwa kitendo cha TTCL kukifungia nje bila kukitaarifu kiliathirika, kwa usumbufu katika utoaji huduma yake.

“Kwa hiyo ninaona inafaa kwamba mdaiwa afidiwe Sh10 milioni, kama fidia ya hasara ya jumla,” amesema Jaji Kamuzora.

Alisema Chuo kitailipa TTCL Sh352.594 milioni baada ya kutoa Sh10 milioni ambayo kimepewa kama malipo ya hasara ya jumla kwa kitendo cha TTCL kukifungia nje bila taarifa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live