Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

THUB yajitosa mauaji ya Polisi Kilimanjaro

Mauaji Pic Data Polisiiii THUB yajitosa mauaji ya Polisi Kilimanjaro

Wed, 16 Mar 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Mauaji ya askari wa upelelezi wilayani Mwanga, Linus Nzema bado ngoma nzito hivi ndivyo unavyoweza kusema, baada ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THUB) kuanza kuchunguza upya mauaji hayo

Mkurugenzi msaidizi wa kitengo cha mawasiliano Joseph Germanus alisema jana kuwa; “Ni kweli kuna timu ilitumwa kufuatilia suala hilo.”

Alipoulizwa iwapo uchunguzi huo unalenga kuanzisha upya kesi hiyo, alisema itategemea matokeo yatakavyokuwa na kwamba kazi yao ni kuishauri Serikali, itakavyoona itachukua hatua.

“Kuna sehemu ya matokeo tutayatoa kwa umma kama ilivyokuwa kwa tukio la Mwangosi (Daudi), na mengine tutawapa wahusika kwenye uchunguzi,” alisema.

Taarifa zilizolifikia gazeti hili wiki iliyopita zilidokeza tume hiyo ilianza uchunguzi na tayari watu kadhaa wamehojiwa wakiwamo maofisa wa Jeshi la Polisi na wananchi wa kijiji cha Kituri zaidi ya sita walioshuhudia mauaji hayo.

“Baada ya ndugu wa marehemu kulalamika inakuwaje ndugu yao ameuawa na waliohusika wanajulikana wasichukuliwe hatua kana kwamba aliyeuawa ni mbwa hapo nafikiri iliiamsha tume,” kilidokeza chanzo chetu.

“Lakini hata ile kauli ya Rais (Samia Suluhu) ya kuwa si sawa polisi wafanye mauaji halafu wajichunguze wenyewe nayo inaweza kuwa ndio sababu ila kiukweli sifahamu ni msukumo wa Rais au tume yenyewe,” kilisisitiza chanzo hicho.

Alipoulizwa mjomba wa marehemu, Atilio Kalinga kama anafahamu uwapo wa tume hiyo Kilimanjaro alijibu; “Nimeambiwa kuna tume imeundwa iko huko, lakini wameona nini kwa kweli na sisi tunasubiria.”

Mwenyekiti wa Kijiji cha Kituri kulipotokea mauaji hayo, Thomas Mgala alipohojiwa alikiri kuwa miongoni mwa waliohojiwa na tume, lakini akakataa kueleza alichohojiwa.

Mmoja wa mashuhuda wa mauaji hayo ambaye ni miongoni mwa waliohojiwa alisema ametoa ushirikiano unaotakiwa kwa kueleza hatua kwa hatua kile alichokiona.

SOMA: DPP: Ushahidi ulikuwa dhaifu mauaji ya askari

Polisi huyo aliuawa kwa kupigwa risasi na askari mwenzake Mei 31 mwaka jana nje ya baa ya Ndafu iliyopo kijiji cha Kituri, Wilaya ya Mwanga, wakati polisi hao wakijiandaa kurejea kituoni baada ya kumaliza operesheni ya kusaka mirungi. Hata hivyo, uongozi wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Mwanga na makao makuu Mkoa wa Kilimanjaro wanadaiwa kula njama kuficha mauaji hayo na kudai yalitokana na kugongwa na pikipiki ya genge la wasafirishaji wa mirungi.

Gazeti hili ndio lilifichua ukweli wa mauaji hayo baada ya kufika eneo la tukio na kuzungumza na mashuhuda ambao walidai kumuoana askari akienda kuchukua bunduki kwenye gari na kumfyatulia risasi mwenzake.

SOMA: Agizo la Rais Samia lazua kilio upya

Taarifa ilimfanya mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Camilius Wambura kuunda timu ya makachero kutoka ofisini kwake kwenda Kilimanjaro kuchunguza tukio hilo na kubaini ukweli tofauti na taarifa ya awali ya polisi.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz